Kauli Za Maimaam Wanne Kuhusu Kushikamana Na Sunnah Na Kuacha Kufuata Rai Zao

 

Kauli Za Maimaam Wanne Kuhusu Kushikamana

Na Sunnah Na Kuacha Kufuata Rai Zao

 

Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy 

 

Imefasiriwa na 'Abu 'Abdillaah kutoka kitabu cha: 'Swiffatus-Swalaatin-Nabiy (Sifa ya Swalah ya Nabiy صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّم) kilichoandikwa na Shaykh Al-Albaaniy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Itakuwa ni manufaa makubwa ikiwa tutazieleza baadhi ya kauli zao hapa, kwani labda hii itamuonya mtu au itawakumbusha wale ambao wanafuata rai za Imaam au madhehebu maalum, bali wanaofuata kwa upofu wale Waalimu au Mashaykh na wale walio chini ya daraja ya hao Imaam wanne wakubwa[1] wakishikilia madhehebu yao au rai zao kama kwamba zimeteremeshwa kutoka mbinguni! Na hali Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

 اتَّبِعُواْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلاَ تَتَّبِعُواْ مِن دُونِهِ أَوْلِيَاء﴿٣﴾

Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Rabb wenu na wala msifuate badala Yake marafiki walinzi. [Al- A’raaf: 3]

  

 

Wasemavyo Imaam

 

 

 

1.    Abu Haniyfah (Rahimahu Allaah) 

 

 

Wa kwanza wao ni Abu Haniyfah Nu'maan bin Thaabit.

 

Wafuasi wake wamesimulia kauli zake mbali mbali pamoja na maonyo tofauti ambayo yote lengo lake ni moja, nalo ni: Wajibu wa kuikubali Hadiyth na kuachilia mbali kufuata rai za Imaam ambazo zinakhitilafiana nayo.

 

a. "Ikiwa Hadiyth imeonekana kuwa ni sahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu"[2]    

 

b. "Hairuhusiwi[3] kwa mtu yeyote kukubali rai zetu ikiwa pindi hawatojua wamezipata kutoka wapi"[4]     

Katika usimulizi mwengine:"Imekatazwa[5] mtu ambaye hajui dalili zangu kutoa hukmu[6]  kutokana na maneno yangu".

 

 

Usimulizi mwengine imeongezwa: "…Kwani sisi ni wanaadamu, tunasema jambo siku moja na kulirudisha (kulikataa) siku ya pili yake".

 

Na katika usimulizi mwengine: "Ole Ee Ya'quub![7]  Usiandike kila kitu unachosikia kutoka kwangu kwani huwa natoa rai moja leo na kesho huikataa. Au hutoa rai moja kesho na kuikataa keshokutwa".[8]   

 

 

c. "Ninaposema jambo linalokhitilafiana na kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) au yaliyosimuliwa na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi mpuuze usemi wangu".[9]     

 

 

   

  

2.   Maalik Ibn Anas (Rahimahu Allaah) 

 

Imaam Maalik bin Anas yeye amesema:

 

a. "Hakika mimi ni mwanaadamu: Ninafanya makosa (mara nyingine) na ninakuwa sahihi (mara nyingine). Kwa hiyo, tazameni rai zangu: zote ambazo zinakubaliana na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, zikubalini; na zote ambazo hazikubaliani na Kitabu (Qur-aan) na Sunnah, basi zipuuzeni". [10]

   

b. "Kila mmoja baada ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), atakuwa na kauli yake itakayokubaliwa na kukataliwa, isipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)"[11]   

 

 

 c. Ibn Wahb amesema: "Nilimsikia Maalik akiulizwa kuhusu takhliyl ya vidole vya miguu (kuvichanganua vidole ili kupitisha maji) wakati wa wudhuu. Akasema: "Watu si lazima kufanya hivyo". Sikumkaribia hadi zogo la watu lilipopunguka. Nilipomwambia: "Tunajua kuwa ni Sunnah kuhusu jambo hilo". Akasema: "Jambo gani hilo? Nikasema: "Laith ibn Sa'd, ibn Lahiy'a na 'Amr ibn Al-Haarith wamesimulia kwetu kutoka kwa Mustawrid bin Shaddaad Al-Quraishiy ambaye amesema: "Nilimuoma Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akisugua baina ya vidole vyake vya miguu kwa kidole change kidogo". Akasema: "Hadiyth hii ni hasan (njema); sikuwahi kuisikia abadan ila leo". Kisha baadaye nikamsikia akiulizwa kuhusu jambo hili hili, naye akaamrisha kufanya takhliyl ya vidole vya miguu"[12]

