Zingatio: Sisi Tutaingia Peponi?
Sisi Tutaingia Peponi?
Naaswir Haamid
Hili ni suala ambalo kila mmoja wetu yabidi ajiulize kwa dhati ya nafsi yake bila ya kujiongopea: “Hivi vitendo na maisha yalivyo sasa kweli nitakuwa ni miongoni mwa watakaonusurika na Moto?”. Allaah Atuepushe na huo Moto.
Bila ya Muislamu kujiuliza hilo suala, huwenda akajisahau na kuchanganya yaliyo halali na haramu. Kwani tabia na mila za hapo kale takriban zote zimetoweka. Wanawake zama za utiifu na heshima walikuwa wakivaa nguo za kujistiri. Tabii hii haikuwa kwa Uislamu tu, bali hata kwa nchi za Magharibi. Bahati mbaya, Magharibi wameanza kuukana utu na huku Waislamu wakiendelea kuufuata mkondo huo huo.
Maisha yetu ni yenye kila aina ya mushkel wa chakula na vivazi vyetu. Inafikia hadi kwamba tunayoyaomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Hatukubalii kwa sababu ya uharamiyya wetu. Kutokana na Hadiyth iliyopokelewa na Abuu Hurayrah ya (mtu aliyekwenda safarini akachoka na kujaa vumbi, kisha akanyanyua mikono juu na kuomba "Ewe Mola, Ewe Mola" lakini chakula chake ni haraam, kinywaji chake ni haraam na mavazi yake ni haraam, amerutubishwa kwa haraam, vipi atatakabliwa?)) [Muslim]
Hali yaenda mbali zaidi kwa kushiriki riba, uzinzi, uongo, ulevi, utapeli na mengineyo mengi. Wengine wamezua vitendo vya kizushi na ambavyo havipatikani ndani ya Uislamu na kuzitetea kinaga ubaga kwamba ni ibaadah. Hata yale yanayotegemewa kuwa ni halali huingizwa chembe chembe za uharamu. Masikitiko makubwa ni kwamba mambo yamekorogeka wakati ambao elimu imekuwa wazi kuliko zama nyengine! Mfano ni mawasiliano ya umeme (e-com) ambazo zina muziki, uzushi, ukafiri, picha zisizofaa na kadhalika. Hata watu wenye ‘ilmu sahihi ya Uislamu wamejikuta wanakusanya dhambi ndani ya mzunguko huu bila ya kutarajia.
Taariykh inatuonesha namna Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alivyokuwa akiamka usiku. Usiku ambao alikuwa akikesha na Mola wake huku akilia na akisimama kisimamo kirefu hadi miguu kuvimba! Wakafuatia Maswahabah (Radhiya Allaahu ‘Anhum) ambao wanapotoka kwenda kuswali alfajiri walionekana kuwa na alama za kukesha usiku. Sasa tukae na tujiulize vizuri. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwa na dhambi na hizo ni shukrani zake tu kwa Mola wake. Maswahabah wengi wacha Mungu ni walio bashiriwa pepo, lakini wakiamka usiku na pia wakishindana kutenda mema. Peponi tutaingia sisi? Tumelala fofofo usiku na mchana. Hadi yaje mauti ndio tuamke?
Wanawake kama Bibi ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha) walikuwa ni wacha Mungu mno, lakini hata hivyo sio miongoni mwa waliotajwa kuwa ni wanawake walio wakamilifu. Ni wanawake wanne tu waliosimuliwa kuwa ni wakamilifu ambao ni Bibi Asya, Maryam, Khadiyjah na Faatwimah (Radhiya Allaahu ‘Anhunna). Jee, sisi tunajiweka ndani ya kundi gani? Inasemekana kwamba Bibi ‘Aaishah aliwahi kuswali dhuhaa huku akilia na kurudia tena na tena aya ifuatayo kwa zaidi ya nusu saa:
“Hakika sisi tulikuwa kabla kwenye ahli zetu wenye kuogopa. Basi Allaah Akatufadhilisha, na Akatuokoa na adhabu ya moto unaobabua [At-Twuur: 26-27]
Hata hivyo, tusivunjike moyo na wala tusikate tamaa kwa rehma za Mola wetu. Huyo sie Muislamu aliye na imani ya kweli. Cha muhimu ni kuwa na jitihada na ikhlaasw ya kweli, sio leo tunatubia kesho tupo pamoja na washirikiyna. Pia, Mtume anaupenda ummah wake, kwani ametuwekea wazi yaliyo haramu na halali. Tushikamane na njia hiyo aliyoamrishwa Mtume kuifikisha kwetu kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).