Hadiyth Katika Swahiyh Al-Bukhaariyiy Zote Ni Swahiyh?

 

SWALI:

Assalamu aleikum warahmatullahi wabarakatuhu, ninapenda kuuliza kama ni kweli kuwa Hadiyth zote zilizo katika Kitabu cha Swahihi Bukhari ni sahihi au la, na kama zote ni sahihi mbona kuna Hadiyth ambazo zinapingana waziwazi na Qur'an tukufu! Naomba munipe faida kwa kunijibu

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Imani anayotarajiwa awe nayo kila mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho ni kuwa hakuna juu ya ardhi hii kitabu kilichosahihi kisicho na kosa wala shaka zaidi ya Qur-aan.

Pia ni iman anayotarajiwa awe nayo kila Muislam kuwa Sahihi Al-Bukhaariy na Muslim ni vitabu vilivyo sahihi zaidi katika vitabu vya Hadiyth baada ya Qur-aan.

Na umma umevikubali kwa kuvipokea; Imam Al-Bukhaariy amenukuliwa akisema: ‘Sikutia katika kitabu changu al-Jaami’ –mkusanyiko kamili ambao haujaacha sehemu au ilmu yoyote inayohusiana na Hadiyth isipokuwa Hadiyth zile tu zilizothibitishwa kwa ukamilifu kuwa ni za kweli (Sahihi) na pia nimeziacha Hadiyth nyingi Sahihi kuchelea kitabu kuwa kikubwa.

a- ni kweli kuwa Hadiyth zote zilizo katika Kitabu cha Swahihi Bukhari ni sahihi au la,

Suala hili ni katika maswali wanayoyapandikiza maadui wa Kiislamu kama Mashia, Qur-aniyuun na Mustashriyqiyna na wenye urafiki nao kujaribu kuwatilia shaka Waislam katika chanzo chao cha pili cha dini yao kama walivyojaribu kuwatilia sumu kama hii katika imani zao juu ya Qur-aan lakini hawakuweza kufaulu na wala hawataweza, mwisho wakaanzisha sumu kali yenye kusema kuwa kwanini tuchukuwe Hadiyth ambazo ziko sahihi na dhaifu na kadhalika; ni bora tutosheke na Qur-aan pekee.

Hadiyth zote zilizopo katika kitabu cha Swahiyh Al-Bukhaariy ni sahihi kama jina la kitabu linavyoashiria; wataalamu wa Hadiyth (Muhaddiythiyn) wanaposema hivyo huwa wanakusudia kuwa kila walichokipokea Al-Bukhaariy na Muslim ni kilichoshikamana (Muttaswil), Silsilah au mfululizo wa wasimulizi hicho ndio kinachokusudiwa na kuhukumiwa kuwa ni sahihi katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim.

Ama walichokipokea na kuwa na upungufu wa mmoja katika wasimulizi wa mwanzo au wengi ‘Mu’allaq’: kilichodondosha katika mwanzo wa isnaad yake msimulizi mmoja au wengi kwa mfululizo na akasema tu amesema Swahaba au Taabi’- ambayo katika Swahiyh Al-Bukhaariy ni nyingi lakini iko katika Tafsiyr –Taraajum- za milango na utangilizi wake na wala hakuna namna hii –Mu’allaq- ndani ya milango kabisa, na katika Swahiyh Muslim hakuna isipokuwa katika Hadiyth moja tu katika mlango wa Tayyamum kwani hakuiwasilisha katika sehemu nyingine.

Hata hivyo wataalamu wa Hadiyth wamezitolea hukumu Hadiyth zenye sifa kama hizo ambazo zimo katika Swahiyh Al-Bukhaariy na Muslim kwa kusema kuwa:

1.  Alichokisema kwa kutumia -Jazm- kwa kutumia matamshi ya namna kama hii: amesema, ameamrisha, ametaja; basi hukumu yake ni sahihi.

 

2.  Alichokisema na akawa hakutumia -Jazm- bali ametumia matamshi ya namna kama hii: imepokelewa, imetajwa, imehadithiwa, na yenye kufanana na haya yenye kuficha Faa’il (Mtendaji) wake; basi hukumu yake ni kuwa Hadiyth hiyo si sahihi, pamoja na hayo hakuna katika Al-Bukhaariy Hadiyth za namna hii bali katika kitabu kinachooitwa Swahiyh.

Tumeeleza kuwa Imaam Al-Bukhaariy ametaja baadhi ya Hadiyth ambazo zinaeleweka na kufahamika kwa wataalamu wa Hadiyth kuwa ni katika ‘Hadiyth Mu’allaq’, Hadiyth hizi zimefanyiwa kazi na kuchunguzwa na kufikia kutwaja isnaad zake kwa ukamilifu bila ya kudondoka msimulizi hata mmoja kama alivyozikusanya al-Haafidh Ibn Hajar katika kitabu chake Tafliyq at-Ta’liyq.

