Ukusanyaji Wa Hadiyth Na Ikhtilaaf Zake
SWALI:
Assalaam aleikum.
Hongereni kwa kazi kubwa mnayofanya ya kuelimisha ummah. Allaah atawalipa kila la kheri.
YAH: UANDISHI WA HADITH ZA MTUME
Naomba kufahamishwa kuhusiana na kuwepo kwa RUHUSA AU MARUFUKU YA KUANDIKA HADITH ZA MTUME MUHAMMAD (SAW).
- Je ni kweli kuwa katika vitabu vinavyotegemewa vya hadith kuna hadith zenye kugongana maudhui yake?
- Naomba mninukulie (quote) Hadith zinazodaiwa (a) KUKATAZA KUANDIKWA KWA HADITH (b) KURUHUSIWA KUANDIKWA KWA HADITH (c) KUTABIRI KUWA ITAFIKA ZAMA WATU WATAMSINGIZIA MTUME KUWA KASEMA KADHA WA KADHA, yapimeni maelezo hayo kwa Qur-aan.
Nikitaraji mtanijibu kwa haraka, Natanguliza shukrani
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muuliza swali kuhusu mas-ala ya Hadiyth.
Tunapozungumzia Hadiyth Ki-Istilahi basi huwa inamaanisha kauli, vitendo na yaliyofanywa mbele ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) naye asikataze. Hii ni taarifu fupi kuhusu Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ama tukija katika maswali yako tunasema yafuatayo:
1. Ni kweli zipo Hadiyth katika vitabu vya Hadiyth vinavyotegemewa ambavyo dhahiri yake inaonyesha kugongana. Hili ni jambo ambalo liko dhahiri na halina utata wowote miongoni mwa wanachuoni na wanafunzi wa elimu. Lakini utata na kugongana huko kunaondoka pale tunapoelewa ima dhumuni za Hadiyth hizo, wakati ziliposemwa, kupo kufuta na kufutwa kwa hukumu (yaani zipo hukumu ambazo zilikuwa awali kwa sababu moja au nyingine kisha hukumu hiyo ikabatilishwa), kupata maelezo yake na kadhalika.
Huenda tukaeleweka lau tutatoa baadhi ya mifano katika mada hii. Mfano wa kwanza ni kule kukatazwa Waislamu kuzuru makaburi na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na baadaye kuruhusiwa. Hii ilikuwa ni kwa sababu ndio watu wameingia katika Uislamu na walikuwa na ada ya kuabudu waliokufa walioonekana kuwa ni watukufu. Baada ya Imani kukita ndani ya vifua vyao waliruhusiwa hilo na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatoa sababu yake. Anasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Nilikuwa nimewakataza kuzuru makaburi, sasa zuruni kwani hilo linawakumbusha nyinyi Akhera” (Muslim).
Ama mfano mwingine ni kukatazwa kunywa maji kusimama na kuruhusiwa kwake. Zipo Hadiyth ambazo zinakataza, kisha kukaruhusiwa kunywa maji kusimama kwa kufanya hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mwenyewe. Miongoni mwa Hadiyth inayokataza ni ile iliyopokewa kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asinywe mmoja wenu kwa kusimama, na anayesahau basi ajitapishe” (Muslim). Ilhali zile zenye kuruhusu ni kama zifuatazo:
Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Nilimpa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maji ya Zamzam akanywa huku amesimama” (Al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na an-Nasa’iy).
An-Nazzaal bin Sabrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema: Alikuja ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwenye mlango wa Rahbah (sehemu pana iliyopo Kufah) na akanywa akiwa amesimama, na akasema: “Hakika mimi nimemuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifanya kama munavyoniona nikifanya” (Al-Bukhaariy, Abu Daawuud na an-Nasaaiy).
Na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Tulikuwa tukila katika zama za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nasi twatembea na tukinywa nasi tumesimama” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Sahiyh. Pia imenukuliwa na Ahmad, Ibn Maajah na ad-Daarimiy. Isnadi yake ni Hasan).
Na imepokewa kwa ‘Amru bin Shu‘ayb kutoka kwa babake kutoka kwa babu yake (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: “Nilimuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinywa kwa kusimama na kwa kukaa” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadith Hasan Sahiih. Na imenukuliwa na Ibn Maajah na Isnadi yake ni Hasan. Pia ipo kwa Ahmad kwa njia nyengine kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu). Hivyo Hadiyth ni Sahihi).
