Usharifu Nini Maana Yake? Je Ukoo Wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Uko Kweli?

SWALI:

 

Assalaam Alaykum

 

 Ya Maalim, Hua tunasikia kua kuna Koo (family) za MASHARIFU ktk baadbi ya Vijiij  vyetu Vya E.Afrika je hii ni kweli na kama ni kweli nini Maana halisi ya neno hili kilugha na kisheria

Na vipi CHEO hichi hupatikana mbele ya Allah?

 

 

JIBU:  

Neno Sharifu limetokana na neno la Kiarabu Sharaf lenye maana ifuatayo kwa Kiswahili: utukufu, adhama, heshima, hadhi, sifa, cheo kikuu, ulodi, usharifu, uungwana.

 

Hili ni neno kama maneno mengine ya Kiswahili ambayo yemetoka nje ya maana ile halisi ya Kiarabu na mara nyingi tunaifasiri kama tunavyotaka. Mfano ni neno Sheikh ambalo kwetu lina maana ya mwanachuoni lakini katika lugha ya Kiarabu lina maana ya uzee, utemi, uchifu, uongozi. Na sharifu nalo limekumbwa na tafsiri hiyo, kwani kwetu tunachukulia ni ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  kwa hakika kilugha neno hili lina maana tuliyoitoa hapo juu na hii inakwenda sambamba na mafunzo ya Kiislamu kuwa wanaadamu wote wamekirimiwa na kutukuzwa na Allah, yanayosema:

}} وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ وَحَمَلْنَاهُمْ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَرَزَقْنَاهُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ وَفَضَّلْنَاهُمْ عَلَى كَثِيرٍ مِّمَّنْ خَلَقْنَا تَفْضِيلا{{ً  

{{Na hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba}} (Israa 17: 70).

Na Allah Anasema ubora upo katika uchaji Mngu:

}}إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ إِنَّ اللَّهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ{{

{{Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mchaji Allaah zaidi katika nyinyi}} (AL-Hujuraat 49: 13).

 

Na Mtume wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  katika Hijjatul Wida'a alisema kwamba hakuna tofauti wala ubora kwa Mwarabu juu ya asiyekuwa Mwarabu, wala mweupe na mweusi isipokuwa kwa uchaji Mungu.

 

Swali ambalo tunaweza kujiuliza ni kuwa: Sharifu ni nani? Kwa huku kwetu na Waislamu ulimwengu mzima ni yule mwenye kizazi cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  isipokuwa katika nchi ya India, Pakistan wanamuita Sayyid (bwana). Kizazi cha Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ni Quraysh. Je, Maquraysh wote ni Masharifu? Jawabu kwetu ni kuwa si wote.

 

Wengine wanaweza kusema ni Baniy Hashim na kutaka kutukuzwa na kupata fursa ya kuwatawala watu. Nchi ya Jordan inajiita al-Mamlaka al-Urduniyah al-Haashimiyyah (Ufalme wa Jordan wa Baniy Haashim, kwa kifupi inaitwa Jordan). Swali ni kuwa, je, Bani Haashim wote ni Masharifu? Jawabu ni hapana. Je, Baniy 'Abdul-Mutwallib? Jawabu ni hapana kwani wengine wao kama kina Abu Lahab waliupiga vita Uislamu na wakafa katika ukafiri.

 

Na tufahamu ya kwamba katika mas-ala haya mafungamano halisi si ya kidamu kwani mahusiano ya ki-Imani ndio yaliyo halisi. Ndio Nabii Nuh (‘alayhis-salaam.) akaambiwa kuwa mtoto wake si wake japokuwa walikuwa na unasaba wa kidamu. Allah Anasema:

}}وَنَادَى نُوحٌ رَّبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابُنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ{{

 }} قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ فَلاَ تَسْأَلْنِ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّي أَعِظُكَ أَن تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ{{   

{{Na Nuwh alimwomba Mola wake: Ee Mola wangu! Hakika mwanangu ni katika ahli zangu, na hakika ahadi yako ni haki. Na Wewe ni Mwenye haki kuliko mahakimu wote. Akasema: Ewe Nuwh! Huyu si katika ahali zako. Mwendo wake si mwema. Basi usiniombe jambo usio na ujuzi nalo}} (Huud: 11: 45 - 46).

 

Tukichukulia mambo ya kinasaba tunajikuta tuna maswali mengi na utata mkubwa, kwani huku kwetu inachukuliwa kuwa ni wale waliozalikana na 'Aliy na Faatimah bint Rasuul (Radhiya Allaahu ‘anha) Je, nasaba Kiislamu inachukuliwa upande gani? Upande wa mama au wa baba? Jawabu ni kuwa nasaba inachukuliwa kwa upande wa baba.

