Makundi 72 Yatakayoingia Motoni
Makundi 72 Yatakayoingia Motoni
SWALI:
assalam aleikum.amma baad namshukuru Allaah kuniwezesha tena kuandika sula hili ambalo natumai litakuwa bayana kwako kwa uwezo wake Allaah. Naomba uanitajie makundi 73 ambayo Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)(s.a.w) kayabashiria kuwa yataingia motoni ila moja tu na unifafanulie vizuri tofauti zao? Ahsante wajazakAllaahu kheir.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Ieleweke kuwa hapa si mahala pake pa kuweza kuyaeleza makundi hayo kufanya utafiti huo itabidi tusiwe ni wenye kujibu maswali wala kufanya kazi wala shughuli nyengine isipokuwa hiyo. Hivyo ni juu ya mwanafunzi kwenda katika vitabu vingi vilivyoelezea hayo.
Kwa kifupi tu kwa kukupa mwangaza kidogo, utayajua yale makundi yaliyo potofu kwa kuona na kujua itikadi zao. Mfano mzuri leo utaona wanaodai kuna mtume baada ya Nabiy wa haki na wa mwisho Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), utawaona pia wale wanaowakufurisha Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na kuwatukana wake za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), pia utawaona wengine wanaokufurisha Waislam na kuwatoa katika Dini kwa sababu wanaamini kuonekana Allaah Qiyaamah, na wanakufurisha Waislamu kwa sababu ya kufanya baadhi ya maasi, na pia utawaona wengine wanakataa Hadiyth za Nabiy na kudai kuwa wao wanafuata Qur-aan pekee, na pia utawakuta wengine wanakwenda kuwaomba watu waliokufa makaburini ili wawasaidie haja zao, na wengi wengine wasio na idadi.
Tutalijua kundi lililookoka na ambalo halipo katika hayo makundi 72, kwa kuitazama ile Hadiyth ya bwana Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
"Wamegawanyika Mayahudi katika mapote 71, wakagawanyika Wakristo katika mapote 72 na Ummah wangu utagawanyika mapote 73. Yote hayo yataingia motoni ila moja tu)) Swahaba waliuliza: Ni lipi hilo, ee Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allaah! Akasema: ((Ni lile nililokuwemo mimi na Swahaba zangu". [Ahmad, Abu Daawuwd, At-Tirmidhiy na Ad-Daarimiy].
Kundi hilo litakuwa ni lenye kufuata maagizo ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa), Sunnah za Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Makhalifa waongofu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na Swahaba wengine (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na wema wote waliotangulia (Salafus-Swaalih). Muislam atakayejikita na kuwa imara katika hayo basi atakuwa katika njia nyoofu. Dalili ni nyingi katika Qur-aan na Sunnah. Miongoni mwayo ni kauli ya Aliyetukuka:
..وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ فَازَ فَوْزًا عَظِيمًا ﴿٧١﴾
Na anayemtii Allaah na Rasuli Wake, basi kwa yakini amefanikiwa mafaniko adhimu.[Al-Ahzaab: 71].
Pia Amesema Aliyetukuka:
قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣١﴾
Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi, Atakupendeni Allaah na Atakughufurieni dhambi zenu. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu. [Aal-Imraan: 31].
Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) naye anatueleza yafutayo katika khutbah yake ya Hijjatul Wadaa: "Hakika nimewaachia kitu ambacho hamtapotea baada yangu lau mtashikana nacho, Kitabu cha Allaah" [Muslim].
Sehemu nyengine kasema: "Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu" [Al-Bukhaariy na Muslim].
Na katika masimulizi ya Abu Najiih al- 'Irbaadh bin Saariyah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba: "Alituwaidhia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) yaliyozifanya nyoyo kuingia hofu na macho yakatokwa na machozi. Tukamwambia: "Ee Rasuli wa Allaah! Yaonyesha kama haya ni mawaidha ya kuaga, basi tuusie". Akasema: "Nawausia kumcha Allaah, Kwani hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni kufuata Sunnah zangu na Sunnah za Makhalifa walioongoka, yashikeni kwa magego mambo yao". [Abu Daawuwd, Ahmad, At-Tirmidhiy, Ibn Maajah na Ad-Daarimiy].
Mambo muhimu ambayo tunayapata katika dondoo za hapo juu ni kuwa, kuwepo kwetu katika kundi litakaloongoka ni kufuata mwendo aliokuwa nao Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Makhalifa wake (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na kushikamana nao kivitendo barabara.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atufanye ni wenye kuyashikilia hayo vilivyo ili tuwe ni wenye kuingia katika Rehma Yake na kuwa ni kundi lililosalimika na moto, kundi lililonusurika na ni kundi liliokoka. Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atusahilishie hatua zetu katika kuelekea katika mwendo wa sawa na wa haki.
Na Allaah Anajua zaidi