Hikmah Ya Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Kwa Nini Tumswalie Ilhali Yeye Ametakaswa?
Hikmah Ya Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
Kwa Nini Tumswalie Ilhali Yeye Ametakaswa?
SWALI:
Assalama aleykum.
Namshukuru Allah kwa kutujaalia kuipata website yenye kutunyoosha juu ya dini yetu. Baraka za Allaah ziwaendee wote wenye kujihusisha na 'website hii', kila mmoja kwa kiwango apendacho Allaah.
Suali langu kwa leo ni hili: Nini hekima ya kumswalia mtume. Nahangaishwa na mawazo yangu kwamba Mtume ni mjumbe wa Allaah na ameshamtakasa na kila ovu na ameshamwahidi Pepo yake, kila zuri yeye ni kiongozi huko Akhera. Ameshatakasika, sasa kwa nini tunahitaji kumuombea ombea kila wakati na wengine hata hatuna kauli njema nini kumtaja-taja kipenzi cha Allaah. Nadhani sisi ndio tuko njia panda, hatujijui, tunahitaji kuombeana kila wakti.
naomba mafahamisho juu ya hekima iliyopo asante.
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kauli yako kuwa Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameshatakaswa na maovu na ameshaahidiwa Jannah (Pepo) na kadhalika, na kwamba sisi ndio tunaohitaji kuombeana yote hayo ni kweli kabisa. Lakini bila shaka umetatizwa kufahamu hikmah ya kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), basi tutakufahamisha kwa kadiri tunavyoelewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anajua zaidi
Kwanza Allaah ('Azza wa Jalla) Hatotuhitaji sisi tumuombee au tumswalie Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ikiwa sisi hatutopenda kufanya hivyo. Bali sisi ndiye wenye kumhitaji Allaah ('Azza wa Jalla) kwa kutaraji Neema Zake na kutupa fadhila kama hizo za kumuombea na kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa hiyo ikiwa tutampenda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au hatumpendi vile vile Rabb wetu hatuhitajii sisi tumpende Rasuli Wake kwani Yeye Mwenyewe pamoja Malaika wake Wanampenda na wamekwishatangulia kumswalia kabla ya kutuamrisha sisi kama Anavosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
إِنَّ اللَّـهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ ۚ يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﴿٥٦﴾
Hakika Allaah na Malaika Wake wanamswalia Nabiy. Enyi walioamini mswalieni na msalimieni kwa mamkizi ya amani na kwa tasliymaa. [Al-Ahzaab: 56]
Lakini kwa nini basi tumswalie Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)? Jibu la swali hakika ni refu sana itaweza kuwa ni makala ndefu au kitabu kizima cha mas-alah haya. Lakini tutafupisha ifuatavyo:
1. Kumtukuza Nabiy Wa Mwisho
Kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni katika kumtukuza kwani yeye ndiye Nabiy wa mwisho, na hii ni neema kwetu Ummah wa Kiislamu kujaaliwa sisi kuwa yeye ndiye Nabiy wetu. Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Ametuambia kuwa sisi ni Ummah bora kabisa. Bila ya yeye tusingeliweza kupata uongofu kamili (Qur-aan) na mafunzo ya Sunnah ambayo yametutoa kizani na kutuingiza katika nuru.
Na ikiwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Mwenyewe Amemtukuza kwa kumtofautisha na Manabii mingine wote, kwani wote Amewaita kwa majina yao katika Qur-aan isipokuwa
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) pekee Amemwita kwa kutaja cheo chake cha Unabii; Bonyeza kiungo kifuatacho upate faida:
Basi sisi kumswalia ndio mojawapo ya njia ya kumtukuza.
2. Ni ‘Ibaadah Kwetu:
Kwa vile ni amri kutoka kwa Rabb wetu kama tulivyoona katika Aayh hiyo ya juu, na ndio maana tunamswalia mpaka kwenye Swalaah zetu za fardhi na za Sunnah, na bila ya kumswalia Swalaah huwa haikamiliki.
3-Kudhihirisha Mapenzi yetu kwake
Muumini ni yule mwenye kumpenda kikweli Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kabla ya kupenda chochote hata nafsi yake kwani ilipoteremka Aayah hii:
النَّبِيُّ أَوْلَىٰ بِالْمُؤْمِنِينَ مِنْ أَنفُسِهِمْ ۖ
Nabiy ana haki zaidi kwa Waumini kuliko nafsi zao. Na wake zake ni mama zao. [Al-Ahzaab: 6]
'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alisema kuwa yeye anampenda Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuliko chochote ila nafsi yake. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia 'Umar kuwa hadi ampende hata kuliko nafsi yake ndipo yatakapothibitika mapenzi yake, naye 'Umar akakubali kuwa anampenda kuliko hata nafsi yake. Kwa hiyo na sisi Waumini tuwe na mapenzi makubwa ya kumpenda na dalili mojawapo ni kupenda kumswalia na kufuata aliyokuja nayo na kujiepusha na aliyotukataza nayo ya uzushi (bid’ah) na mengine.
4. Ni Rahmah Kwetu Kuchuma Fadhila Na Thawabu Tele:
Mwana-Aadam kila siku ana makosa hata awe anafanya ‘ibaadah kwa wingi vipi, kwa hiyo ni neema kwetu kuzidishiwa fadhila kwa kutekeleza ‘amali za Sunnah fulani ili kujiongezea thawabu na kujaaliwa daraja za Jannah (Pepo) kwani hakuna mtu asiyependa ziada ya neema.
5. Kumswalia Kwetu Ni Thawabu Alizokwishaahidiwa
Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekwishamuahidi Rasuli Wake kuwa atapata malipo mengi yasiyokatika, Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):
وَإِنَّ لَكَ لَأَجْرًا غَيْرَ مَمْنُونٍ ﴿٣﴾
Na hakika wewe bila shaka una ujira usiokatika. [Al-Qalam: 3]
Mbali ya kuwa ni ujira tele kwake kwa sababu ya Unabii wake na kufikisha Risaala kwa tabu na mashaka, vile vile kumswalia kwetu kila siku katika Swalaah zetu kila mara, na kuswaliwa na Ummah mzima wa Kiislaamu tokea Unabii wake hadi siku Qiyaamah ni mojawapo ya kuthibitisha kauli hiyo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). Kwa faida zaidi kuhusiana na nukta hii bonyeza kiungo kifuatacho:
33-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Ana Ujira Usiokatika Anasifika Na Maarufu Mno
Bonyeza viungo vifuatavyo upate faida tele nyenginezo na maelezo bayana kabisa ya hikma na fadhila za kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
Maana Ya Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
Fadhila Za Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Vipi Kumswalia
Kumpenda Kikweli Nabiy (صلي الله عليه وسلم)
Kumpenda Nabiy ﷺ Ni Kumtii Na Kumfuata
13-Fadhila Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم): Waumini Wanapaswa Kumpenda Kuliko Nafsi Zao
082-Lu-ulu-un-Manthuwrun: Fadhila Za Siku Ya Ijumaa Na Kumswalia Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)
Mwisho kama ulivyosema kuwa sisi ndio tuliokuwa njia panda na tunaohitaji kuombeana, bila shaka tunahitaji kufanya hivyo, na kwa hiyo pia kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni kutuzidishia uzito wa Mizani zetu za mambo mema na kufanya nyepesi Mizani ya mambo maovu Siku ya Qiyaamah.
Na Allaah Anajua zaidi