Nataka Kuolewa Na Kijana Nimpendaye Lakini Wazazi Hawatakubali Kwa Ajili ya Ukabila Na Rangi.

SWALI:

 

A. Aleykum! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 21 na hapa karibuni nimepata mchumba anataka kunioa lakini kuna tatizo moja kabila, na wazazi wangu nauhakika hawatakubali mimi kuolewa naye..Nampenda huyo kijana maana Allaah habagui rangi wa kabila sisi wote ni wa kwake..Sheikh sipendi kuwaudhi wazazi wangu nawapenda na kuwaheshimu sana na sitaki kumkosea Allaah kama alivyo sema ti wazazi wako lakini usiwati pale ambapo utanikosea mimi..! Je sheria ya kiislam inasemaaje kuhusu hilo?? Nikiwapinga wazazi wangu nitapata dhambi? Nisaidie na ndoa hiyo itakuwa na kheri na baraka ndani yake bila ya baraka toka kwa wazazi? Asante naomba nijibu soon! (Nisamehe kama kiswahili changu hakieleweki..Sijui kandika vzuri Kiswahili)


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika  Salaam hazifai kufupishwa kwa kuandikwa (A.A) au (A.A.W.W.) au kama ulivyoandika kwani haijafundishwa hivyo na pia ni kujikosesha fadhila za Salaam kama tulivyoelezwa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo nayo tujizoeshe kuandika (Assalaamu ‘alaykum) au (Assalaamu ‘alaykum wa rahmatullaah) au (Assalaamu ‘alaykum wa Rahmatullaah wa Barakaatuh) kwa ukamilifu na tutakuwa tumeiga mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na pia tutakuwa tumezoa thawabu zote za Salaam kama tulivyofundishwa. Na Mafunzo yote na fadhila zake zimo Alhidaaya katika kiungo kifuatacho: Maamkizi Ya Kiislamu.  

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu posa na ndoa kwa kijana asiyekuwa kabila lako. Na kulikuwa hakuna haja kwako kuomba msamaha kwa Kiswahili ulichoandika kwani swali hilo lamefahamika vyema.

 

Utata uliopo ni kuwa tayari wewe umeamua kuwa wazazi watakataa posa ya kijana huyo hata kabla ya wazazi wake kuja kuposa. Inatakiwa dada yetu hata kabla ya kuwa na rai hiyo umwambie huyo kijana awaambie wazazi wake wakapeleke posa rasmi kwenu. Nyinyi lenu ni kungojea majibu yatakayotoka huko. Hatujui maoni yako umeyatoa kwa sababu alikuja mtu wa kabla jingine akakataliwa au maoni yako yamefungamanishwa kwa kuwajua kuwa wazazi wako ni wabaguzi? Mara nyingi huwa tunakosea katika hilo au huwa tuna nadhariya ambazo hazijajaribiwa. Kwa hiyo, no bora kujaribu na kumwachia Allaah ambaye Ndiye mwenye maamuzi.

 

Waache wazazi wakatae baada ya kuwa wazazi wa kijana wamekwenda kwa njia ya halali. Wala wewe usichukue hatua yoyote kwa wakati wote huo na uwe ni mwenye kuwatii kwa yote. Hata hivyo, labda tukuulize swali kidogo kuhusu hilo: Huyu kijana umpendaye, umependezwa na nini? Je, Dini na maadili yake ni ya Kiislamu? Au unampenda kwa sababu ya uzuri au mali au mumeshaanza mahusiano yasiyo ya kisheria? Ikiwa unampenda kwa sababu ya Dina na maadili yake basi tutakupatia ushauri wetu chini. Lau itakuwa unampenda kwa ajili ya uzuri au mali au mengineyo, basi nasaha zetu kwako ni achana naye haraka kabisa wala usijisumbue kwani utakwenda kupata matatizo ya bure.

 

Pia, je huyo kijana mwenyewe anataka kukuoa au wewe unamlazimisha?

Kuwa na maisha mazuri katika ndoa ni lazima kijana mwenyewe awe naye anakupenda, ikiwa ni kinyume na hivyo, kijana huyo atakutumia bure.

 

Ikiwa kijana ameshika Dini na anataka kuja kuposa sio kukuchezea na kisha kukutupa, tutaweza kukupatia ushauri katika hilo. Ushauri wetu ni kama ufuatavyo:

 

  • Swali Swalah ya Istikhaarah umtake ushauri Allaah Aliyetukuka.

  • Waache wazazi wa kijana waje kuposa rasmi kwa wazazi wako.

  • Ikiwa wazazi wote wako watakataa kwa sababu ya ukabila basi jaribu kuzungumza na jamaa zako ambao wanakuelewa ili waweze kuwakinaisha wazazi wako kuhusu hilo.

  • Ikiwa hilo halikufanikiwa basi msichukue sheria mikononi mwenu bali inabidi muende kwa Qaadhi kupeleka malalamiko yenu. Qaadhi au Shaykh wa mji mnaokaa atawaita wazazi kuwasikiliza hoja walizo nazo kuhusu kukataa kwao. Ikiwa wazazi wana hoja nzito basi hata Qaadhi ndoa hiyo hataifungisha. Ikiwa wazazi hawana hoja ya kisheria, Qaadhi atabeba jukumu la uwalii na kuwaozesha nyinyi.

 

Tunalohofia ikiwa uko sawa kutowafuata wazazi si laana kwani laana ya batili haimfikii mtu, lakini ni kutokuwa na kinga wewe kijana wa kike. Wanaume wanaeleweka, wengi wao ni wazuri na wengi pia ni wabaya wasiokuwa na misimamo ya sawa na ya kidini. Mwanamme kawaida anamdharau mwanamke ambaye amewaasi wazazi na kumfuata yeye. Tumepata mashtaka mengi ya kuteswa wanawake kama hao kwa sababu ya kutokuwa na kimbilio. Mume leo ni wako kesho si wako. Tatizo likitokea wewe utakimbilia wapi na wazazi watakuwa wamekupiga vita. Zingatia na ufikirie sana kuhusu hilo. Ndoa yako ukiozeshwa na Qaadhi itakuwa sahihi kabisa kisheria lakini kwa thamani gani.

 

Hata ndoa ikifaulu watoto wenu watakuwa na raha gani ikiwa hawawezi kuwazuru mababu na mabibi zao. Kuwa makini, wewe kutoolewa na kijana huyo sio mwisho wa ulimwengu. Wakikataa wazazi wewe hutalaumiwa na Allaah Aliyetukuka bali wao ndio watakaopata madhambi kwa hilo ikiwa hawana sababu.

 

Usifanye uamuzi wa haraka na tunamuomba Allaah Aliyetukuka ikiwa mume huyo ana kheri nawe Akusahilishie mambo yako na aifanye harusi na tangamano la kheri. Ikiwa si kheri nawe basi Akuepushie mbali sana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share