Kundi La Twariyqah Likoje Na Linafungamana Vipi Na Mashia?

 

 

Kundi La Twariyqah Likoje Na Linafungamana Vipi Na Mashia?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Je, kundi la twarika ni kundi gani inafungamana vipi na mashia  au ithna shari? Na limetimbuka kutoka wapi?

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.  

 

Kundi hili la Twariqah ni kundi la Kisufi na ambalo wafuasi wake zaidi wanafuata matamanio ya nafsi zao kinyume na Uislaam. Wanakuwa ni wenye kufanya mambo mengi ya uzushi na hata ushirikina. Kwa mfano ni watu ambao wanapenda sana Mawlidi, Khitmah, matanga na mengineo.

 

Katika ushirikina ni kuwa wanawatukuza Manabii na mawalii kwa sifa za Allaah au saa nyingine zaidi ya Allaah.

 

Hao wana kisa kimoja kinachodaiwa kuwa cha kweli na ambacho kimeenea nacho ni  cha Shaykh ‘Abdul-Qaadir Jaylaaniy kisa ambacho kimejaa uzushi na shirki wakidai kuwa Shaykh huyo alikuwa na uwezo wa kurudisha roho za watu!

 

Itikadi nyingi za watu wa Twariyqah zinafanana na Rawaafidhw (Mashia) Ithnaa ‘Ashaeri, nyenginezo ni mbaya zaidi.

 

Wa kwanza katika kufuata na kueneza Twariyqah za Kisufi ni al-Husayn bin Manswuwr anayejulikana zaidi kwa al-Hallaaj aliyezaliwa mwaka 244H. Huyu alikuwa na itikadi ya kwamba Allaah Hushukia ndani ya mwana Aadam. Akaendelea kusema kuwa yeye na Allaah ni kimoja, yeye na Allaah ni roho mbili zilizoushukia mwili mmoja. Katika hayo alikuwa na beti za mashairi aliposema:

 

Mimi nimpendae naye ni mimi kwa kweli,

Sisi kwa atambuae ni roho mbili kwenye mwili mmoja.

Unaponiona basi umemuona,

Na unapomuona basi umetuona sote (wawili).

 

Mwengine aliyechupa mipaka katika itikadi mbaya ni Muhyid-Diyn Muhammad bin ‘Aliy bin Muhammad bin Ahmad bin ‘Abdillaah ibn al-‘Arabiy aliyezaliwa mwaka 560H.  Madai yake makuu yalikuwa:

 

  • Alidai “Wahdatul-Wujuwd” Yaani: Viumbe na Muumbaji ni kitu kimoja.
  • Yeye hupokea ilimu yake moja kwa moja kutoka kwa Allaah.
  • Alizua Dini yake aliyoiita kwa jina “Dini ya Mapenzi.”  Hiyo ni kwamba yeye hapingani na dini yoyote wala hawachukii wafuasi wa dini yoyote.

 

Naye alikuwa na beti zisemazo:

 

Umekuwa moyo wangu,                   Wakubali kila dini.

Ya wana paa kwangu,                      Na kanisa la kasisi.

Majumba ya masanamu,                  Na al-Ka‘bah dawamu.

Na mbao za Tawraat,                         Na Msahafu wa Qur-aan.

Dini niifuatayo,                                 Ya mapenzi yendapo.

‘Ibaadah yangu ni hiyo,                      Na Iymaan ipo hapo.

 

Ukiyapima haya utaona ni ukafiri mtupu, tunamuomba Allaah ('Azza wa Jalla)  Atulinde.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share