Mas-ala Kadhaa Ya Hedhi na Istihaadhwah
Mas-ala Kadhaa Ya Hedhi na Istihaadhwah
SWALI:
Assalaam aleykum warahmatullaahi ta'ala wa barakaatuhu. Amma ba'ad:
1. Kwa baadhi ya wanawake, baina ya hedhi mbili hua kuna "discharge" ya rangi kama hedhi inapomaliza. Jee hii ni kitu gani au ni katika process za "ovulation"? Nini hukmu ya sala na ibada nyengine katika hali hii?
2. Hedhi inayozidi wiki 2, ikaambatana na damu "bright red lakini ni nzito kidogo ni istihaadhwah? Tohara ifanyike baada ya wiki 2 au siku 7?
3. Haya matatizo kwa uzoefu wenu, yanasababisha kukosa kizazi?
Hili jambo linatia wasiwasi sana na naomba mnisaidie nifanye nini au nishikamane na dhikri gani ya Allah ili nitoe khofu na niwe karibu zaidi na mola wangu?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu
Hakika ni kuwa masuala haya hayafai kuwapatia dada na mama zetu utata aina yoyote. Hii ni dalili kuwa hatuna malezi ya kisawasawa katika mambo haya katika majumba yetu. Wazazi hasa kina mama wanatakiwa wawafunze watoto wao wa kike kuhusu uuke na masuala haya wakati wanakarabia kuvunja ungo (kubaleghe) ili wasipate matatizo hayo. Kwa kila hali, hilo halifanyiki hivyo inabidi sisi tuwe tutafanya kazi hiyo na imekuwa wajibu wetu kufanya hilo.
Hata hivyo, kabla ya kuingia kujibu maswali hayo yaliyoulizwa ni muhimu kwa wasichana kwenda katika darsa ambazo zinaandaliwa na kina dada walio na taaluma ya Uislamu ili wapate kujifunza hayo na mengi. Hatufai kudharau hilo ili tusije tukaingia katika tata na mashaka hapa duniani na kesho Akhera.
Mwanzo tunatakiwa kufahamu kuwa hedhi yenyewe ni ugonjwa, kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ ۖ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُوا النِّسَاءَ فِي الْمَحِيضِ ۖ وَلَا تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىٰ يَطْهُرْنَ ۖ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللَّـهُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ ﴿٢٢٢﴾
Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Sema: “Hiyo ni dhara; basi waepukeni wanawake katika hedhi. Wala msiwakaribie kujimai nao mpaka watwaharike. Watakapotwaharika basi waendeeni kupitia pale Alipokuamrisheni Allaah.” Hakika Allaah Anapenda wenye kutubia na Anapenda wenye kujitwaharisha. [Al-Baqarah: 2: 222].
Adha maanake ni ugonjwa na mwanamke ambaye yuko katika hedhi mambo yake mengi yanabadilika. Pia ni ugonjwa kwa kuwa damu kama ile ikibakia ndani ya mwili italeta madhara kwa mwanamke ndio kwa rehema ya Allaah Aliyetukuka Akaifanya kuwa inatoka mwilini katika nyakati zake maalumu.
Tufahamu kuwa damu ya hedhi inafahamika bila ya matatizo yoyote na hasa wanawake wenye kutokwa na damu kama hiyo. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Faatwimah bint Abi Hubaysh (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) ambaye alikuwa akitokwa na damu kwa wingi na muda mrefu, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia,
“Ikiwa ni damu ya hedhi, itakuwa ni nyeusi yenye kujulikana. Ikiwa ni hiyo, acha Swalah. Ikiwa ni nyingine mbali na hiyo, chukua wudhuu na uswali, kwani huo ni mshipa tu” (Abuu Daawuwd, an-Nasaa’iy, Ibn Hibbaan na ad-Daaraqutwniy).
Zipo aina kadhaa za damu, kwa mfano:
1-Nyekundu: Rangi asili ya damu.