 

 

 

3.   Ash-shaafi'iy (Rahimahu Allaah)

 

Ama kutoka kwa Imaam Ash-Shaafi'iy, kauli zake zilizonukuliwa ni nyingi na nzuri mno.[13] na wafuasi wake walikuwa ni bora kabisa katika kufuata.

 

a.  "Sunnah za Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) zinamfikia na kumkwepa kila mmoja wetu. Kwa hiyo kila ninapotaja rai yangu au nikiunda sheria, na ikiwa ipo dalili kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), inayopinga rai yangu, basi rai iliyo sahihi ni aliyosema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hiyo ndio rai yangu"[14]  

 

 

b. "Waislamu wamekubaliana pamoja kwamba ikiwa Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) imebainishwa dhahiri kwa yeyote, hairuhusiwi[15]  kwake kuiacha kwa kufuata kauli ya mwengine yeyote”[16] 

 

 

c.   "Ukiona katika maandishi yangu jambo ambalo ni tofauti na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi zungumza kwa kurejea Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na acha niliyoyasema mimi".

 

Katika usimulizi mwengine: "…basi ifuate (Sunnah) na usitazame tena pembeni kufuata kauli ya mwengine yeyote"[17]    

 

 

d.   Hadiyth ikipatikana kuwa ni sahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu"[18]  

 

 

e.    "Wewe (Imaam Ahmad)[19] ni mwenye elimu zaidi kuhusu Hadiyth kuliko mimi. Kwa hiyo Hadiyth ikiwa ni sahiyh basi nijulishe, ikiwa ni kutoka Kufah, Basrah au Syria, ili nichukue rai ya Hadiyth madamu tu ni sahiyh"[20]

 

 

f.  "Katika kila jambo, ambako wenye kusimulia wakipata ripoti kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambayo ni kinyume na niliyoyasema, basi narudisha usemi wangu nyuma, ikiwa wakati wa maisha yangu au hata baada ya kufa kwangu"[21]  

 

 

g. "Ukinisikia nasema kitu, na kinyume yake ni Hadityh Sahiyh kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi tambua kuwa akili yangu imetoweka"[22]  

 

 

h. "Kwa kila ninalosema, ikiwa upo usimulizi ulio Sahiyh, basi Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) inakuja mwanzo, kwa hiyo usifuate rai yangu"[23]   

 

i.   "Kila kauli kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni rai yangu pia, japokuwa hujaisikia kutoka kwangu"[24]  

 

 

 

 

4.   Ahmad Bin Hanbal (Rahimahu Allaah) 

 

Imaam Ahmad alikuwa wa mbele miongoni mwa Imaam kukusanya Sunnah na kuzishikilia sana hadi alichukizwa kuona kitabu kilichokuwa na yaliyegeuzwa na rai kiandikwe[25] kwa sababu hii akasema:   

 

a.  Msifuate rai yangu,wala msifuate rai ya Maalik, au Ash-Shaafi'iy au ya Awzaa’iy, wala Ath-Thawriy, lakini chukueni kutoka walikotoa"[26]

 

Katika usimulizi mmoja: "Msiige dini yenu kutoka kwa mtu yeyote katika hawa, bali chochote kilichotoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake, chukueni, kisha kwa At-Taabi'iyn (Waliofuata) ambako mtu ana khiari".

 

Kuna wakati akasema: "Kufuata[27] ina maana kwamba mtu anafuata yaliyokuja kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake, baada ya At-Taabi'iyn (Waliofuata) anayo khiari" [28] 

 

 

b.  "Rai ya Al-Awzaaiy, rai ya Maalik, rai ya Abu Haniyfah, zote ni rai, na ni sawa katika macho yangu. Lakini, dalili ni yale masimulizi kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake"[29] 

 

 

c.   "Yeyote atakayekanusha kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) basi yumo katika ukingo wa kuangamia"[30]           

 

Hizi ndizo kauli za wazi kabisa za Imaam (Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa Awe radhi nao), kuhusu kushikamana na Hadiyth na kukataza kufuata rai zao bila ya kuwa na dalili iliyo dhahiri kabisa.

