Hadiyth Ya Kuteremka Allaah Thuluthi Ya Mwisho Ya Usiku Na Aayah: وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ
Usahihi Wa Hadiyth Ya Kuteremka Allaah Thuluthi Ya Mwisho Ya Usiku,
Na Aayah
وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ
“Na Sisi Tuko Karibu Naye Kuliko Mshipa Wa Shingo
SWALI:
assalam aleykum warahmatullah wabarakatu
swali langu ni hili. je hadithi hii ni ya kweli? Kuwa Allaah hushuka katika robo tatu ya usiku akinadi aliye na haja ya kusamehewa aombe? kama kweli vipi kuhusu aya inayosema alla yu karibu kuliko mshipa mkubwa wa fahamu?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika ni kuwa Hadiyth hiyo ipo ni sahihi kabisa nayo ni kama ifuatavyo:
عنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ: ((يَنْزِلُ رَبُّنَا تَبَارَكَ وَتَعَالَى كُلَّ لَيْلَةٍ إِلَى السَّمَاءِ الدُّنْيَا حِينَ يَبْقَى ثُلُثُ اللَّيْلِ الْآخِرُ يَقُولُ: مَنْ يَدْعُونِي فَأَسْتَجِيبَ لَهُ، مَنْ يَسْأَلُنِي فَأُعْطِيَهُ، مَنْ يَسْتَغْفِرُنِي فَأَغْفِرَ لَهُ)) البخاري و مسلم
Imepokelewa kutoka kwa Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa Huteremka (kwa namna inavyolingana na utukufu Wake) kila siku katika mbingu ya dunia inapobakia thuluthi ya mwisho ya usiku na Husema: Nani ananiomba du’aa Nimuitike? Nani Ananiomba jambo Nimpe? Nani ananiomba maghfirah Nimghufurie?)) [Al-Bukhaariy, Muslim]
Imenukuliwa na al-Jama’ah, kumaanisha Ma-Imaam Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah.
Ama kuhusu Aayah uliyoitaja iliyoko katika Suwrah Qaaf Namba 50 Aayah Namba 16 ambayo Allaahs Subhaanah wa Ta’aala Anasema:
وَنَحْنُ أَقْرَبُ إِلَيْهِ مِنْ حَبْلِ الْوَرِيدِ
"Na Sisi Tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake."
inatufahamisha kuwa Allaah ('Azza wa Jalla) yuko karibu sana nasi kwa elimu Yake na hivyo hatuna haja ya kupiga makelele tunapoomba. Yeye Anasikia vilio na maombi yetu yote. Hivyo, Aayah hii na Hadiyth hazigongani kabisa.
Na hayo ni majibu kwa mukhtasari tu.
Na Allaah Anajua zaidi