Hadiyth Ya Allaah Kumsamehe Mja Mpaka Miaka Sitini Ina Khitilafu?

SWALI:

 

Ssalam Alaikum Warahmatullahi Wabarakatuh

 

Nashukuru kwa kazi nzuri na yenye manufaa kuhusu imani yetu na ni mengi tuyapatayo kuhusu dini yetu sahihi. Mwenyezi Mungu Azza wa Jalla Awalipe mema na Aikithirishe ALHIDAAYA.

 

SWALI: Kuna hadith katika Riyadhul Swalihiin, Abu Hurairah anasema Mtume Muhammad Rehema na Amani Zimshukie amesema, “Mwenyezi Mungu anamsamehe Mja wake mpaka miaka sitini" (Bukhari). ILIZUA MABISHANO MSIKITINI KUWA HII HADITH INA KHALIFU SIFA YA ALLAH, TUUSIE INSHALLAH

 

Wa Billahi Tawfiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu Hadiyth uliyoitaja. Hadiyth hiyo ipo pia katika Riyaadh asw-Swaalihiyn, mlango wa 12, Hadiyth namba 112. Hata hivyo, swali lako halipo wazi kabisa kwani mwisho umesema Hadiyth inakhalifu sifa ya Allaah bila kututajia sifa yenyewe.

 

Tukija katika Hadiyth hiyo labda tukiifasiri kama ilivyo kutoka katika Kiarabu huenda tukaondosha utata wote. Maana ya Hadiyth yenyewe ni, “Allaah lau Atamcheleweshea mja mpaka afike miaka sitini, hatakuwa na udhuru wowote (wa kutotubia kutokana na madhambi yake)”. Wanachuoni wamesema kuwa maana ya Hadiyth hii ni, “Hatakuwa na udhuru mja kama huyo ikiwa ataachiliwa mpaka afike umri huo”. Kwa hivyo, maana ya Hadiyth itakuwa inafaa kwa mja na hasa Muislamu awe ni mwenye kutubia kwa madhambi yake asiwe ni mwenye kungoja mpaka akafika miaka sitini, guu kaburini.

Kwa hiyo, hapo hakuna kinachopinga au kukhalifu sifa ya Allaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share