 

Kwa hiyo, yeyote aliyeshikamana na lolote la Sunnah ambayo imeshuhudiwa kuwa ni Sahiyh hata kama imepinga kauli ya baadhi ya Imaam, hatokuwa anapingana na madhehebu yao, wala hatopotoka katika njia zao, bali mtu huyo atakuwa anawafuata wote na atakuwa amekamata kile kilichoaminiwa zaidi akishika mkono ambao hautavunjika. Lakini hii haitakuwa hali ya yule anayeziweka kando Sunnah Sahiyh kwa sababu tu zimepingana na rai za Imaam, bali mtu huyo atakuwa sio mtiifu kwao na amepingia kauli zao hizo za juu.  Na tunaona Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

فَلاَ وَرَبِّكَ لاَ يُؤْمِنُونَ حَتَّىَ يُحَكِّمُوكَ فِيمَا شَجَرَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ لاَ يَجِدُواْ فِي أَنفُسِهِمْ حَرَجًا مِّمَّا قَضَيْتَ وَيُسَلِّمُواْ تَسْلِيمًا

Basi Naapa kwa Rabb wako, hawatoamini mpaka wakufanye wewe ni mwamuzi katika yale wanayozozana baina yao, kisha wasipate katika nyoyo zao karaha katika yale uliyohukumu na wajisalimishe, kwa kujisalimisha kikamilifu. [ An-Nisaa: 65]

 

Pia Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

Basi watahadhari wale wanaokhalifu amri yake, isije kuwasibu fitnah au ikawasibu adhabu iumizayo.  [An-Nuwr: 63]

 

Kwa vile hii ni uthibitishaji kuwa kwa nini Abu Haniyfah mara nyingine alikhitilafiana na Hadiyth zilizokuwa Sahiyh bila ya kukusudia na ni sababu barabara ya kukubaliwa, kwani Allaah Haikalifishi nafsi kwa yale isiyoweza kubeba. Hairuhusiwi kumtukana kwa sababu hiyo kama walivyofanya watu wajinga. Bali ni wajibu kumheshimu, kwani yeye ni mmoja wa Imaam wa Waislamu ambao wameihifadhi hii dini hadi ikafikishwa kwetu kutoka katika kila matawi yake. Na kwa vile yeye analipwa Na (Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa hali yoyote ile; ikiwa ni Sahiyh au amekosea. Wala hairuhusiwi kwa wafuasi wake wapenzi kuendelea kushikilia kauli zake ambazo zinakhitilafiana na Hadiyth zilizo Sahiyh kwani kauli hizo sio madhehebu yake kama kauli zake hapo juu zilivyosema. Kwa hiyo hii ni mipaka miwili; ukweli na uongo katika yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) anasema katika Qur-aan yake tukufu:

 

وَالَّذِينَ جَاءُوا مِن بَعْدِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ

Na wale waliokuja baada yao wanasema: Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr: 10]

 

  

 

 

 

 

[1] Hii ni aina ya taqliyd (kufuata kwa upofu [kiujinga]) ambayo Imaam At-Twahaawiy alihusisha aliposema: "Hafuati rai ila ni mtu mkaidi au mjinga" (kufuata kama kipofu)

 

 

[2]  Ibnul-'Aabidiyn katika al-Haashiyah (1/63) na katika inshaa yake   Rasm al-Mufti (1/4 kutoka Mkusanyiko wa Inshaa za Ibnul-'Aabidyin). Shaykh Swaalih Al-Fulaaniy katika al-Iyqaadhw al-Himaam (uk.62) na wengineo. Ibnul-'Aabidiyn amenukuu kutoka Sharh al-Hidaayah ya Ibn Al-Shahnah Al-Kabiyr, mwalimu wa Ibn Al-Himaam, kama ifuatavyo:

"Ikiwa Hadiyth iliyo kinyume na Madhehebu imeonekana kuwa ni sahiyh basi mtu atende kwa kufuata hiyo Hadiyth na aifanye kuwa ni madhehebu yake. Kuifanyia kazi Hadiyth hakutombatilisha mtu kuwa sio mfuataji wa madhehebu ya Hanafi, kwani imeripotiwa kuwa Abu Haniyfah alisema: "Ikiwa Hadiyth imeonekana kuwa ni sahiyh, basi hiyo ndiyo madhehebu yangu". Na hii imeelezewa na Imaam Ibn 'Abdul-Barr kutoka kwa Abu Haniyfah na kutoka kwa Maimaam wengine".

