Nani Qur-aniyyuwn?
Nani Qur-aniyyuwn?
SWALI:
Assalamu Alaikum
Naomba Kufahamishwa Kuhusiana Na Ahlu-al-quran? Misingi Wanaoamini.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Na maana yake ni kama ifuatavyo:
Ahl maanake ni watu na al-Qur-aan ni Qur-aan. Kwa hiyo, ibara hiyo ina maana ya watu wenye kuifuata Qur-aan. Hakika hii ni sifa ya kila Muislamu ambaye ana Imani japo chembe ndogo ya hardali.
Kusudio la muulizija ni kuhusu kundi potofu linalojulikana kama Qur-aaniyyuwn. Ni kikundi ambacho kimeanzishwa muda mrefu kwa sasa na kimeanza kuenea na kufika hata Afrika mashariki kwa wakati huu. Itikadi yao ni kuwa sisi (Waislamu) tunafaa kufuata Qur-aan peke yake kwani hayo ndio maneno ya Allaah Aliyetukuka. Na sababu ya kutofuata kwao Sunnah na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ile nadharia yao potofu kuwa katika Hadiyth zipo ambazo ni Sahihi, Hasan, Maudhui, Dhaifu na kadhalika, na pi madai yao kuwa Hadiyth zimeanza kukusanywa baada ya miaka mingi ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki.
Hii ni itikadi potofu kwa kuwa Qur-aan yenyewe inatuamuru na kutuagizia tuwe ni wenye kumfuata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kila hali na kumfuata yeye ndiko kumfuata Allaah Aliyetukuka, kuwa yeye hazungumzi kwa matamanio yake bali ni wahyi anaoteremshiwa. Pia leo tukisema tufuate Qur-aan pekee bila ya Sunnah hata Ibadah kama Swaalah hatutaweza kuitekeleza kwani hakuna maelezo hayo kama idadi zake, wakati wake maalumu uliowekwa, vilevile Swawm na hukumu zake, Zakaah na vigawanyo vyake, Miyraath, Hajj na utekelezaji wake, n.k. yote hayo hayakufafanuliwa ndani ya Qur-aan bali yanapatikana maelezo yake kwenye Hadiyth za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hivyo, kupinga na kukataa Sunnah, ni kuikataa Qur-aan pia, na hao wanaojidai wanaifuata Qur-aan pekee na kukataa Sunnah, basi wajue kuwa wao wanapingana na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na watakuwa washatoka katika njia ya Uislam.
Hayo kwa ufupi ndio tunayoweza kueleza kuhusu kipote hicho. Ama kwa maelezo zaidi ya kina kuhusu kikundi hicho kilichopotea, utapata kwenye makala hii chini:
Qur-aniyuun – Wanaopinga Hadiyth Za Mtume (Swallah Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam)
Na Allaah Anajua zaidi