Mume Kapoteza Thamani Kwa Mke Na Katumia Pesa Zake

 

SWALI:

A.A.KWANZA NAWASHUKURU SANA NDUGU ALHIDAYA. SWALI HILI NITAKALO ULIZA NI LA RAFIKI YANGU AMEOLEWA SASA NIMIAKA 16. MWANZO WANDOWA WALIKUWA WAKIELEWANA NA MUMEWE WALIPOKUWA WAKIISHI AFRIKA KENYA LAKINI TOKEYA WAJE UINGEREZA HAWANA MAELEWANO MKE NI SHARIFU KUTOKA LAMU NA MUME NI MPAKISTANI TOKEYA WENDE PAKISTANI BWANA AMENUNUWA NYUMBA KUWAWEKA WATU WAKE NA NYUMBA INAMPAKA MADUKA YALETA KODI. PESA ZAKUNUNUWA NYUMBA HIYO NUSU YAKE AMEMTIYA MKE KUTWA DENI BENKI MWAKA WA 4 HAJAMLIPA MKEWE MAPENI YAKE NA
HIYO KODI PIYA HAIYONI NA JUU YAKE MANENO NA WATU WA MKE HAWATAKI HATA KUWAONA HAMWAMKUI HATA BABAKE MKE. NA KUWATIYA WATOTO MANENO MAMA YENU APATA PESA ZA
SERIKALI NA NI ZENU AWAPA WATU WAKE MIMI KUOLEWA NA YEYE NI MUME WA PILI PIYA AWAMBIA WATOTO MPAKA MAJIRANI AMEOLEWA AKAWATWA KWA SABABU ANA MDOMO YUWAJIBU WAUME. NIWAITA JAMII BABANGU HADI JIRANI KUMSEMESHA LAKINI TABIYA YAKE ILE
ILE. SASA MPAKA NIMECHOKA NDIYO NIKAAMUWA KUWAULIZA NYINYI NDUGU WA ALHIDAYA MUNIPE MAONI YENU



 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa dada yetu ambaye ameonyesha Al-Hidaaya tunaweza kumsaidia katika tatizo alilonalo rafiki yake ambaye yu matatizoni.

 

Matatizo katika ndoa na kwa wanandoa ni suala ambalo linatarajiwa lakini hata hivyo halifiki katika kiwango hicho ikiwa kweli uchaguzi wao ulifanywa kwa njia za Kiislamu.  Lakini mara nyingi uchaguzi wetu haui kwa njia hiyo ndio matatizo na shida za wanandoa zimekithiri katika jamii yetu.

 

Hata hivyo, Uislamu umeweka njia za kuoana na pia ukaweka ufumbuzi barabara kwa matatizo pindi yanapotokea. Kwa hiyo, shida zinapotokea inabidi turudi katika misingi ya Kidini ili tuweze kutatua kwa njia safi kabisa na bila kuacha kinyongo kutoka kwa upande wowote ule.

 

Tatizo hapa limetokea lakini tumepata ufahamu wa tatizo hilo kutoka upande mmoja na inakuwa vigumu kutatua kwa njia hiyo. Mbali na hayo tutakupatia nasaha zetu za kijumla na twataraji kuwa shida hiyo itaondoka.

 

Kama tulivyotangulia kusema kuwa Uislamu umetupatia muongozo wa kutatua matatizo yetu ya kindoa. Tuna Imani kuwa lau njia hizi zitafuatwa basi kwa kiasi kikubwa shida hizo zinaweza kuondoka au kupunguzwa. Njia zenyewe ni kama zifuatazo:

 

1.      Kila upande lazima uwe na nia safi na njema. Ikiwa suluhu inatakiwa na inahitajika ipatikane ni lazima tufanye hayo kwa kutaka kweli suluhu na kuondosha tatizo ambalo lipo kwa wanandoa. Allaah Aliyetukuka Anasema: "Ikiwa kweli mnataka suluhu basi Allaah Atawawafikisha katika hilo" (4: 35).

2.      Mke akiwa anapata matatizo kutoka kwa mumewe anahitajika kumuweka mumewe chini ili aweze kuzungumza naye kinaganaga ili waweze kusuluhisha hata kabla ya kwenda kwa watu walio nje yao wenyewe.

3.      Ikiwa hakuna natija yoyote nzuri basi kutakuwa hapana budi ila kuwaita wawakilishi wa familia hizo. Maana ya hilo ni kupata mwakilishi (au wawakilishi) kwa upande wa mume na mke, na wanandoa wenyewe wawepo katika kikao hicho. Wakati huo inatakiwa kila mmoja aeleze haki kwa yale yaliyotokea ili kupatikane ufumbuzi. Hii ni kwa mujibu wa Suratun Nisaa' (4); Aayah ya 35.

4.      Ikiwa haukupatikana ufumbuzi wowote kwa tatizo hilo basi kutakuwa hakuna budi ila kwenda kwa Qaadhi ikiwa wapo. Ikiwa hawapo maqaadhi katika nchi hiyo (ya Uingereza) basi atakwenda kwa centre yoyote ya Kiislamu au kumpata Imaam aliye muadilifu kusikiliza kesi hiyo ya rafiki yako na mumewe.

 

Hii njia ya mwisho ndiyo yenye kutegemewa ikiwa njia zote nyingine zimeshindikana kupatika kwa suluhu ya aina yoyote ile. Katika njia ya mwisho bado mume au mke amekaidi basi hapo kutakuwa hakuna budi isipokuwa kupite talaka na kila mmoja aishe kivyake mpaka kila mmoja wao atakapopata kheri nyingine. Ima mke apate mme watakaoelewana na mume naye apate mke watakaosikilizana.

 

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Awasikilizanishe na Awadumishe pamoja ili wapate kulea watoto wao kwa njia nzuri.

 

Matatizo mengine uliyoyaelezea ni nyeti sana kwetu sisi kuweza kusaidia kwa sababu ya umbali wetu nanyi. Kama mume kuchukua haki ya mkewe, kuwatia watoto maneno na kadhalika. Hakika hayo ni mambo mabaya kwa Muislamu kuyafanya na tena kumfanyia mwenza wake. Nasaha ambayo pia tunaweza kukupatia ni kuwa hayo yazungumzwe katika vikao vyote ambavyo watakaa kuzungumzia tatizo nyeti la ndoa yao

 

Tunaona ajabu kuwa mwanzo walikuwa wanaishi vizuri kama ulivyosema kisha baadaye mume akageuka kwa ghafla lakini hayo kwa mwanadamu huenda yakatokea. Cha muhimu ni kuwa suala hilo lisiachwe lichukue muda bali inatakiwa mlishughulikie mara moja ili ubaya na matatizo yasizidi.

 

Tunakutakia kila la kheri na fanaka katika kusaidia hiyo ndoa nasi du’aa zetu kwa Allaah Aliyetukuka zipo pamoja nanyi. Na tunamuomba Manani Awapatie suluhu na ufumbuzi muafaka kabisa inshaAllaah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share