Hadiyth hizi zinaonekana kuwa zinagongana lakini Imaam an-Nawawiy yeye amezifasiri Hadiyth hizi kwa kuziwekea mlango wa 114 katika kitabu chake Riyaadh asw-Swalihiin wenye kichwa cha habari “KUBAINISHA KUJUZU KUNYWA KWA KUSIMAMA
Kugongana kwengine ni kule kunakopatikana kwa sababu ya utumiaji wa Hadiyth dhaifu au Mawdhu’u (za kutungwa) na hapa ndipo tunakotakiwa kuwa na tahadhari kubwa zaidi. Mfano mmoja wa aina hii ni kule kusingiziwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa alisema kuwaambia Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipokuwa wametoka kutoka katika Jihadi ya vita: “Mumetoka katika Jihadi ndogo na kuja kwenye Jihadi kubwa”. Akaulizwa: “Ni ipi Jihadi kubwa?” Akasema: “Jihadi an-Nafs (kupigana na nafsi)”. Hii inapingana na Qur-aan na Hadiyth nyingi sahihi zinazotufahamisha kuwa Jihadi ya kupigana ndio amali kubwa baada ya kumuamini Allaah na Mtume Wake.
Tunatumai hii mifano mitatu imetuweka sawa katika hilo.
2. Ama kukatazwa kuandika Hadiyth na kuruhusiwa ni suala linalofanana na mifano ya hapo juu katika jawabu la swali la kwanza na InshaAllaah tutatoa dondoo kuhusu hayo.
Utata wa suala hili unakuja kwa sababu wapinzani ambao ni wataalamu wa mambo ya Mashariki (orientalists) na baadhi ya Waislamu wasio na Imani thabiti mara nyingi hujaribu kutia shaka kuhusu usahihi wa Hadiyth ili kuitweza Sheria na kuipaka matope hadhi na Siyrah ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wao wanadai kuwa Hadiyth zimekuwa ni mambo yaliyopokelewa baada ya Mtume kwa muda mrefu, kisha wakadai kuwa ni kwa muda mfupi tu zimekusanywa kama kiasi cha karne mbili hivi. Wataalamu hawa kama Sir Wiliam Muir na Ignaz Goldziher, wameleta kwa pamoja uwezakano mkubwa wa shaka kuhusu usahihi wa Hadiyth katika uandishi na ukusanyaji. Wengine kama Schacht wakashutumu kuwa isnadi zilizuliwa baadaye.
Lakini msomi, Sayyid Sulaymaan an-Nadwi katika kitabu chake amezijibu tuhuma hizi ambazo pia itakuwa ndio jibu letu kuhusu masuala yako. Amesema: “Kuna kumbukumbu kadhaa zenye kuonyesha kuwa amri na mazungumzo, matukio na matendo yanayohusiana na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yalikusanywa hata katika uhai wake. Wakati wa kutekwa Makkah kwa amani, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitoa hotuba. Al-Bukhaariy anaripoti kuwa kwa maombi ya Abu Shah (Radhiya Allaahu ‘anhu), Swahaba kutoka Yemen, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliamuru hotuba hiyo aandikiwe.
Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) alisikika wakati mmoja akisema kuwa hakuna mtu mwingine isipokuwa ‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ndiye mwenye mkusanyiko mkubwa zaidi wa Hadiyth. Sababu yake ni kuwa Ibn ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikuwa akiandika yale aliyokuwa akiyasikia kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na yeye alikuwa hafanyi hivyo. Maswahaba wengine walikataa hii desturi ya kuandika. Ibn ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alimzungumzia jambo hilo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye aliashiria kwenye mdomo wake na kusema: ‘Unaweza kuandika yote yenye kutoka hapa kuwa ni ya uadilifu na ya haki’.
Kitabu cha Hadiyth kilichoandikwa na Ibn ‘Amr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) kinajulikana kama Swaadiqah. Khalifah ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) pia alikuwa na nyaraka zilizoandikwa Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hukumu za Sheria.
Wakati mmoja Khalifah ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliwauliza watu kuhusu matendo ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika malipo ya pesa kwa wajane baada ya waume zao kuuliwa. Adh-Dhahhaak bin Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alilijibu suala hilo kwa kutumia waraka ambao ulitumwa kwa kabila lake na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) {ad-Daraqutniy}.
Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alikusanya Hadiyth baada ya kupatiwa ruhusa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) amepata hadhi ya kuzisambaza Hadiyth nyingi zaidi miongoni mwa Maswahaba. Mwanafunzi wake mmoja, Hammaam bin Munabbih alikusanya Hadiyth alizojifunza kutoka kwa mwalimu wake, ambayo inajulikana kama Swahiyfah Hammaam. Swahiyfah hii imeungishwa kwenye mjalada wa pili wa Musnad ya Imaam Ahmad bin Hambal.
