Amemuota Aliyefariki Anayemdai Kuwa Anawambia Atoe Sadaka Pesa Zake
SWALI:
ASSALAMU ALYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.
Kuna mtu fulani nilimkopa kiasi cha fedha lakini sikumbuki kiwango lakini hazizidi 5000Tsh. Kwa bahati yule mtu amefariki muda mrefu tena ina fika miaka sita au saba kama sikosei lakini lile deni limenikaa kila nikilifikia sijui nilipeke kwao au vipi. Kwa ule wasi wasi nilonao wa deni la watu nilimuota aliyefariki akiniambia kuwa pesa zake nimtolee sadaqa, kutokana na hali hii sasa jee nimtolee sadaka au nizipeleke kwao halafu niwaelezee jinsi nilivyoota naomba ushauri wenu inshallah ili nipate kutoka kwenye khofu hii. Wabillahi tawfiq.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ndoto.
Ndoto zipo aina nyingi ambazo mwanaadamu huota kwa sababu moja au nyingine. Zipo ndoto ambazo huwa tunaota kwa sababu ya kulifikiria jambo wakati wa asubuhi au mchana au kitu kukuingia sana rohoni au kutamani kitu. Au pia huletwa na shetani ili kukutia wasiwasi katika mambo yako mengi.
Kwa aliyefariki anayekudai ilikuwa akuelezee hayo kuwa umtolee sadaka kabla ya kuaga dunia au atie katika wasiya wake kabla ya kuaga dunia kwake. Pindi anapokufa huwa mali si yake tena bali ya warithi wake. Hivyo, jambo ambalo unafaa kufanya ni kulipeleka deni hilo unalodaiwa na aliyefariki kwa warithi wake kama vile wazazi wake, au mkewe au watoto. Kama hao tuliowataja pia nao wameaga basi kwa nduguze na wala usiwaelezee ndoto yako.
Na Allaah Anajua zaidi