 

Ikiwa ni kutoka kwa baba, kwa nini watoto wa nduguze 'Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama watoto wa 'Aqiil na Ja'far (Radhiya Allaahu ‘anhu) wasiwe pia ni masharifu? Jawabu la swali hilo halipo na halipatikani. Ikiwa nasaba inatoka kwa mama, yaani Faatimah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa kuwa ni binti wa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  Je, Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  alikuwa na binti mmoja pekee? Jawabu ni hapana, kwani alikuwa na mabinti wengine kama Ruqayyah, Zaynab na Umm Kulthum ambao waliolewa na kuzaa.

 

Ikiwa tutasema ya kuwa watoto wa 'Ali na Faatimah (Radhiya Allaahu ‘anha) wote walikuwa ni Bani Haashim, hivyo kuingia katika usharifu. Je, kwa nini tunabagua baina ya watoto wao? Inafahamika kuwa wao walikuwa na watoto kadhaa miongoni mwao ni Hasan, Husayn, Muhsin, na kadhalika mbali na kuwa 'Ali (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikuwa na watoto wengine wa kiume kwa wake wengine. Swali ni kuwa ni kwa nini masharifu wanachukuliwa kuwa ni wale wazawa wa Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) na ilhali Hasan (Radhiya Allaahu ‘anhu) ndiye aliyekuwa mkubwa (mtoto wa kwanza) naye alizaa watoto kadhaa wa kiume?

 

Labda tukiafikiana katika maana ya Sharifu kinasaba huenda tukapata ufumbuzi madhubuti kuhusu familia hiyo. Ajabu ni kuwa tunapata masharifu wa makabila yote ya kilimwengu kwa mfano Tanzania wapo Masharifu wa Kiarabu, Kihindi,  Kidigo, Kizaramo, Kirangi n.k. na Kenya vilevile wapo Masharifu wa Kiluhya, Kiswahili, Kikikuyu, Kibajuni, wa Kiarabu, wa Kisomali, wa Kiborana na wengine. Na ukienda nchi nyengine utapata wapo wengi zaidi ya hao. Na ili kupata jaha na utukufu wameleta hekaya chungu nzima ambazo zinamuingiza mtu katika kufuru. Wangapi wanaodai ni Masharifu huko Afrika ya Mashariki tunaowajua na kuwasikia wana matendo yasiyokuwa ya Kiislam? Wangapi wana wanawake zaidi ya kumi na watoto hata wenyewe hawawajui!! Kila wakienda kijiji fulani wanapewa mwanamke na hata ilifika baadhi ya sehemu, baadhi ya hao wanaojidai ni Ma-Sharifu anapewa mke wa mtu alale naye kama mtu huyo ana wake wawili au zaidi!! Tujiepushe na hayo yote ili tusalimike katika dunia na Akhera.

 

Tukumbuke kuwa yale madai wanayosema Masharifu kuwa wao wataingia Peponi bila ya hesabu ni uongo na tujihadhari sana na hilo. Hii ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema: "Na mwenye kucheleweshwa kwa amali yake haitamtanguliza nasaba yake" (Muslim na Ahmad).

 

Kadhalika Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alipoteremshiwa aya isemayo:

}}وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ {{

{{Na uwaonye jamaa zako walio karibu nawe} (Ash-Shu'araa 26: 214),

alisema: "Enyi Maquraysh! Okoeni nafsi zenu kutoka kwa Allah, kwani mimi sitowafaa kwa chochote mbele ya Allaah. Enyi Bani 'Abdi Manaf! Sitowafaa kwa chochote mbele ya Allaah! Ewe Swafiya (shangazi yake), sitokufaa kwa chochote mbele ya Allaah! Ewe Faatimah (bint Muhammad) niombe utakalo, lakini sitokufaa kwa chochote mbele ya Allaah" (Ahmad).

 

Na miongoni mwa kauli zilizotangaa sana hapa Afrika Mashariki hata kwa Waislamu wa kawaida ni ile ibara inayotupatia maana halisi ya sharifu pale waliposema: "Man Sharafa nafsahu fahuwa shariif - Mwenye kuitukuza nafsi yake basi yeye ni sharifu". Na kauli hii ni miongoni mwa ibara inayotufupishia malengo ya shari'ah ambayo tumeyaelezea hapo juu kutumia Aya na Hadithi kwa mfano:

 

{{Hakika aliye mtukufu zaidi kati yenu kwa Allaah ni huyo aliye mchaji Allaah zaidi katika nyinyi}} (49: 13).

 

Hivyo, yeyote mwenye kufanya matendo mema na kuacha maovu na akamcha Allah basi anakuwa katika cheo kitukufu mbele ya Allah kuliko yule mwenye nasaba nzuri lakini matendo mabaya.

 

wa Allaahu A'alam

 

 


Share