Baada ya kutawazishwa Uamiri wa Waislamu, ‘Umar bin ‘Abdul-‘Aziyz (99-101 H), yeye mwenyewe akiwa msomi alimtumia ujumbe Qaadhi Abubakar bin Muhammad bin ‘Amr bin Hazm al-Answaariy (k. 117 H) akisema: “Anza kukusanya Hadiyth za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani nahofia hizi huenda zikapotea pole pole” (ad-Daarimiy). Qaadhi Abubakar alikusanya ripoti zote zilizokuwepo na kuzipeleka kwa Amiri huyo. Nakala zilipelekwa miji yote mikubwa ya mikoa katika Dola ya Kiislamu. Qaadhi Abubakar alichaguliwa hasa kwa kazi hii kwani yeye alikuwa ni Qaadhi wa Madiynah na mamake mdogo (halati) ‘Amrah alikuwa mwanafunzi mkubwa wa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Qaadhi Abubakar alikuwa ameandika kila halati yake alichojifunza kutoka kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha).
Hamu na hamasa zilizoonyeshwa na Maswahaba, Tabi‘in na waliowafuata kwa wema katika kusoma, kuandika na kusomesha Hadiyth ilitokana kwa mkazo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema: ‘Fikisheni ujumbe kutoka kwangu hata kama ni ayah moja’ (al-Bukhaariy).
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kusisitiza kusambazwa kwa maneno na vitendo vyake ameonya kuwa: ‘…Yeyote atakayegeuza mafundisho au kusambaza ripoti za uwongo kuhusu mimi basi makao yake ni Motoni’ (al-Bukhaariy)” {Muhammad – The Ideal Prophet}.
Abu Qaabiyl amesema: Tulikuwa na ‘Abdullaah bin ‘Amr bin al-‘Aasw (Radhiya Allaahu ‘Anhuma) akaulizwa: “Ni mji ambao utafunguliwa mwanzo Constantinople (Istanbul) au Roma?” Hivyo, ‘Abdullaah akaitisha sanduku lililofungwa na akasema: Akachukua kitabu ndani yake. Kisha akasema: “Tulipokuwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiandika, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Ni mji gani utakaofunguliwa mwanzo, Constantinople au Roma?” Hapo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Mji wa Heraclius utafunguliwa mwanzo, akimaanisha Constantinople” (Imaam Ahmad, ad-Daarimiy na al-Haakim).
Sayyid Sulaymaan an-Nadwi anatupatia mifano ya watu wacha Mungu ambao walikataa rushwa ili wazue Hadiyth na kukataa kauli za baba zao kwa sababu moja au nyingine: “Imaam Wak‘iy alikuwa Muhaddith ambaye babake alikuwa mshika hazina wa Dola. Wak‘iy alikuwa akizikubali Hadiyth kutoka kwa babake tu alipata mpokezi mwingine muaminifu na mapokezi sawa na ya babake na kuyakataa ikiwa yamepokewa na babake tu. Wakati mmoja Mu‘adh bin Mu‘adh alipewa dinari elfu kumi za dhahabu ili asitowe ushahidi kuhusu uaminifu au uwongo wa mtu Fulani, lakini alikataa ofa hiyo kwa kusema: ‘Siwezi kuficha yaliyo sawa’. Je, kuna mfano wowote wa ukweli na ushupavu katika nyaraka za historia ya mataifa mengine?” (Muhammad – The Ideal Prophet, uk. 102-103).
Huenda ikawa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekataza kuandikwa kwa Hadiyth ili sizichanganikane na Qur-aan au kwa sababu nyingine yoyote hapo awali lakini baadaye akaruhusu kuandikwa kama tulivyoona hapo juu.
Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametabiri mambo mengi miongoni mwayo ni kuwa watakuja watu ambao watamzulia mambo. Ishara hii ipo katika Hadiyth zake kadhaa, miongoni mwazo ni:
- Imepokewa na ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Msiniongopee kwani anayeniongopea kwa kukusudia ataingia motoni”.
- Anas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Atakayeniongopea kwa makusudi basi ajiandalie makazi yake motoni”.
- Imepokewa kwa Abu Hurayrah kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amesema: “Anayeniongopea kwa makusudi basi ajiandalie makazi yake motoni”.
Hadiyth zote hizi zimenukuliwa na al-Bukhaariy na Muslim.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atuongoze katika njia ya sawa na Atupatie hima ya kuweza kuifuata.
Na Allaah Anajua zaidi