Hivyo ni kusema kuwa hakuna katika kitabu chenye kuitwa Swahiyh Al-Bukhaariy Hadiyth isiyokuwa sahihi.

b- mbona kuna Hadiyth ambazo zinapingana waziwazi na Qur'an tukufu!

Ilikuwa vyema ulete mfano wa Hadiyth kama hizo unazodai, kwani kama tulivyoeleza katika utangulizi kuwa Qur-aan ndio kitabu pekee sahihi juu ardhi hii mpaka mwisho wa dunia; kwa maana kama utapata chochote chenye kupingana na Qur-aan hata kama ni Hadiyth sahihi kama unavodai, basi huwa hakina nguvu wala hakishughulikiwi; wasiwasi wetu ni kuwa huenda ukawa hujaifahamu Hadiyth na hiyo Aayah unayodai kuwa inapingwa wazi wazi na Hadiyth; kwani hata katika Qur-aan  kuna Aayah, kwa uchache wa ufahamu, zinaonekanwa na watu kama wewe kuwa zinapingana wazi wazi jambo ambalo si kweli, na katika Hadiyth pia zipo kama hizo ambazo, hata hivyo kuna fani ya Naasikh na Mansuukh ambayo ina vipengele vyake –kama wahusika watashindwa kuwafikishwa baina ya Hadiyth na Hadiyth au na aya- kimoja wapo ni kuwa Naskh Qur-aan kwa Sunnah Mutawaatir na Naskh Sunnah kwa Qur-aan –kuelekea Baytul Muqadis kumethibiti katika Sunnah pekee na hakuna katika Qur-aan chenye kuthibitisha na Qur-aan ikanaskh kuelekea huko kwa kuwataka kuelekea al-Ka’bah- na Naskh Sunnah kwa Sunnah.

Lakini vipi tutaweza kutegemea Swahiyh Al-Bukhaariy na hali Al-Bukhaariy hajapata kuonana na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)?

Swahiyh Al-Bukhaariy hakusimulia lolote lilotoka moja kwa moja kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), bali amesimulia yaliyotokana na Mashaykh walioaminika waliojaaliwa kupata cheo cha juu kabisa katika kuhifadhi na kuthaminiwa na kuaminiwa. Nao pia wamepokea na kusimulia yale yaliyotokana na Mashaykh kama wao waliotegemewa na kuaminika, na mtiririko wa upokezi (isnaad) imeendelea hivyo hivyo hadi kufika kwa Maswahaba. Namba ya wasimulizi walio wachache kabisa baina ya Al-Bukhaariy na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), ni tatu. Hivyo basi tunamtegemea Shaykh Al-Bukhaariy kwa sababu amechagua wasimulizi ambao amesimulia Hadiyth zao kwa kuchukua hadhari kubwa na walioaminika kabisa. Juu ya hivyo, hakuandika Hadiyth yoyote katika Swahiyh yake hadi kwanza afanye ghusl, aswali Raka'ah mbili za Swalaatul-Istikhaarah, akimuomba Allaah Amuongoze kabla ya kuandika Hadiyth hiyo. Imemchukua miaka kumi na sita kukusanya Hadiyth katika kitabu chake hiki ambacho Ummah mzima umekikubali na wamekubaliana kwamba yaliyosimuliwa humo ni Swahiyh na Allaah Ameuhifadhi Umma huu kutokana na upotofu.

 

Imaam An-Nawawiy (Rahimahu Allaah) amesema katika utangulizi wa Sharh Muslim (1/14):

'Maulamaa (Rahimahumu Allaahu) wamekubaliana kwamba vitabu vilivyo  Swahiyh kabisa baada ya Qur-aan ni Swahiyh Mbili; Al-Bukhaariy na Muslim ambavyo vimekubaliwa na Ummah. Kitabu cha Al-Bukhaariy ndicho kilichoongoza na kilicho na faida zaidi baina ya hivyo viwili"

 

Ukimuuliza Shi'ah (au Raafidhiy) kuhusu kauli ya 'Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) ambazo Maimamu wao wamesimulia, na kauli ya Al-Baaqir na Ja'far As-Swaadiq na wengineo wa Ahlul-Bayt (Rahimahumu Allaahu) ikiwa wamewasikia kutoka kwao au wamesimulia kwa isnaad (mtiririko wa wasimulizi), jibu litakuwa dhahiri. Kuna tofauti kubwa baina ya isnaad ya Al-Bukhaary na isnaad za watu wapotofu ambao hawana dalili ya majina ya wasimulizi katika ripoti zao (masimulizi ya Hadiyth zao) isipokuwa utakuta katika vitabu vyao kuna masimulizi dhaifu, uongo na wasimulizi walio na kasoro. Mwenye kupenda akarejee kwenye vitabu vyao vya Hadiyth vya kutegemewa kama Al-Kaafiy cha Al-Kulayniy na waone vituko humo ndani na matusi na laana kwa Maswahaba na wake za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na shirki tele zilizozagaa.

Tunamuomba Allaah Atulinde na hayo inshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share