Mume Amenitekeleza Karibu Mwaka Hanijali, Hataki Ushauri, Je Niombe Talaka Au Itakuwa Nakosea?
SWALI:
Salaam alaykum,
Mimi ni binti mwenye umri wa miaka 26, nimeolewa Alhamdulillah miaka mitatu iliyo pita, sikubahatika kupata mtoto. Mume wangu amenitelekeza takribani kipindi cha mwaka sasa hanijali kwa kula, kuvaa wala kwa maradhi. Yupo mbali nami ninapojaribu kumuuliza ananipa majibu mabaya nimejaribu kumwitia wakubwa lakini hali ni ile ile, sasa nimechoka na hii hali je nifanyeje?
Mimi nashindwa kufanya maamuzi ya kudai talaka kwa kumuhofia Mwenyezi Mungu kwani hii ndoa mimi nilifanya ibada ya maombi kumuomba mwenyezi mungu anijalie nusura na mwenyezi Mungu akanijibu, leo hii imekuwa mtihani mkubwa kwangu, hivyo kabla ya kuamua naona bora niombe ushauri kwenu alhidaaya.
Inshaallah Mwenyezi mungu awaongoze na awafanyie tawfiq kwenye kazi nzito ya kuelimisha jamii, kila la kheri.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kudai talaka kwa ajili ya kutelekezwa na mume. Ni lazima dada yetu uwe na hofu kwani kuna onyo kali
Dhulma kisheria ni kubwa zaidi, kwani imeharamishwa na Allaah Aliyetukuka na maafa anayopata mwenye kudhulumu ni makubwa
1. Mwanzo inatakiwa uzungumze na mumeo kwa mara nyingine tena kwani yeye ni mume wako bado mbali na kwamba amefanya dhulma ya kutokuangalia inavyotakiwa Kiislamu. Zungumza naye kuhusu ndoa yenu na kwamba yeye ameamua vipi kwa kule kukuacha. Je, amekutaliki na hakutaki tena au bado ni mke wake. Ikiwa atatamka kuwa amekutaliki basi utakuwa si mke wa mtu na itakubaki ukae eda lakini lau atasema kuwa wewe bado ni mke wake utafuata kipengele cha pili ili kupata ufumbuzi wa kihakika.
2. Waelezee wazazi wako kuhusu yanayokusibu na matatizo yanayokukabili. Baada ya hapo inahitajika uwaelezee wazazi wa mumeo kwa njia ya kutaka ufumbuzi, nao utapatikana kwa familia hizo mbili kukutana ili muweze kutatatua shida hiyo uliyo nayo. Ikiwa kweli wazazi watataka suluhu basi itapatikana bila ya shida aina yoyote ile. Allaah Aliyetukuka Anasema: “Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari” (an-Nisaa’ [4]: 35).
3. Ikiwa hakukupatikana suluhu kwa sababu moja au nyingine basi inatakiwa upeleke mashitaka yako kwa Shaykh ambaye amewaoza, au mwingine ambaye ana elimu, mcha Mngu na muadilifu au Qadhi wa sehemu unayoishi. Hapo utajieleza kuhusu yanayo kusibu na matatizo uliyokumbana nayo na bila shaka hayo uliyo yaeleza ni sababu tosha ya Qadhi kutoa talaka au mume ajirekebishe na kulipa masurufu yako yote kwa mwaka ikiwa anataka kubaki nawe.
Kwa hiyo kufuatilia suala
Nasaha nyingine ambayo tunaweza kukupatia kwa wakati huu ni kuwa ni vyema unapoomba kitu kwa Allaah Aliyetukuka uombe unavyotaka. Hapa kama tulivyo soma ulikuwa umeomba tu nusra ilhali ilikuwa uombe mume mwenye kheri aliyeshika Dini barabara.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akutoe katika tatizo na shida hiyo na Akuunganishie kila la kheri na alete hatima njema katika kufuatilia ufumbuzi wa tatizo lako.
Na Allaah Anajua zaidi.