Kuwapeleka Watoto Swimming Pool Kwenye Mchanganyiko Wa Wanaume Na Wanawake

SWALI:

 

Asalam Alykum Warahmatullah.

Napenda kuwapongeza kwa kutuwekea web hii kwani imetunufaisha kwa kiasi kikubwa (Alhamdulillah) Ningependa kuuliza sisi tuko Ulaya na kuna baadhi ya wenzetu wanapeleka watoto wao katika swimming pools kwenda kufundishwa kuogelea na wanangu wamekua wakinikera sana na wao niwapeleke lakini mimi nahisi kama haifai kwani huwa na mchanganyiko wa wanawake na wanaume. Ningeomba ufafanuzi kwa hili jambo kwani litawanufaisha wengi waislam wenzangu.

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwapeleka watoto Swimming pool.

 

Mtoto ni kiungo muhimu katika jamii na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana watoto wawe ni wenye kufundishwa kuogelea, kulenga shabaha na kupanda farasi. Hata hivyo, hayo yote yanafaa kufanyika katika mazingira ya Kiislamu. Ikiwa watoto ni wadogo sana kama tuseme hawajaanza kumaizi na wala kujua mas-ala ya uchi hilo litakuwa halina neno. Ama ikiwa labda wamepita miaka 5 na wameanza kumaizi mambo na hata kujua mas-ala ya uchi na tupu basi haitakubaliwa kisheria kuwapeleka huko kuogelea.

 

Baada ya kusema hayo, tunafahamu kuwa mambo mengi hurekebishwa kwa mazungumzo. Ikiwa katika sehemu hiyo wapo Waislamu wengi wenye kupeleka watoto wao kuogelea ni nyinyi kujipanga kwa kuzungumza baina yenu na baada ya kuafikiana mkazungumza na wasimamizi. Mazungumzo ndio hubadilisha mambo na katika mazungumzo mnaweza kuzungumza nao ili jinsia tofauti wawe na nyakati tofauti. Na hiyo itakuwa ni kheri kubwa sana kwenu na kwa kizazi chenu.

 

Fanyeni juhudi kuhusu hilo na Allaah Aliyetukuka Atawapatia tawfiki. Ili kuchukua tahadhari ni afadhali kwa sasa usiwapeleke watoto wako huko.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share