Uzazi Wa Kupanga Unafaa?
SWALI:
Jee Sheikh kuna njia yoyote ya uzazi wa mpangilio ya kiislam na kama ipo ni njia gani? Je, Sheikh kutumia condom kwa mke na mume ni vibaya?
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'Anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika ni kuwa njia za mpango wa uzazi zipo katika ulimwengu huu nyingine zikiwa zinakubalika na Uislamu na nyengine hazifai kutumika. Njia ambayo haifai kutumika ni ile ya kufunga kizazi milele (permanent) isipokuwa kwa haja kubwa ambayo inakubalika kisheria kama shida ya mama katika kuzaa na mfano wake.
Njia ambayo inayokubalika ni ile ya kutumia azl (coitus interuptus -kumwaga nje maji ya uzazi). Jaabir bin ‘Abdillaahi (Radhiya Allaahu 'Anhu) amesema: “Tulikuwa tukifanya 'azl ilhali Qur-aan ilikuwa ikiteremshwa, habari hii ilimfikia Mtume (Swalla Allahu 'Alayhi Wa Aalihi Wasallam) naye hakutukataza” (Al-Bukhaariy na Muslim).
Wanachuoni wameafikiana kuwa njia yoyote ya upangaji uzazi inakubalika isipokuwa ile ya kufunga kabisa kizazi. Na mtu anatakiwa atumie njia ambayo ni salama kwa mwenye kutumia kwa sababu zake za kibinafsi, lakini haifai kuwa ni sheria na kanuni ya dola.
Wanachuoni wametumia Qiyaas ya kwamba kwa kuwa 'azl ilikuwa inatumika kuzuia mbegu kufika kwenye uzao wa mama njia hizi nyengine za upangaji uzazi zinaruhusiwa kwa muda kwa kuafikiana baina ya mume na mke. Hivyo, kutumia condom inaruhusiwa. Kuhusu njia nyengine inabidi wanandoa wapate ushauri kwa daktari Muislamu mtaalamu, Mchaji ili ampatie njia muafaka na maumbile yake.
Tanbihi: Ieleweke kuwa njia nyingi za kutumia madawa na sindano zina madhara makubwa sana kwa binadamu, hivyo tuwe na tahadhari ya hali ya juu katika utumiaji wa vitu hivyo.
Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho :
Kupanga Uzazi Na Si Kuzuia Uzazi
Na Allah Anajua zaidi