2-Manjano: Ni maji maji kama usaha.
3-Udongo: Ni rangi ya katikati baina nyeusi na nyeupe, kama uchafu.
Imepokewa kuwa wanawake walikuwa wakimpelekea ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anha) viboksi vyenye pamba zilizoingia rangi ya manjano, naye akawa anawaambia,
“Msifanye haraka mpaka muone pamba safi nyeupe” (Maalik na Muhammad bin al-Hasan).
Ikiwa hiyo discharge (kinachotoka) ni rangi ya njano au udongo katika masiku ya hedhi, inachukuliwa kuwa ni hedhi. Lakini ikiwa katika siku nyingine zisizokuwa katika zile nyakati za hedhi, haitachukuliwa kuwa ni hedhi. Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Ummu ‘Atwiyyah (Radhwiya Allaahu ‘anha) aliyesema:
“Baada ya kuwa tuliingia katika twahara, hatukuchukulia kutokwa kwa vitu vya manjano au rangi ya udongo (uchafu) kuwa ni chochote” (Abu Daawuwd and al-Bukhaariy, lakini bila ya maneno “...baada ya utwahara...”
Hivyo basi, ikiwa mwanamke anatokwa na umaji baina ya hedhi huwa kutokwa huko hakuchukuliwi ni chochote. Kwa hiyo, mwanamke huyo anafaa aswali na afunge pamoja na kufanya ‘Ibaadah nyingine. Hayo ni katika maumbile au ni ugonjwa ambao mwanamke huenda akapatikana nao.
Ama hedhi ikizidi ada yako, kwa mfano ikiwa unapata hedhi siku saba au wiki mbili, damu yoyote inayotoka baada ya muda huo huwa ni damu ya ugonjwa, Istihaadhwah. Kwa hiyo, unafaa ufanye ‘Ibaadah zote kama Swalah, Swawm na hata kukutana na mumeo kimwili. Ama kuhusu kufanyika twahara inategemea wewe kwa desturi yako unapata hedhi kwa siku saba au wiki mbili. Ikiwa ni siku saba na ikaongezeka zaidi ya hapo inafaa ujitwahirishe baada ya siku hizo na kufanya ‘Ibaadah zako kama kawaida.
Ama kuhusu kusababisha kuzuia kizazi, hakika sisi hatuna elimu na ujuzi wa utabibu na maswali kama haya yanapaswa yaulizwe kwa matabibu wenyewe sio kwetu. Lakini kukufanyia wepesi, tumejaribu kuuliza kwa matabibu wa fani hiyo ni kwamba: Inategemea na kila mwanamke na maumbile yake na pia inategemea na muda wenyewe wa istihaadhwah. Ikiwa isithaadhah inaendelea mfano kwa muda wa baina ya siku 21 au siku 25, . Hii kwa maana mfano mwanamke amepata siku zake za hedhi tarehe 1 - kisha akamaliza tarehe 7, kisha akaja kupata tena baada ya siku 21 au siku 25 basi huwa ni hedhi ya kawaida isiyoathiri uzazi. Lakini ikiwa anarudia kupata siku zake chini ya wiki tatu basi huwa ni kukosekana kutokea uovishaji (ovulation). Na hivyo mwanamke inampasa aende kuonana na tabibu hasa mtaalam wa mambo ya uzazi, mwanajinakolojia (gynecologist) ili apate kuchekiwa kwani hiyo husababisha na inayoitwa 'hormone imbalance'.
Haya matatizo ya kutokwa damu kwa wingi na muda mrefu ni maumbile ya baadhi ya wanawake. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea huo ni ugonjwa. Na kwa kuwa Allaah Aliyetukuka Hakuleta ugonjwa isipokuwa Ameteremsha na dawa yake inafaa ikiwa utapatwa na tatizo hilo uende kwa daktari aliyebobea katika magonjwa ya kike.
Na Allaah Anajua zaidi