Anapotukanwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Muislamu Afanyeje?

SWALI:
Mimi ninauliza swali tu jee kama sisi ni waislamu wa kweli tufanye nini baada ya kutukanwa kwa kipenzi chetu Mtume Muhammad sw 
 


 
 
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea.
 
Shukrani zetu za dhati kwa maswali yako mawili. Ama kuhusu swali lako la kwanza ni kuwa yapo mengi ya kufanywa baada ya kutukanwa kwa kipenzi chetu, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hakika yapo mengi ambao tunaweza kufanya katika hilo, lakini mwanzo na awali ya yote ni lazima turekebishe yaliyomo nyoyoni mwetu. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kutezwa namna hiyo ila sisi ndio tumemshusha hadhi yake. Huku kukosewa heshima mara nyingi hutokana na makosa yetu wenyewe na mara nyengine utakuta nchi inayojiita ni ya Kiislamu imefanya jambo kama la kuchora picha wanazodai ni za Mtume au Maimaam wao 12 na hata kuwatengenezea sinema Manabii, lakini sisi tukanyamaza kimya. Hawa nao wasiokuwa Waislamu wakaiga hilo na kuzidisha kwa kuzichora kwa kuongeza udhalilishaji, mbali na kuwa hiyo haiwezi kuwa ni sababu yao msingi.
 
Yale tunayoweza kuyafanya ni kama yafuatayo:
1.    Tujue Siyrah (maisha) yake kama inavyohitajika kwa Muislamu.
2.    Tufuate Sunnah zake kimatendo pamoja na kuwafikishia wengine hasa Waislamu, nao waige mfano wake.
3.    Kuwaelimisha wasio Waislamu kwa njia tofauti za utangazaji na uandishi waweze kumjua Mtume ukweli wa kumjua, na pia kuandaa mihadhara mbalimbali na mafunzo kwa ajili ya Waislamu ambao pia kuna baadhi hawafahamu heshima na hadhi ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kikamilifu na kisawasawa.
4.    Kugawa vijitabu au vipeperushi kwa lugha tofauti kwa wasiokuwa Waislamu kuhusu maisha ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). 
5.    Kuwa na vipindi katika idhaa za Radio na kurasa katika magazeti za kumtambulisha na kuelezea sifa zake tukufu.
6.    Kususia bidhaa za nchi zilizofanya madhila hayo.
 
Na Allaah Anajua zaidi

Share