Aina Za Laana Na Wepi Waliolaaniwa na Allaah?

 

Aina Za Laana Na Wepi Waliolaaniwa na Allaah?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Kwanza kabisa namshukuru Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa. na kumtakia rehma Nabiy Muhammad kiongoza wa Umma (S.A.W) na Masheikh wote ambao usiku na mchana wako macho kujibu maswali yetu/ya waislaam.

Baada ya hapo ningependa kuuliza maswali yafuatayo. Ni Nani Haswa Anastahiki Kuambiwa Laana Za Allaah Ziwe Juu Yako. Je Ni Makafir Au Murtadina Au Wanaafiq? Je Kuna Laana Ya Mtu Mmoja Mmoja Ua Wengi Wengi?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Nabiy, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’aalaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mas-ala ya laana. Laana si kitu kumpata mtu yeyote yule na hasa akiwa ni Muislamu. Laana kutoka kwa Allaah au Nabiy Wake inampata mwenye kuacha amri na yule aliyekengeuka na maagizo yao. Allaah Aliyetukuka na Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) wametutajia watu waliteremshiwa laana hizo.

 

Hebu tutazame baadhi ya mifano:

 

a)            Allaah Aliyetukuka Anasema:

إِنَّ اللَّـهَ لَعَنَ الْكَافِرِينَ وَأَعَدَّ لَهُمْ سَعِيرًا ﴿٦٤﴾

Hakika Allaah Amewalaani makafiri, na Amewaandalia moto uliowashwa vikali mno. [Al-Ahzaab: 64].

 

b)           Allaah Aliyetukuka Anasema:

لَّئِن لَّمْ يَنتَهِ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ وَالْمُرْجِفُونَ فِي الْمَدِينَةِ لَنُغْرِيَنَّكَ بِهِمْ ثُمَّ لَا يُجَاوِرُونَكَ فِيهَا إِلَّا قَلِيلًا ﴿٦٠﴾مَّلْعُونِينَ ۖ أَيْنَمَا ثُقِفُوا أُخِذُوا وَقُتِّلُوا تَقْتِيلًا ﴿٦١﴾

Ikiwa wanafiki, na wale ambao katika nyoyo zao mna maradhi, na waenezao fitnah katika Al-Madiynah hawatokoma, bila shaka Tutakusalitisha juu yao, kisha hawatokaa humo kuwa jirani zako isipokuwa kidogo tu. Maluuni hao!  Popote wanapopatikana, wachukuliwe, na wauliwe mbali mauaji kamilifu. [Al-Ahzaab: 60 – 61].

 

c)           Allaah Aliyetukuka Anasema:

إِنَّ الَّذِينَ يُؤْذُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأَعَدَّ لَهُمْ عَذَابًا مُّهِينًا ﴿٥٧﴾

Hakika wale wanaomuudhi Allaah na Rasuli Wake, Allaah Amewalaani duniani na Aakhirah, na Amewaandalia adhabu ya kudhalilisha. [Al-Ahzaab: 57].

 

d)           Anasema tena Aliyetukuka:

فَبِمَا نَقْضِهِم مِّيثَاقَهُمْ لَعَنَّاهُمْ وَجَعَلْنَا قُلُوبَهُمْ قَاسِيَةً ۖ 

Kwa sababu ya kuvunja kwao fungamano lao, Tuliwalaani na Tukazifanya nyoyo zao kuwa ngumu... [Al-Maaidah: 13].

 

e)          Anasema tena:

..أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ﴿١٨﴾

Tanabahi! Laana ya Allaah iko juu ya waliodhulumu. [Huwd: 18].

 

f)           Anasema tena:

ثُمَّ نَبْتَهِلْ فَنَجْعَل لَّعْنَتَ اللَّـهِ عَلَى الْكَاذِبِينَ ﴿٦١﴾

Kisha tuombe mubaahalah, tuifanye laana ya Allaah iwe juu ya waongo. [Aal-'Imraan: 61].

 

g)         Anasema tena Aliyetukuka:

 

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿٧٨﴾

Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israaiyl kwa lisani ya Daawuwd na ‘Iysaa mwana wa Maryam. Hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakitaadi [Al-Maaidah: 78].

 

Tukizitazama Aayah hizi utapata ya kwamba waliolaaniwa na Allaah Aliyetukuka ni wengi miongoni mwao ni makafiri, madhalimu, walioasi, waliotupa mipaka, wanaomuudhi Allaah na Nabiy Wake, wanafiki, waongo, watangazao uovu, wenye kuficha Aliyoteremsha Allaah, na kadhalika.

 

Ama hawa watakaopata laana ya Allaah, basi Aliyetukuka Anatueleza:

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَعَنَهُمُ اللَّـهُ ۖ وَمَن يَلْعَنِ اللَّـهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ نَصِيرًا ﴿٥٢﴾

Hao ndio wale Allaah Aliowalaani. Na ambaye Allaah Amemlaani basi hatopata wa kumnusuru. [An-Nisaa: 52].

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share