Watu Wananikejeli Kwa Sababu Ya Kuvaa Jilbaab, Je, Nivue Kuwaridhisha?

 

Watu Wananikejeli Kwa Sababu Ya Kuvaa Jilbaab, Je, Nivue Kuwaridhisha?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatullah wabarakat Natoa wingi wa shukurani za dhati kwa waanzishi wa web site hii na Allaah atawajaza kila la kheri naamini wazi si jambo la kawaida bali ni uwezo wake Allaah S.A kuweza kuipa nguvu Uislam

 

 

Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 23 nimeolewa na nina mtoto mmoja swali langu kila siku mimi nilikuwa nikivutiwa sana nikiona watu wamejistiri kwa majilbab ingawa nilikuwa siendi kichwa wazi lakini nilikuwa nahisi kuwa ucha wa Allaah ulioje kuwa mtu kuvaa vazi la heshima kama hilo hadi huwa naota nikimuona mtu kavaa namuhusudu sana sasa na mie nimeanza kuvaa lakini wanakuja watu na maneno ya kila aina weye kijana mzuri unavaa hivyo mume wako ataenda kutafuta wengine huko nje wanovaa siyo weye na mishungi na maneno tele ya karaha na watu hao hao ndio ninao kwani wamo kwenye kazini kwangu sasa nifanyeje na ninataka kuwa karibu sana na Allaah na kuepukana na mambo ya kishetwan yaso faida wala heri.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Awali ya yote tunakuombea kwa Allaah Aliyetukuka Akupe msimamo wa kuweza kusimama imara katika hilo kwani wewe hufuati ya mtu na viumbe bali ya Muumba. Na hakuna jambo zuri kama kufanya hivyo.

 

 

Allaah Aliyetukuka Anasema:

... ۚ وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٧﴾

Na lolote analokupeni Rasuli ((صلى الله عليه وآله وسلم basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Hashr: 7].

 

 

Kufuata watu hakumletei yeyote yule isipokuwa ni matatizo na mashaka. Ndio Allaah Aliyetukuka Akasema:

وَإِن تُطِعْ أَكْثَرَ مَن فِي الْأَرْضِ يُضِلُّوكَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ إِن يَتَّبِعُونَ إِلَّا الظَّنَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَخْرُصُونَ ﴿١١٦﴾

Na kama ukiwatii wengi walioko ulimwenguni, watakupoteza na njia ya Allaah. Hawafuati isipokuwa dhana tu, na hawakuwa ila wenye kubuni uongo. [Al-An'aam: 116].

 

 

Dada yetu wewe uko katika njia ya sawa wala usitazame wala kurudi nyuma kwani kufanya hivyo ni kuwafuata mashetani wa kibinaadamu ambao huwa hawawatakii wenzao mema na mazuri.

 

 

Kuvaa vazi la Kiislamu kwa msichana na mwanamke ni katika amri aliyoitoa Allaah Aliyetukuka kama Alivyosema:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّأَزْوَاجِكَ وَبَنَاتِكَ وَنِسَاءِ الْمُؤْمِنِينَ يُدْنِينَ عَلَيْهِنَّ مِن جَلَابِيبِهِنَّ ۚ ذَٰلِكَ أَدْنَىٰ أَن يُعْرَفْنَ فَلَا يُؤْذَيْنَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٥٩﴾

Ee Nabiy! Waambie wake zako, na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie jilbaab zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allaah daima ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Al-Ahzaab: 59].

 

Na katika Suwrah hiyo hiyo, Allaah Aliyetukuka Akatuambia:

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَن يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَن يَعْصِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُّبِينًا ﴿٣٦﴾

Na haiwi kwa Muumini mwanamume na wala kwa Muumini mwanamke, Anapohukumu Allaah na Rasuli Wake jambo lolote, iwe wana hiari katika jambo lao.  Na anayemuasi Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amepotoka upotofu bayana. [Al-Ahzaab: 36].

 

 

Uamuzi ni wako dada yetu, kufuata njia ya uongofu au ya upotevu kwa kuwafuata wanaadamu wasio na hamu ya Aakhirah. Nasaha yetu ya dhati ni kuwa tunakuomba ufuate ya Allaah Aliyetukuka na Nabiy Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na uache mengine yote. Kadhaalika haifai kumridhisha kiumbe kwa kumuasi Muumba, anasema Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba” [At-Tirmidhiy].

 

 

Kufuata watu ikiwa ni rafiki, wazazi,  mume wako,  au yeyote mwenye mamlaka nawe katika maasi, utakuja kujuta siku ya Qiyaamah:

يَوْمَ تُقَلَّبُ وُجُوهُهُمْ فِي النَّارِ يَقُولُونَ يَا لَيْتَنَا أَطَعْنَا اللَّـهَ وَأَطَعْنَا الرَّسُولَا ﴿٦٦﴾وَقَالُوا رَبَّنَا إِنَّا أَطَعْنَا سَادَتَنَا وَكُبَرَاءَنَا فَأَضَلُّونَا السَّبِيلَا ﴿٦٧﴾رَبَّنَا آتِهِمْ ضِعْفَيْنِ مِنَ الْعَذَابِ وَالْعَنْهُمْ لَعْنًا كَبِيرًا ﴿٦٨﴾

Siku zitakapopinduliwa nyuso zao motoni, watasema: Laiti tungelimtii Allaah, na tungelimtii Rasuli. Na watasema: Rabb wetu! Hakika sisi tumewatii mabwana zetu, na wakuu wetu, basi wametupoteza njia. Rabb wetu! Wape adhabu maradufu, na walaani laana kubwa. [Al-Ahzaab: 66-68]

 

 

Tunakutakia kila la kheri na fanaka pamoja na kuwa na msimamo mwema katika dunia hii na Allaah Akuzidishie mapenzi yako makubwa katika Dini hii na Akuepushe na fitnah za dunia na walimwengu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share