Hii ni sehemu ya ukamilifu wa elimu na uchaji Allaah wa Maimaam, kwani wameonyesha kwa kusema kwamba wao hawakuwa na maarifa  (elimu) kamili ya Sunnah zote. Na Imaam Ash-Shaafi'iy amefafanua wazi wazi (tazama mbele). Hutokea wanapokwenda kinyume na Sunnah huwa ni kwa sababu hawakuitambua. Ndipo walipotuamrisha tushikilie Sunnah na tuizingatie kuwa ni sehemu ya madhehebu yao. Allaah Awashushie Rahma Yake kwao wote.

 

 

 

[3]   Si halaal

 

 

 

[4] Ibn 'Abdul-Barr katika Al-Intiqaa' fiy Fadhwaail Ath-Thalaathah Al-Aimmah Al-Fuqahaa (uk.145), Ibn Al-Qayyim katika 'I'laam Al Muqi'iyn (2/309), ibn 'Aabidiyn katika tanbihi zake kwenye Al-Bahr Ar-Raa'iq (6/293) na katika Rasm Al-Mufti (uk. 29,32) na Sha'raaniy katika Al-Miyzaan (1/55) pamoja na usimulizi wa pili. Usimulizi wa mwisho ulikusanywa na 'Abbaas Ad-Dawriy katika At-Taariykh ya Ibn Ma'iyn (6/77/1) ikiwa na isnaad sahiyh kutoka kwa Zafar, mwanafunzi wa Imaam Abu Haniyfah. Usimulizi uliofanana upo kutoka kwa wafuasi wa Abu Haniyfah; Zafar, Abu Yuusuf na 'Aafiyah bin Yaziyd; taz. Al-Iyqaadhw (uk.52). Ibn Al-Qayyim alithibitisha kwa nguvu usahihi wake kutoka kwa Abu Yuusuf katika I'laam Al-Muwaqi'yn (2/344). Nyongeza ya usimulizi wa pili unarejewa na mwandishi wa Al-Iyqaadhw (uk. 65) kwa Ibn 'Abdul-Barr, ibn Al-Qayyim na wengineo.

      Ikiwa hivi ndivyo wanavyosema kwa mtu asiyejua dalili zao, jibu lao litakuwa nini kwa yule anayetambua kuwa dalili zinapingana na kauli yao, lakini bado anatoa hukumu iliyopinga dalili? Kwa hiyo, fuata usemi huu, kwani pekee unatosheleza kuvunja ufuataji rai kwa ujinga. Ndio maana nilipomlaumu mmoja wa Mashaykh (Muqallid) wa madhehebu katika kutoa fatwa (hukm) kwa kutumia maneno ya Abu Haniyfah bila ya kujua dalili, aligoma kuamini kuwa huo ni kauli ya Abu Haniyfah!

 

 

[5] Haraam

 

 

[6] Mwanafunzi mashuhuri wa Imaam Abu Haniyfah, Abu Yuusuf (Rahimahu-Llaah)

 

 

[7] Fatwa

 

 

[8] Hii ni kwa sababu Imaam kawaida hutoa rai yake kutokana na Qiyaas (analogia). Kisha tena hupata analogia iliyo na nguvu zaidi, au Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) humfikia. Kwa hiyo huikubali hiyo na kuipuuza rai yake ya nyuma. Maneno ya Sha'araaniy katika Al-Miyzaan (1/62) yamewekwa kwa mukhtasari kama ifuatavyo:

