Zingatio: Yatosha

 

Zingatio: Yatosha

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Binaadamu ni kiumbe aliyejawa na nyingi harakati. Muda tu anapozaliwa huwa ni mwenye kuwaza na mwenye matarajio kila aina. Wanaadamu wote wamejawa na shughuli za kufanya ikiwa ni mwenye akili au mwendawazimu. Lakini mbona hatujiulizi ni kwanini tumejawa na shughuli hizi na nini athari zake? Na kwanini huyo aliye na akili shughuli zake zinafanana na mwendawazimu?

 

Tutakapojibu suala hilo na kuelewa azma ya kuumbwa kwetu hapa duniani ndipo tutakapojipanga vizuri ili tupate mafanikio. Uzuri wa hizi shughuli zetu ni kwamba, zinatupelekea kuwa ni wabunifu wa mambo kadha wa kadha. Bahati mbaya hata hivyo vilivyo vizuri vinatumiwa kinyume na maadili ya Uislamu, matokeo yake ni kuporomoka kwa tabia tu.

 

Tunashuhudia miziki, wizi, utapeli, picha zisizofaa, riba, pombe, uongo na usengenyaji ndani ya mizunguko ya shughuli zetu hizi. Masikini wengine, huwa wala hawana nia ya kushuhudia au kuyatenda hayo mambo, lakini kutokana na kuanguka kwa khulqa za wanaadamu ndio huathirika na yeye. Hata hivyo, bado tutakuwa na hoja ya kuijibu mbele ya Muumba kwa kila sekunde tuitumiayo duniani, ikiwa kwa kukusudia au kutokusudia. Sasa ole wao, tena ole wao! Wakayatafuta masuala haya kwa makusudi kabisa, wakayachangia kwa pesa na mali zao, jasho likawatoka kwa kuyafanyia kazi, wakayaingia kwa vichwa na miguu, hao sijui wataenda kumjibu nini Mola Muumba.

 

Basi ndugu yangu Muislamu, haitoshi kupita kwako na kusikia miziki ikipigwa kulifanya kuwa ni kosa? Maisha yetu yamekuwa ni mzunguko wenye aina tofauti katika masuala ya haramu. Akiba zetu ni zenye thamani ya riba, malipo tunayopatiwa ndio yenye kutokana na makusanyo ya pombe, rushwa ni msingi wa mali zetu na kadhalika. Bado tu Muislamu anakwenda kununua miziki, pombe, kuifuata riba na mengineyo kwa makusudi kabisa akayatenda macho yakiwa kupe kupe huku akipumuwa kwa pumzi alizoruzukiwa na Muumba. Muislamu mwenye kudai kuamini Shahadah lakini bado akawa hataki kuachana na miziki, pombe, uzinifu n.k. huyo atakuwa na masuala zaidi ya kujibu.

 

Tuielewe hii dunia yetu na khulqa zinazotuzunguka ni za ajabu kabisa! Kupata mafanikio sio rahisi mbele ya Muumba. Ni lazima tuchukue juhudi kubwa na za makusudi kuepukana na vitimbi hivi. Inatosha kuelewa ni wakosa kwa kuiacha jamii inayotuzunguka kuwa ni walevi, wazinzi na wala rushwa. Sasa huyo anayeyaingia haya masuala kwa makusudi ni sawa na mwenye kidonda kukipalilia kwa kaa la mawe huku akiamini kuwa kitapoa. Tuhimizane kuachana na machafu huku tukijihimu na sisi kuyatokomeza kwa hali na mali.

 

Share