Talaka Hii Sijafahamu Kama Ni Moja Au Ni Tatu
SWALI:
Asalaam/A/W/W Ustadh mi niliolewa tatizo ni kuwa mimi na mume wangu tumekuwa na matatizo mengi ambayo siwezi kuyaelezea, ila kifupi kwa sababu ya matatizo hayo mimi na mume wangu tukawa hatuna mawasiliano mazuri mpaka akaamua kuniipa talaka ambayo imepigwa mihuri ya ADVOCATE and NOTARY lakini ndani ya hiyo talaka amesema "KUTOKANA NA HAYO LEO NAMPA MKE WANGU HUYO NILIYEMTAJA TALAKA MOJA SI MKE WANGU TENA". Sheikh swali langu ni Je talaka yangu ni sawa na aliyepewa talaka TATU? Japo yeye amesema moja tu? Je natakiwa nikae EDA na baada ya kumaliza EDA yangu je naruhusiwa kuolewa tena na mtu mwengine???? Kwa sababu ninavyojua mume akikupa moja ama mbili ni za kujirekebisha ila anapokupa ya tatu ndio watakiwa ukae Eda Natumai utanielewa vizuri inshaallah Sheikh naomba unifahamishe vizuri kwa sababu mpaka sasa sijielewi nifanye nini juu ya talaka hii.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Ni matumaini yetu kuwa tutaweza kukufahamisha kwa njia ambayo itakuwa sahali na rahisi kwako kuelewa. Suala lako halina utata kabisa ila tu tatizo linakuwa kwa sababu ya mazingira pamoja na ada na desturi tulizonazo kwa njia moja au nyingine.
Awali ya yote tufahamu kuwa mwanamke anakaa eda baada ya kupatiwa na mumewe talaka. Na talaka ya kwanza na ya pili inaitwa talaka rejea kumaanisha kuwa unapokuwa katika eda yako ya twahara tatu au hedhi tatu mume anaweza kukurejea bila ya nikaha mpya. Katika wakati wa eda mke hafai kutoka katika nyumba yake (japokuwa nyumba inaweza kuwa ni ya mume) wala kutolewa mpaka eda imalizike.
Baada ya eda ikiwa mke hakurudiwa na mumewe ana ruhusa ya kuolewa na mwanamme mwingine yeyote anayekuja kuleta posa yake kwake naye akakubali.
Hiyo talaka uliyopatiwa ni moja, hivyo unafaa ukae eda mpaka muda wake umalizike. Ikiwa atakurudia kabla ya eda kumalizika itakuwa ni kheri kwenu. Ikiwa eda itamalizika bila kukurudia basi akiamua kukurudia baada ya eda itabidi alete posa nawe ukikubali upewe mahari mapya
Kwa muhtasari ni kuwa hiyo ni talaka moja. Unafaa ukae eda na baada yake unaweza kuolewa na mwanamme mwengine yeyote.
Na Allaah Anajua zaidi