     "Imani yetu na ya kila mtafiti wa Imaam Abu Haniyfah (Rahimahu-Llaah) ni kwamba, aliishi hadi iliporikodiwa Sharia. Na safari za wahifadhi wa Hadiyth katika miji mbali mbali na mipakani kwa ajili ya kukusanya na kuzipata. Angeliipokea na kupuuza analogia zote ambazo alizozitumia, idadi za qiyaas katika madhehebu yake zingelikuwa kidogo kama zilivyo katika madhehebu mengine. Lakini kwa vile dalili za Sharia zimetapakaa kwa Waliotangulia na waliowatangulia, na haizikukusanywa wakati wa maisha yake, ilihitajika kuwepo qiyaas nyingi katika madhehebu yake kulingana na Imaam wengine. ‘Ulamaa wa baada ya hapo, kisha wakafanya safari kutafuta na kukusanya Hadiyth kutoka nchi mbali mbali na miji na wakaziandika. Hivyo baadhi ya Hadiyth za Sharia zimeelezea nyingine. Hii ni sababu ya kuweko idadi kubwa ya qiyaas katika madhehebu yake wakati kwenye madhehebu mengine ilikuwa ni idadi ndogo"

     Abul-Hasanaat Al-Luknawi amenukuu maneno yake kikamilifu katika An-Naafi' Al-Kabiyr (uk.135) akiandika na kupanua tanbihi zake. Kwa hiyo yeyote anayependa kutafuta maelekezo yake afanye humo.

 

 

 

[9][9] Al-Fulaaniy katika Al-Iyqaadhw Al-Himaam (uk.50), ikifuatilia kwa Imaam Muhammad na kisha kusema: "Hii haimhusu mujtahid, (mwenye kujitahidi kwa elimu yake na kutoa hukmu) kwa vile hakujifunga katika rai zao, bali inamhusu muqallid (mwenye kufuata).

 

 

[10] Ibn 'Abdul Barr katika Jaami'ul Bayaan Al'Ilm (2/32), ibn Hazm   akinukuu kutoka kwake katika Usuul-Al-Ahkaam (6/149) na hali kadhaalika Al-Fulaaniy (uk. 72).

 

 

[11] Hii inajulikana sana miongoni mwa Maulamaa wa baadaye kuwa ni kauli ya Maalik. Ibn 'Abdul-Haadi alikiri kuwa ni Sahiyh katika Irshaad As-Saalik (227/1); Ibn 'Abdul Barr katika Jaami'ul-Bayaan Al-'Ilm (2/91) na Ibn Hazm katika Usuul Al-Ahkaam (6/145, 179) alisimulia kama ni kauli ya Al-Hakam ibn 'Utaybah na Mujaahid; Taqid-Diyn As-Subki alisimulia  katika Al-Fataawa (1/148) kama ni kauli ya Ibn 'Abbaas akishangazwa kwa uzuri wake kisha akasema: "Haya maneno yameanzia kwa Ibn 'Abbaas na Mujaahid, na Maalik (Rahimahu-Allaah) aliyachukua, na akawa mashuhuri kwayo". Inavyoelekea kwamba Imaam Ahmad kisha akachukua kauli hii kutoka kwao, kama Abu Daawuud alivyosema katika Masaaiil ya Imaam Ahmad (uk 276). "Nilimisikia Ahmad akisema: Kila mmoja anapokelewa na anakatiliwa katika rai zake, isipokuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)"

 

 

[12] Kutoka kwa Utangulizi wa Al-Jarh wat-Ta'diyl ya Ibn Abi Haatim (uk.      31-32)

 

 

[13] Ibn Hazm anasema katika Usuul al-Ahkaam (6/118)

"Hakika, Mafuqahaa wote ambao rai zao zilikuwa zikifuatwa zilipingwa kwa taqliyd na waliwakataza wafuasi wao kufuata rai zao kijinga. Aliyekuwa mkali kabisa miongoni mwao ni Ash-Shaafi'iy (Rahimahu-Allaah), kwani yeye alirudia kutilia mkazo zaidi kuliko yeyote mwengine kufuata usimulizi ulio Sahiyh na kukubali dalili yoyote iliyoamriwa. Vile vile alidhihirisha wazi na kujitenga kuwa hana hatia ikiwa atafuatwa yeye tu pekee na aliwatangazia hayo wale waliokuwa naye. Tunaomba hii imnufaishe mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) na thawabu zake ziwe za juu kabisa kwani alikuwa ni sababu ya mema mengi".

