Kuinuliwa Mtoto Mchanga Magharibi Na Kumlaza Kifudifudi Imethibiti Usahihi Wake?
Kuinuliwa Mtoto Mchanga Magharibi Na Kumlaza Kifudifudi Imethibiti Usahihi Wake?
SWALI:
As. kum In Shaa Allaah wote wazima.
Naomba niulize hivi – Ina maana gani kumlaza mtoto kifudifudi?
Watu wengi utawasikia wakisema mtoto mchanga ainuliwe (asiwekwe chini hata kama kalala umuinue) wakati wa maghrib kwa nini?
JIBU:
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa RahmatuLLaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaahi wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho:
Maamkizi Ya Kiislaam: Maamrisho Na Fadhila Zake
Haikuthibiti katika mafunzo ya Dini yetu kuwa inapofika Magharibi mtoto mchanga ainuliwe au alazwe kifudifudi. Hivyo ni vyema kuepukana na mambo ya kuzushwa.
Pia itambulike kuwa aina hii ya kulala ya kifudifudi kumekatazwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama inavyotuelimisha Hadiyth ifuatayo.
Imepokewa kwa Ya‘iysh bin Twikhfah Al-Ghifaariy (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba aliniambia babangu: Nilipokuwa nimejilaza katika Msikiti juu ya tumbo langu mara nikahisi mtu ananitingisa kwa mguu wake, akisema: “Hakika ulalaji huu haupendi Allaah”. Akasema: “Nikamuangalia na kumuona kuwa ni Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)” [Abuu Daawuwd kwa Isnadi Swahiyh. Ahmad na at-Tirmidhiy wamenukuu kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), nayo ni Hadiyth Swahiyh].
Katazo hili ni kwa kila Muislamu awe ni mtoto au mtu mzima, japokuwa mtoto huwa hawezi kujimudu kutekeleza hivyo. Kwa hiyo, ni wajibu wa mzazi kutomlalisha mtoto wake kifudifudi. Hekima ya jambo hilo lipo wazi kabisa kwani anapolala hivyo hasa mtoto mchanga anaweza mara moja kujiziba pumzi, ukosefu wa pumzi unaweza kumfanya kuaga dunia.
Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha namna ya sisi kulala, mlalo wa kufuata Sunnah na hivyo kupata thawabu kwayo. Amesema Mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa): “Alikuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiswali rakaa kumi na moja za usiku, lakini pindi inapoingia Alfajiri alikuwa akiswali rakaa mbili hafifu (fupi), kisha akijilaza kwa ubavu wake wa kulia mpaka aje Muadhini amuarifu ya kwamba watu wamejumuika (kwa ajili ya Swalaah) [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na hayo katika maswali yako ni mambo ambayo ameyafunza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), bali lililo sahihi wakati huo ni kuwazuia watoto wasitoke nje ili wasije kukumbwa na mashaytwaan wakadhurika kama ilivyo katika Hadiyth ifuatayo:
قَالَ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّم: ((إِذَا كَانَ جُنْحُ اللَّيْلِ أَوْ أَمْسَيْتُمْ فَكُفُّوا صِبْيَانَكُمْ، فَإِنَّ الشّيَاطِيَ تَنْتَشِرُ يَنْتَشِرُ حِينَئِذٍ، فَإِذَا ذَهَبَ سَاعَةٌ مِنْ اللَّيْلِ فَخَلُّوهُمْ، وَأَغْلِقُوا الْأَبْوَابَ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ فَإِنَّ الشَّيْطَانَ لَا يَفْتَحُ بَابًا مُغْلَقًا، وَأَوْكُوا قِرَبَكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ، وَخَمِّرُوا آنِيَتَكُمْ وَاذْكُرُوا اسْمَ اللَّهِ وَلَوْ أَنْ تَعْرضُوا عَلَيْهَا شَيْئًا، وَأَطْفِئُوا مَصَابِيحَكُم))
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وسلم) amesema: ((Ikiingia jioni [yaani jua linapokuchwa wakati wa Magharibi] wazuieni watoto wenu kutoka toka nje kwani mashaytwaan wanatawanyika nyakati hizo. Ukishapita wakati waacheni. Na fungeni milango yenu na mtajeni Allaah mnapoifunga [mseme: BismiLLaah], kwani shaytwaan hafungui mlango uliofungwa. Na fungeni viriba vyenu vya maji, na mtajeni Allaah [mseme: BismiLLaah]. Na funikeni vyombo vyenu na mtajeni Allaah [semeni: BismiLLaah] (funikeni) hata kama ni kwa kuwekea kitu ju. Na zimeni taa zenu
[Al-Bukhaariy pamoja na al-Fat-h (10/88), Muslim (3/1595)]
Na Allaah Anajua zaidi