Mama Yangu Hamtaki Mume Wangu Kwa Sababu Alikuwa Mtumishi Wetu

 

SWALI:

Aslam aleykum

Mimi niliolewa mara ya kwanza na binamu yangu, haikufika muda tukaachana, nikaja  kupata mchumba  ambae alikuwa ni mfanyakazi wa mama yangu, mama akakataa mimi niolewe na huyo mvulana,upande wa baba wakaniozesha, mama akaniambia nisiende nyumbani wala kwa ndugu yake yeyote, mimi nikawa nina kwenda lakini kila nikifika mama anatoka nyumbani,kwa kweli ilikuwa ikiniuma sana lakini nilikuwa sina jinsi sababu nilishaamua kuolewa na nampenda mume wangu na nampenda mama yangu,kwa kweli ilikuwa ni muda mgumu sana kwangu,ikafika muda, mama yangu akatuma maneno ya vitisho yani kama tusipoahana atamfanyia mume wangu kitu kibaya,mume wangu akawa na mawazo sana sababu yeye alikuwa si mzaliwa wa hapo,kwahiyo akaingiwa na hofu ikabidi tuachane,lakini tulipanga kuwa tutakuwa tunaonana pale kila mmoja atakomuhitaji mwenzake.

Akaniandikia talaka moja nikarudi nyumbani mama yangu alifurahi sana aliponiona,haikufika muda tukakutana kimwili mimi na mume wangu, tukawa kila siku za mapunziko tunaonana,lakini hatukai nyumba moja,lakini tuko mji mmoja, Baada ya mienzi mimi nikapata safari lakini kabla sijaondoka tukatafuta sehemu  tukakaa wiki nzima ili tuwe na muda wa kuongea kwa kina.

Sasa niko mbali na mume wangu lakini tunawasiliana kama kawaida je bado tunaishi kama mume na mke au? je nikirudi nirudi kwangu au niendelee kuishi na mama? na mama hataki hata kusikia ndugu na majamaa na marafiki wote wameongea nae lakini hamtaki mume wangu hata kumuona na sisi tunapendana.

Naombeni msaada wenu wa kiislam ndugu zangu kama Allaah (SW) alivyosema kuhusu ndoa basi naombeni misaidi kwa hili linalonisibu.  

 SHUKRANII.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani dada yetu katika Imani. Hakika haya ni matatzo makubwa katika jamii yetu kwa wazazi kutojali matakwa ya watoto wao hasa mabinti. Mambo ya ukabila, utaifa, rangi na ubaguzi mwengineo ndio unaozorotesha Uislam kwa ujumla na familia haswa. Wazazi wanatakiwa wajali sana wanaume kwa mabinti zao wenye Dini na maadili. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia nasaha ifuatayo: “Anapokujieni anayekuridhisheni Dini na maadili yake basi mwozesheni. Musipofanya hivyo kutakuwa na fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa” (at-Tirmidhiy).

 

Ndoa yako hapo awali ilikuwa sahihi kabisa, kwani ndoa kama Ibaadah nyingine yoyote ina masharti kukubalika kwake. Masharti yake ni kama yafuatayo:

  1. Idhini ya walii kwa mfano baba, ikiwa hayupo jamaa wa baba wa karibu anashikilia mahala pake kama babu, kakake shaqiqi na mfano wao.

  2. Kupatikana mashahidi wawili waadilifu

  3. Kuridhika kwa msichana au mwanamke (wewe mwenyewe).

  4. Mume kukupa mahari utakayoridhia au muliyokubaliana.

 

Ama kuwa huyo mume si mtu wa hapo au alikuwa ni mfanyikazi wa mamako haijalishi wala si msingi wa ndoa katika Uislamu bora awe ni Muislamu aliyeshika Dini na kuwa na maadili mema. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Enyi watu! Kwa hakika Tumekuumbeni nyote kwa mwanamume mmoja na mwanamke mmoja. Na Tumekfanyeni mataifa na makabila mbali mbali ili mjuane, siyo mkejeliane. Hakika aliye bora mbele ya Allaah ni yule mwenye taqwa zaidi kati yenu” (49: 13). 

 

Japokuwa ilikuwa muhimu sana kumbembeleza zaidi mamako mpaka akubali na aridhie kwa chaguo lako la mume kwani katika hilo huondoa husuma na chuki kama ilivyotokea kwako. Ikiwa imeshindikana Uislamu unakupatia haki ya kujiamulia na hivyo utaendelea na ndoa yako bila wasiwasi wowote kwani imetimiza masharti yote ya kisheria.

Hakika vitisho vya mama au mtu mwengine yeyote haviongezi wala kupunguza maadamu mutakuwa na kinga kwa hilo. Tufahamu kuwa hakuna linaloweza kumpata mtu isipokuwa kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kisomo cha asubuhi na jioni ambacho hutupatia kinga kwa idhini ya Allaah Aliyetukuka na kutuepusha na balaa, wasiwasi, vitisho, mashetani ikiwa tutashikilia. Ilikuwa ni juu yenu musitishike maadam mpo katika jambo la haki.

 

Katika maelezo yako umesema kuwa: “Kwa hiyo akaingiwa na hofu ikabidi tuachane, lakini tulipanga…” na “Akaniandikia talaka moja nikarudi nyumbani…” Swali kwako ni muda gani ulipita kabla hamujakutana tena kimwili? Je, uliketi eda ya kuachwa? Ikiwa ulikaa eda baada ya kuachwa, na mkakutana kimwili katika kipindi hicho cha eda mumeo atakuwa amekurudia lakini ikiwa mlikutana kimwili baada ya eda mtakuwa mnazini na mnapata madhambi kwa kufanya maasiya hayo ya zinaa. Ifahamike kuwa eda linapomalizika kabla ya kukutana kimwili au kusema amekurudia itabidi akuoe upya kwa kukupa mahari yako na kufungwa nikaah. Ikiwa mlirudiana wakati wa eda, je mtaendelea kuishi kwa njia hiyo mpaka lini?

Kwa kuwa hakuna siri katika mas-ala hayo ya muda mrefu. Huenda siku moja mamako akapata habari ya hilo. Je, wakati huo utafanyaje? Utarudi katika lile tatizo la awali na mara hii linaweza kuwa gumu zaidi kuliko awali.

Ikiwa mlikutana kimwili wakati wa eda mtakuwa ni mume na mke. Lau itakuwa kinyume cha hivyo itabidi muombe maghfira na Tawbah ya dhati kabisa kwa Allaah Aliyetukuka na mfunge Nikaah upya na kwa wakati huu muache kuwasiliana kabisa ili msije mkavurugwa na shetani na mkabaki katika madhambi. Ikiwa jibu la kwanza litakuwa mmekutana kimwili katika eda itabidi ukirudi kutoka katika safari uende katika nyumba yako, yaani kwa mumeo. Hakika ni kuwa yeye ana haki juu yako na kujificha machoni mwa watu na haswa mamako kunaondoa haki hiyo na hivyo kubidi nyinyi kuibia katika kitendo cha halali.

Muombe Allaah Aliyetukuka katika Ibaadah zako za kawaida na Swalah ya usiku huku unamlilia Yeye Aulainishe moyo wa mamako kwani Yeye ni muweza wa hilo. Hata hivyo jua na fahamu kuwa ni wajibu wako kumfanyia wema mamako japokuwa yeye anakupiga vita.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akufayie sahali na Akuondolee tatizo lako hilo, Amiin.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share