Zingatio: Ole Wao Siku Hiyo Hao Wanaokana

 

Zingatio: Ole Wao Siku Hiyo Hao Wanaokana

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Muumba Mwenye viapo kila aina,

Anatuhakikishia kuwa ipo Siku itasimama,

Wakati ukiwadia wa kuisagasaga milima,

Mwezi na nyota zitakapokunjana,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Aliyetolewa tumboni atamkimbia wake mama,

Aliyebeba mashaka tisa miezi atamuacha mwana,

Rafiki na wapenzi walio karibu watafarikiana,

Ndugu kwa ndugu watakaribia kupigana,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Sauti ya Mwingi wa Rehema Itakaponguruma,

Makafiri na wanafiki nyoyo zao hazitatuwama,

Waliokadhibisha kwao haipo katu salama,

Vilio vyao havitawaweka sehemu njema,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Umri uliopotezwa hautarudi nyuma,

Kwa nguvu watajaribu meno kuyabana,

Wakijuta kujishughulisha zaidi na ngoma,

Mipira na starehe zisizokuwa na maana,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Wale waliokadhibisha Zake nyingi neema,

Wakafanya usengenyaji kuwa amali ya kuchuma,

Wakati ukawapita Aakhirah hawakuitizama,

Wataburuzwa ndani ya moto hutwama,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Waliokadhibisha neema watashuhudia Qiyaamah,

Wataingizwa katika moto ulio mrefu na mpana,

Usio kuwa na kizuri chakula wala huruma,

Adhabu zitapanda daraja kwa kufuatana,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Watiifu kwa Rabb waliotumia vyema zama,

Wataingizwa Jannah nyoyo zipate salama,

Amani na utulivu utokao kwa Karima,

Utawapatia faraja na furaha daima,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Waliomcha Allaah watalipwa mema,

Watakula na kustarehe wapendavyo namna,

Watakuwa na maisha yasiyo koma,

Ni malipo yatokayo kwa mwingi wa Rehema,

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

Ee Muislamu haujafika wakati bayana?

Wa kujiweka mbali na sifa za anayekana?

Ukatenda mazuri na yaliyo mema?

Je unataka kulipwa mfano wa huyo anayekana?

Ole wao siku hiyo hao wanaokana.

 

 

Share