Kuna Ubaya Gani Mashia Kuwatukuza Maimaam Na Hali Sunni Wanawatukuza Maswahaba, Na Vipi Kuswali Nao?

 

Kuna Ubaya Gani Mashia Kuwatukuza Imaam Na Hali

Sunni Wanawatukuza Swahaba, Na Vipi Kuswali Nao?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Asalamun alaykum

Poleni kwa kazi, niliona majibu yenu lakini nashangazwa sana kwni kuhusu hao mashia ni kuna ubaya gani wao kuwapenda watu wa Nabiy? Kwani sio watu wa mbali na ni wakaribu sana kwa Nabiy wetu Muhammad(Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na wao maisha yao ni vigezo kwetu sisi kwani ndio waliokua na Nabiy bega kwa bega kama tukisoma tarekh na ikiwa wao wao wanasifu sna watu wa mtume na kuwatukuza watu wa Nabiy na ikiangalia hao watu wa Nabiy sio wa mbali ni mtoto wa mtume na wajukuu wa mtume. sasa na sisi tutawakjibu nini ikiwa watawambia kua nanyi mnawapenda sna swahaba na kuliko watu wa Nabiy na vile vile hao Nabiy hakuwachagua kua viongozi mutawajibu nini? Na jengine mm nilikua nauliza kusali na mshia mthnasharia vibaya au laa? Na kama vibaya kwa nini?

Salamun alaykum.

 

Kwanza poleni kwa kazi na jengine niliuliza kipindi kidogo suali langu lakini nashangaa mbona hamkunijibu? Na suali langu nilitatanishwa pale kuhusu yule mtu aliyeuliza je kusali au kuwatolea salam mashia inafaa au haifai? Kwani muliongea kuwa wao hawawapendi maswahaba na wanapenda sna watu wa mtume. Yaani bibi fatma na watoto wake. Sasa mm hapa nilikua nauliza kwani kuna ubaya kuwapenda watu wa mtume? Na vile vile kama wao wanawapenda watu wa mtume hata nasi pia tunawapenda hao swahaba na ukiangalia hasa watu wa mtume ndio waliokua karibu zaidi kuliko hata mtu yoyote yule. Basi ikiwa mutafahamu na mnalo suala langu basi naomba mnijibu kwa haraka sana.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

 

Hakika ni kuwa haiwezekani kama unavyotaka kuwa swali lako lijibiwe haraka sana kwani katika alhidaaya kuna nidhamu ya kujibu maswali. Ikiwa kila mmoja wetu atataka hivyo basi hatutaweza kujibu swali lolote. Maswali yanajibiwa yanavyokuja, la mwanzo kujibiwa mwanzo na yanayokuja baadaye kujibiwa kwa utaratibu huo. Kwa kuwa tumelipata swali lako na kumekuja wakati wa kulijibu twalijibu bila ya upendeleo wala kwenda kinyume na nidhamu hiyo.

 

Kisha twashangazwa na ibara yako, hata nasi pia tunawapenda hao masahaba. Hilo neno ‘hao’ linaonyesha kuwa ni kama kujitoa kuwa wewe huwapendi. Ni itikadi ya Muislamu iliyo sahihi kuwapenda Swahaba wote bila kubagua (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na pia jamaa ‘Aali Bayt’ za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Mwenyewe Ametutaka tuwapende na kuwaheshimu Swahaba kwani Yeye Alikuwa radhi nao na ndivyo alivyotuagizia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Allaah Aliyetukuka Amesema:

 

وَالسَّابِقُونَ الْأَوَّلُونَ مِنَ الْمُهَاجِرِينَ وَالْأَنصَارِ وَالَّذِينَ اتَّبَعُوهُم بِإِحْسَانٍ رَّضِيَ اللَّـهُ عَنْهُمْ وَرَضُوا عَنْهُ وَأَعَدَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي تَحْتَهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا ۚ ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿١٠٠﴾

