Vipi Wazazi Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Wawe Motoni Ilhali Allaah Haadhibu Watu Hadi Atume Rusuli?

 

SWALI:

Assalaam alaykum.

Kutokana na maelezo ya swali lililoulizwa juu ya wazazi wa Mtume Muhammad (Swala Allah alayhi wasalam) inaonesha kuwa Allah (Subhanahu wa taala) amemkata Mtume kumuombea mama yake kwa sababu alikufa kaafir kama ambavyo inaelezwa katika qur'an 9: 113):

Lakini nimesoma katika Qur’an kuna aya inayosema kuwa Allah (subhana wa taala) hauadhibu umma mpaka kwanza awapelekee muonyaji (Mtume

Swali ni je, vipi makafiri waliokufa kabla ya Mtume (swala Allah alayhi wa salam) kuja wawe watu wa motoni ikiwa ujumbe wa Allah hawakuupata?

Naomba yeyote mwenye maelezo/ majibu anisaidie.

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kauli za Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) ulizozigusia ni zifuatazo ambazo zinadhihirisha kuwa Aliyetukuka Anatueleza kuwa hakuna taifa ila Alipeleka Nabii:

 

((إِنَّا أَرْسَلْنَاكَ بِالْحَقِّ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خلَا فِيهَا نَذِيرٌ))

 

((Hakika Sisi Tumekutuma wewe kwa haki, kuwa ni mbashiri na mwonyaji. Na hapana Ummah wowote ila ulipata mwonyaji kati yao)) [Faatwir: 24].

 

(( وَمَا كَانَ رَبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَى حَتَّى يَبْعَثَ فِي أُمِّهَا رَسُولاً يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِنَا وَمَا كُنَّا مُهْلِكِي الْقُرَى إِلَّا وَأَهْلُهَا ظَالِمُونَ))  

 

((Na Mola wako Mlezi Haangamizi miji mpaka ampeleke Mtume katika miji yake mikuu awasomee Ishara Zetu. Wala hatuiangamizi miji mpaka watu wake wawe madhaalimu)) [al-Qaswasw: 59]  

 

(( ذَلِكَ أَن لَّمْ يَكُن رَّبُّكَ مُهْلِكَ الْقُرَى بِظُلْمٍ وَأَهْلُهَا غَافِلُونَ ))

 

((Hayo ni kwa sababu ya kuwa Mola wako Mlezi Hakuwa wa kuiangamiza miji kwa dhulma, hali wenyewe wameghafilika)) [Al-An’aam 131]

 

Hiyvo ni dhahiri kwamba watu wa Makkah pia nao walitumiwa Nabii Ismaa‘iyl (‘Alayhis Salaam) na kwa hakika hata kabla ya kuzaliwa kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kulikuwa na watu waliokataa kuabudu masanamu. Hakuna kafiri aliyekuwa kabla ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ila alikuwa ametumiwa Mjumbe kwa njia moja au nyingine

 

Na yeyote atakayefariki katika hali ya kufru basi atakuwa ni mtu wa motoni hata kuhusiana kwake na aliyekuwa karibu na Allaah hakutamsaidia chochote siku ya Qiyaamah. Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alimjibu mtu alipomuuliza kuhusu mzazi wake:

 

عَنْ أَنَسٍ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَجُلا قَالَ : يَا رَسُولَ اللَّهِ ، أَيْنَ أَبِي ؟ قَالَ: ((فِي النَّارِ))  فَلَمَّا قَفَّى دَعَاهُ ، فَقَالَ: ((إِنَّ أَبِي وَأَبَاكَ فِي النَّار))  مسلم

 

Kutoka Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba mtu mmoja alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam): Ewe Mjumbe wa Allaah, baba yangu yuko wapi? Akasema: ((Motoni)). Alipogeuka akamwita kisha akamwambia: ((Baba yangu na baba yako wako motoni)) [Muslim]

 

Na kwa kuwa Allaah Aliyetukuka ni Mwadilifu na mbele Yake hadhulumiwi yeyote anajua hali ya kila mmoja. Na kuwaombea makafiri maghfira tumekatazwa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala):

 

((مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُواْ أَن يَسْتَغْفِرُواْ لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُواْ أُوْلِي قُرْبَى مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ))

 

((Haimpasii Nabii na wale walioamini kuwatakia msamaha washirikina, ijapokuwa ni jamaa zao, baada ya kwisha bainika kuwa hao ni watu wa motoni)) [At-Tawbah: 113]

 

 

 

Zifuatazo ni kauli za baadhi ya Maulamaa:

 

 

 

Imaam An-Nawawiy:

 

“Yeyote atakayefariki katika fatrah (kipindi cha mapumziko ya wajumbe baina ya Utume wa Nabii ‘Iysa (‘alayhis Salaam) na Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akiwa akifuata ibada ya masanamu, basi atakuwa miongoni mwa wa watu wa motoni. Hatakuwa na sababu kuwa ujumbe haukumfikia kwani mwito wa Nabii Ibraahiym na Mitume wengine utakuwa umewefikia ila wenyewe wamechagua kuabudu masanamu.