 

 

 

[14]   Imesimuliwa na Al-Haakim ikiwa ina isnaad ya kuendelea hadi kwa Ash-Shaafi'iy kama ilivyo katika Taariykh Dimashq ya Ibn 'Asaakir (15/1/3), I'laam Al-Muwaqi'yn (2/363,364) na Al-Iyqaadhw (uk. 100)

 

[15] Halaal

 

 

[16] Ibn al-Qayyim (2/361) na Al-Fulaaniy (uk. 68)

 

 

[17] Al-Haraawiy katika Dhamm Al-Kalaam (3/47/1) Al-Khatiyb katika Al-Ihtijaaj bi Ash-Shaafi'iy (8/2), Ibn 'Asaakir (15/9/10), An-Nawawiy katika Al-Majmuu' (1/63), Ibn al-Qayyim (2/361), na Fulaani (uk 100) usimulizi wa pili ni kutoka Hilyah Al-Awliyaa ya Abu Nu'aym.

 

 

[18] An-Nawawiy katika Al-Majmuu' (1/63), Sha'raaniy (1/57), akitoa chanzo chake kama Al-Haakim na Al-Bayhaqiy na Al-Fulaaniy (uk. 107). Ash-Sha'raaniy kasema: "Ibn Hazm kasema: "Kwamba imeonekana ni sahiyh naye au kwa Imaam mwengine". Kauli yake nyingine imethibitisha ufahamu huu.

An-Nawawiy amesema: "Wafuasi wetu walitenda kutokana na hili katika mambo ya tathwiyb (mwito wa Swalah baada ya adhana), shuruti za kutoka katika ihraam kwa ajili ya ugonjwa, na mambo mengine yaliyojulikana vyema katika vitabu vya madhehebu. Miongoni wafuasi wetu ambao wameripotiwa kuwa walitoa hukumu kutokana na chanzo cha Hadiyth (yaani kuliko kuchukua kauli ya Ash-Shaafi'iy) ni Abu Ya'quub Al Buwiity na Abul-Qaasim Ad-Daariki. Wafuasi wa Muhaddithiyn (Wakusanyao Hadiyth), Imaam Abu Bakr Al-Bayhaqi na wengineo walitenda kwa kufuata kauli hii. Wafuasi wengi wetu wa zamani, walipokumbana na jambo ambalo ilikuweko Hadiyth na madhehebu ya Ash-Shaafi'iy yalikuwa ni kinyume nalo, basi walitenda kwa kufuta Hadiyth na kutowa fatwa (hukmu) pia wakisema: "Madhehebu ya Ash-Shaafi'iy ni kila kinachokubaliana na Hadiyth". Shaykh Abu 'Amr (Ibn As-Swalaah) alisema: "Yeyote miongoni mwa Ash-Shaafi'iy akiona Hadiyth inayopinga madhehebu yake, alichukulia kama alitimiza shuruti za ijtihaad kwa kawaida, au katika maudhui au jambo lile khaswa ambalo alikuwa huru kutenda kwa kufuata Hadiyth; kama sio. Lakini hata hivyo aliona vigumu kupingana na Hadiyth baada ya utafiti zaidi, hakuweza kupata uthibitishaji wa kukinaisha wa kupinga Hadiyth. Kwa hiyo, alibakia kutenda kwa kufuata Hadiyth ikiwa Imaam mwingine mwenye kujitegemea mbali na Ash-Shaafi'iy, basi alitenda kuifuata. Na hii huwa ni kithibitisho chake cha kuacha madhehebu ya Imaam wake katika jambo hilo". Alichosema (Abu 'Amr) ni Sahiyh na lililokubalika. Na Allaah Anajua zaidi.

Kuna uwezekano mwingine ambao Ibn As-Swalaah alisahau kutaja: Afanyeje mtu ikiwa hakumpata mtu yeyote ambaye alitenda kwa kufuata Hadiyth? Hii imejibiwa na Taqiud-Diyn As-Subkiy katika makala yake 'Maana Ya Kauli ya Ash-Shaafi'iy: Ikiwa Hadiyth ikipatikana kuwa ni sahiyh, basi ndio madhehebu yangu' (uk.102, Mjalada 3). "Kwangu, lililo bora kabisa ni kufuata Hadiyth. Mtu na awaze kwamba yuko mbele ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kama vile ameisikia kutoka kwake, je, atakwenda demani (kufuata mweleko wa upepo) acheleweshe kutenda kwa kuifuata? Hapana! Wa-Allaahi, na kila mmoja anabeba jukumu kutokana na ufahamu wake".