Na wale waliotangulia awali (katika Uislamu) miongoni mwa Muhajirina na Answaar na wale waliowafuata kwa ihsaan; Allaah Ameridhika nao, nao wameridhika Naye. Na Amewaandalia Jannaat zipitazo chini yake mito, ni wenye kudumu humo abadi. Huko ndiko kufuzu adhimu. [At-Tawbah: 100]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema kuhusu Answaar: "Hawapendi Ma-Answaar isipokuwa Muumini na hawachukii wao isipokuwa mnafiki" [al-Bukhaariy na Muslim]. Zipo Hadiyth za kuonyesha fadhila za Swahaba na kuhitajika sisi kuwapenda. Wale waliokuwa msitari wa mbele zaidi Makhalifa waongofu (Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan na ‘Aliy) ambao tunahitajika kufuata Sunnah zao bila kusita. Baadaye wapo wale kumi waliobashiriwa Pepo na Swahaba wanaume na wanawake waliopatiwa sifa moja au nyingine. ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikubali ubora wa Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma). Kwa hiyo, Muislamu anafaa awapende Swahaba, hata hivyo asiwatukuze kupita mipaka ya kidini, Uislamu.

 

Ama familia ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Muislamu wa kweli anatakiwa awapende kwa dhati, hasa wake zake watukufu na wale waliojulikana kwa wema, kama ‘Aliy, Faatwimah, Zaynab, Ummu Kulthuum, Ruqayyah, al-‘Abbaas, Hasan na Husayn na wengineo waliojulikana. Inafaa wao pia tuwapende kwa mipaka iliyowekwa na Uislamu sio zaidi ya hapo. Na ndio kwa kuwapenda kwetu huwa tunawaombea kila tunapomswalia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Hata hivyo, Mashia mbali na kusema wanawapenda Ahlul Bayt, lakini wanafanya mambo ya ajabu na kuwapatia sifa za ajabu wale ambao wanawaita ni Imamu. Wamewapatia sifa za uungu wanaadamu. Kwa mfano mwanachuoni wao mmoja kwa jina Tabatabai amesema kuwa hawa Imamu wao 12 wanapata Wahyi, kumaanisha kuwa walikuwa Manabii. Ilhali twafahamu kuwa Allaah Aliyetukuka Amesema:

 

مَّا كَانَ مُحَمَّدٌ أَبَا أَحَدٍ مِّن رِّجَالِكُمْ وَلَـٰكِن رَّسُولَ اللَّـهِ وَخَاتَمَ النَّبِيِّينَ ۗ وَكَانَ اللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمًا ﴿٤٠﴾

Hakuwa Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) baba wa yeyote miongoni mwa wanaume wenu, lakini ni Rasuli wa Allaah na ni mwisho wa Manabii. Na Allaah daima ni Mjuzi wa kila kitu. [Al-Ahzaab: 40]

 

Sisi twatakiwa tumfuate katika mwisho wa utume Allaah Aliyetukuka au Tabatabai au Kulayniy aliyesema kuwa ‘Hao Imamu wao wanajua Ghaibu na wanajua siku yao ya kufa na wanachagua kifo wanachotaka wafe!!’ Ilhali Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufahamisha kuwa yeye ni Nabiy wa mwisho hakuna mwengine atakayekuja baada yake, na yeyote atakayedai utume ni Dajjaal (mwongo).

 

Pia Mashia wanasema kuwa Imamu wao wanajua yote yaliyotokea hapo mwanzoni na yatakayotokea mpaka mwisho wa dunia. Je, hii ni sifa ya mwanaadam au ya Allaah Aliyetukuka? Katika miaka ya themanini, Bilaal Muslim Mission, taasisi ya Kishia Kenya iliiandikia Wizara ya Elimu kuwa masomo ya Kiislamu yanayosomeshwa mashuleni yanakwenda kinyume na itikadi yao kwa hivyo kuwe na syllabus yao ya Kishia. Kwani wao na Masunni wanatofautiana katika misingi hasa ya Dini. Hiyo ni kumaanisha Dini yao ni tofauti kabisa na tuliyonayo sisi. Allaah Aliyetukuka Atuepushe na hayo ya maajabu.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share