Ameacha Kaka na Madada Na Dada Wa Mama Mmoja

 

SWALI:

Aliyefariki ameacha kaka na madada hawa wote baba mmoja mama mmoja na aliyefariki. Pia kulikua na dada wa mama mmoja.

Je?? Mali ilowachwa na aliyefariki itagawiwa vipi?? Huyu dada wa mama mmoja atarithi nae??

AL-HIDAAYA ILIBIDI KURUDI KUMUULIZA MUULIZAJI:

Tunasikitika kwamba Swali lako haliko wazi, hatukuweza kulielewa ili tukujibu. Hivyo tafadhali tujulishe:

1-    Je hao ndio warithi waliobakia?

2-    Aliyefariki hakuwa na mke,

3-    Hakuwa na wazazi  

4-    Hakuwa na watoto  

MUULIZAJI KARUDI KUJIBU:

Nashukuru kwa kunijibu, ALLAH atujaze mema.

 

Majibu ya masuali ulioniuliza ambayo yamesababisha kutokueleweka vizuri ni haya :-

 

   1.  Hao ndio waliobakia , yaani  SHAKIKI ni  Kaka (1)  na madada (4)

        pia alikua na dada (1) wa kwa mama.

 

   2. Aliyefariki hakua na mke

 

   3. Wazazi wake wote wamefariki kabla yake.

 

   4. Hakua na watoto.

 

   Imani yangu kubwa  sasa nimeeleweka, INSHAALLAH  nategemea nitajibiwa bila  uchelewesho.

 

SAMAHANI: Naomba mniwie radhi kwa lugha nilioitumia yaani KISWAHILI nilichotumia, na kilivyofahamika/kilivyoeleweka. 

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza, tunawaomba wenye kuandika maswali yote na hasa la mirathi waandike kwa njia nzuri kwa kuelezea wazi wazi kila kitu na hali ilivyo ili  kutuwezesha sisi kuweza kuyajibu maswali yenu bila utata.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu urithi wa aliyefariki. Swali lako lina utata na halipo wazi kama inavyotakiwa. Je, madada ni wangapi? Je, wazazi wa aliyefariki wapo hai au nao wamekufa? Ikiwa hao uliowataja ndio warithi wa pekee, urithi utakuwa kama ifutavyo:

Dada wa mama mmoja atapata sudusi (1/6) na kinachobakia watagawanya ndugu shaqiqi, mwanamme sehemu mbili ya mwanamke. Kwa sababu hakuna idadi ya madada zake utafanya hesabu mwenyewe na sidhani itakuwa ngumu. Sehemu iliyobaki ni 5/6, kwa mfano ikiwa waliobaki ni kaka mmoja na dada mmoja pia shakiki. Kaka atapata 5/9 na dada atapata 5/18. Lau kaka atakuwa ni mmoja na madada wawili, kaka atapata 5/12 na kila dada atapata 5/24. Na hesabu itakwenda hivyo.

Baada ya kupata ufafanuzi wa muulizaji ambaye alituma baada ya kujibiwa hili swali, majibu yamkuwa hivi:

1.      Dada kwa mama atapata 1/6.

2.      Kaka shakiki atapata 10/36.

3.      Kila dada shakiki atapata 5/36.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share