Mjadala wake uliobakia umetolewa kuchambuliwa  katika I'laam Al-Muwaqi'iyn (2/303,370)  na katika kitabu cha Al-Fulaaniy, (Kichwa cha habari kamili) Al-Iyqadhw Himam Uul Al-Abswaar, lil-iqtidaa bisayyid Al-Muhaajiriyn wal-Answaar, wa Tahdhiyrihim 'an Al-Ibitidaa' Ash-Shaai' fit-Quraa wal-Amswaar, min taqlyid Al-Madhaahib ma'a Al-Hamiyyat Wal-'Aswabiyyat Bayna Fuqahaa Al-A'swaar"

Kitabu hicho ni cha pekee katika maduhui hii, ambacho kila mpenda haki akisome kwa ufahamu na kutafakari.

 

 

[19] Akimwambia Imaam Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah)

 

 

[20] Imesimuliwa na Ibn Abi Haatim katika Aadaabu Ash-Shaafi'iy (uk.94-5), Abu Nu'aym katika Hulya Al Awliyaa (9/106), Al-Khatiyb katika Al-Ihtijaaj bish-Shaafi’iy (8/1) na kutoka kwake Ibn 'Asaakir (15/9/1), Ibn 'Abdul-Barr katika Al-Intiqaa' (uk.75), Ibn Al-Jawziy katika Manaaqib Al-Imaam Ahmad (uk.499) na Haraawiy (2/47/2) katika njia tatu kutoka kwa 'Abdullaah bin Ahmad bin Hanbal kutoka kwa baba yake kwamba Ash-Shaafi'iy alimhusisha nayo katika I'laam (2/325) kama alivyofanya Al-Fulaaniy katika Al-Iyqaadhw (uk.152) na kisha akasema: "Al-Baihaqy amesema: "Hii ndio maana yeye, yaani Ash-Shaafi'iy alitumia Hadiyth sana, kwa sababu alikusanya elimu kutoka kwa watu wa Hijaaz, Syria, Yemen na Iraq. Kwa hiyo alikubali yote aliyoona kuwa ni sahiyh bila ya kutegemea au kuangalia yale yaliyokuwa nje ya madhehebu ya watu wa nchi yake,wakati ukweli ulipodhihirika kwake kutoka sehemu nyingine. Wengineo kabla yake, walijiwekea mipaka kwa waliyoyakuta katika madhehebu ya watu wa nchi yao bila ya kujaribu kuhakikisha usahihi wa yale yaliyokuwa kinyume nayo. Allaah Atusamehe sote"   

 

 

[21] Abu Nu'aym (9/107), Harawiy (47/1), Ibn al-Qayyim katika I'laam Al-Muwaqqi'iyn (2/363) na Fulaani (uk. 104)

 

 

[22] Ibn Haatim katika Al-Adaab (Uk. 93), Abul-Qaasim Samarqandi katika Al-Amaali, kama katika uchaguzi kutoka kwa Abu Hafsw al-Mu'addab (234/1), Abu Nu'aym (9/106), na Ibn 'Asaakir (15/10/1) ikiwa ni sanad sahiyh.

 

[23] Ibn Abi Haatim, Abu Nu'aym na Ibn 'Asaakir (15/9/2)

 

 

[24] Ibn Abi Haatim (uk 93-4)

 

 

[25]Ibn Al-Jawziy katika Al-Manaaqib (Uk. 192)

 

 

[26] Al-Fulaaniy (uk.113) na Ibn Al-Qayyim katika I'laam

 

 

[27] Ittibaa'

 

 

[28] Abu Daawuud katika Masaail ya Imam Ahmad (Uk 276-7)

 

 

[29] Ibn 'Abdul-Barr katika Jaami' Bayaan Al-'Ilm

 

 

 

[30] Ibn Al-Jawziy (uk 182)

 

 

 

Share