 

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ قَالَ : قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ  ((اسْتَأْذَنْتُ رَبِّي أَنْ أَسْتَغْفِرَ لأُمِّي فَلَمْ يَأْذَنْ لِي ، وَاسْتَأْذَنْتُهُ أَنْ أَزُورَ قَبْرَهَا فَأَذِنَ لِي ))  مسلم  

 

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Niliomba ruhusa kutoka kwa Allaah kumuombea msamaha mamangu, lakini Hakunipa ruhusa. Nikamuomba idhini nilizuru kaburi lake (mamangu), Naye Akanipatia ruhusa)) [Muslim]

 

Inaelezwa katika Kitabu cha ‘Awn al-Ma’abuud:

 

“Kauli yake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ((lakini Hakunipa ruhusa)) ina maana kuwa (mama yake) alikuwa kafiri na hairuhusiwi kumuombea maghfirah kafiri.”

 

 

 

Shaykh Ibn Baaz (Rahimahu Allaah):

 

“Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema ((Baba yangu na baba yako wako motoni)) amesema hivyo kwa elimu kwani yeye hasemi kwa matamanio yake ila kwa wahyi kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala):

 

((وَمَا يَنطِقُ عَنِ الْهَوَى))  (( إِنْ هُوَ إِلَّا وَحْيٌ يُوحَى))

 

((Wala hatamki kwa matamanio)) ((Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa)) [An-Najm: 3-4]

 

Ingelikuwa dalili haikupatikana dhidi ya ‘Abdulllaah bin ‘Abdul-Mutwalib, baba yake Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) asingelisema kama alivyosema kumhusu. Bila shaka amepata dalili dhidi yake (baba yake) kutokana na asili ya dini ya Ibraahiym kwa sababu walikuwa wakifuata dini ya Ibraahiym hadi uzushi ulipoanzishwa na ‘Amr bin Luhayy al-Khuzaa’i na uzushi wake ukasambaa kwa upana miongoni mwa watu kama uenezwaji wa masanamu na kuwaabudu badala ya Allaah. Labda ‘Abdullaah atakuwa amesikia lolote kumjulisha kwamba kuabudu kwa Maquraysh kulikuwa sio sawa lakini aliendelea kuwafuata na hivyo ni dalili ikapatikana dhidi yake.

 

Hali kadhalika Hadiyth ambayo Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) aliomba ruhusa kumuombea maghfira mama yake na akakataliwa, lakini alipoomba ruhusa ya kuzuru kaburi lake akaruhusiwa, labda naye atakuwa amesikia ndipo hoja ikasimama dhidi yake. Au huenda watu wakati wa Jaahiliyyah wanachukuliwe kwa mtazamo kuwa ni makafiri kama  ilivyo sheria ya dunia, hivyo tusiwaombee maghfira kwa sababu kidhahiri ni makafiri au kuwa kwao na makafiri na hivyo wanachukuliwa na kuhukumiwa  kwa mtazamo kama ni makafiri, Na hali yao kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anajua Atakavyowahukumu siku ya Qiyaamah” [Fataawa Nuur ‘alaa ad-Darb

 

Imaam As-Suyuutwiy ana rai yake kwamba wazazi wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wataokolewa (na moto) na kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliwarudishia uhai baada ya kufa kwao kisha wakamwamini (Mtume Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Rai hii imekanushwa na Maulamaa wengi ambao wamehukumu kwamba ni rai iliotokana na Hadiyth iliyozushwa au ni dhaifu sana. Miongoni mwa waliochambua kuwa ni dhaifu; Ad-Daaraqutwniy, Al-Jawzawaaniy, Ibn Shahiyn, Al-Khaatwib, Ibn ‘Asaakir, Ibn Naaswir, Ibn al-Jawziy, As-Suhayliy, Al-Qurtubiy, Atw-Twabariy, Ibn Taymiyyah na wengineo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share