Barua Za Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Zimehifadhika Hadi Leo?
SWALI:
Assalamu aleikum
Ni kweli zipo mpaka leo barua za mtume wetu{s.a.w} alizowaandikia wafalme wa Kisra na wa Habasha na wa Rumi alizoziandika kwa mkono wake? kwa sababu mimi nilizipata katika site fulani,na zimeandikwa kwa kiarabu na kwamba zimehifadhiwa tokea zama hizo mpaka leo,na pia muna picha za makaburi ya mashuhadaa, je ni kweli zimehifadhiwa? Na hizi nilizonazo ndizo? Shukra
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allahu 'anhum jamiy'an) na watangu wema mpaka Siku ya Qiyaamah.
Shukran kwa swali lako hilo kuhusu barua za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizowaandikia wafalme, watemi, maliwali, masultani wa wakati wake kuwaita katika Dini ya Uislamu.
Kabla ya kuingia katika swali hilo, mwanzo tunapenda kurekebisha kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa Ummiy (asiyejua kusoma wala kuandika), hivyo alikuwa na waandishi wake wa kuandika barua na si yeye mwenyewe. Hii ni kwa mujibu wa ayah inayosema: “Ambao wanamfuata Mtume, Nabii aliye Ummiy” (7: 157).
Barua hizo zilizoandikwa kupelekewa wakubwa kadhaa wa dola tofauti kwa mfano, Najjaashiy mfalme wa Ethiopia, Muqawqisw mfalme wa Misri, Kisra mfalme wa Uajemi, Qayswar mfalme wa Roma, kwa mfalme wa Oman na watemi kama al-Mundhir ibn Saawiy, Hawdhah ibn ‘Aliy al-Haarith ibn Abi Shamr al-Ghassaaniy na wengineo. Hizi barua zimehifadhiwa kwani zilinukuliwa katika vitabu vya Hadiyth kama Swahiyh al-Bukhaariy na vitabu vya Siyrah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kitu cha wewe kufanya ni kuangalia hiyo nuskha uliyoipata katika tovuti na zile barua zilizoandikwa katika kitabu maarufu cha Sirah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kinachoitwa ar-Rahyiqul Makhtuum kilichoandikwa na Shaykh Swafiyyur-Rahmaan al-Mubaarakpuri kuanzia ukurasa wa 392 – 405. Kitabu hiki kimetarjumiwa kwa lugha ya Kiingereza na pia Kiswahili.
Hakuna la ajabu ikiwa barua hiyo imehifadhika hadi leo kwani inakuwa ni kurasa moja peke yake. ni jambo lenye kujulikana kuwa kati ya misahafu kadhaa iliyoandikwa katika ukhalifa wa ‘Uthmaan (Radhiya Llaahu ‘anhu) mmoja mpaka sasa unapatikana Tashkent na mwengine Uturuki.
Lakini barua na picha za upanga, picha za unywele wa ndevu na mengineyo yanayodaiwa kuwa ni ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambazo zinasambazwa sana kwenye mtandao ‘internet’, ni mambo yasiyo na ukweli wala ushahidi, yamezushwa tu na baadhi ya watu hasa walio bara Hindi kwa ‘hawaa’ zao binafsi.
Na Allah Anajua zaidi