Muujiza Wa Kupasuka Mwezi Na Mnyama Kuzungumza

SWALI:

 

Naomba kufahamishwa kisa ambacho kinasimuliwa sana na watu kuwa mwezi ulishuka na kumshuhudia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wa Allah?

Pia naomba kufahamishwa kama kweli kuwa paa (mnyama) aliwahi kuzungumza na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akimuomba amuombee ruhusa kwa bedui aliyemkamata ili akanyonyeshe watoto wake porini?.

 

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Waumini wa kweli huwa hawana shaka na kila muujiza sahihi uliothibiti kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)

Kupasuka kwa mwezi:

 Suala la kupasuka kwa mwezi na kumshuhudia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni jambo lisilo shaka kwa waumini, Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)  Anasema, "Saa yakufika Qiyaamah) imekaribia; na mwezi umepasuka" [Al-Qamar:1)    

Ukirejea kwenye sababu za kushuka kwa aayah hiyo utakuta zinaeleza wazi jinsi watu wa Makkah walivyomshurutisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) waweze kumwamini, awaoneshe muujiza wa kupasuka kwa mwezi vipande viwili. (Al-Bukhaariy Namba 3637 na Muslim 2800).

Vile vile Imaam Ahmad amerekodi kuwa Jubayr bin Mutw'im alisema: "Mwezi ulipasuka vipande viwili wakati wa Mjumbe wa Allah na sehemu ya mwezi ulikuwa juu ya mlima na sehemu nyingine kwenye mlima mwingine. Wakasema (makafiri) "Muhammad ametufanyia uchawi". Kisha wakasema: "Angeliweza kututeka kwa uchawi asingeliweza kufanya kwa watu wote" [Imaam Ahmad]

Usimulizi wa 'Abdullaah bin 'Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma):

Ibn 'Abbaas alisema: "Mwezi ulipasuka wakati wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) [Al-Bukhaariy na Muslim]

Ibn Jariyr alirekodi kwamba Ibn 'Abbaas alisema kuhusu kauli ya  Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):  

 

 ((اقْتَرَبَتِ السَّاعَةُ وَانشَقَّ الْقَمَر))ُ   (( وَإِن يَرَوْا آيَةً يُعْرِضُوا وَيَقُولُوا سِحْرٌ مُّسْتَمِرٌّ  ))

((Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!))  

((Na wakiona Ishara hugeuka upande na husema: Huu uchawi tu unazidi kuendelea)) [Al-Qamar:1-2]

 

Ama swala lako la pili: kuhusu kisa cha paa ni kama ifuatavyo:

Kisa hicho kimepokewa na Imam At-Twabaraniy na Al-Bayhaqiy na Abuu Nu’aymi kutoka kwa Anas bin Maalik (Radhiya Allahu 'anhu) kutoka kwa Zaid bin Arqam, Na amepokea Imam Al-Bayhaqiy kutoka kwa ‘Aliy bin Qaadim na Abu 'Alaa Khalid bin Tahman-kutoka kwa 'Atwiyah, kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriy; anasema Qutbu al-Hadhramiy katika Khaswais yake ya kuwa, "Baadhi ya wanachuoni bingwa wa kuhifadhi Hadiyth wameidhoofisha hadith hii pamoja na kuwa zikikusanywa njia za mapokezi ya Hadith zinaweza kuipa nguvu" (Mwisho wa kunukuu) Na anasema Hafidh katika kitabu chake Al-aamal-Hadiyth hii ni ngeni - na huyu ‘Aliy bin Qaadim na Shaykh wa Mashaykh zake wote ni watu wa (kufa) Iraq na wote wana walakini. Na kati ya hao mwenye udhaifu zaidi kuliko wote ni 'Atwiyyah-na lau hii Hadiyth ingelifuatiliwa ningeliihukumu kuwa ni Hasan" (Maj-mau Zawaid 8/294)

 

Lakini kuna visa vingine vya wanyama wawili waliozungumza vinavyopatikana katika Sahiyh Al-Bukhaariy Mjalada wa 3 Nambari 517, navyo ni:

 

Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Wakati mtu alikuwa amempanda ng'ombe, alimgeukia na kusema:"Sikuumbwa kwa ajili hii (yaani kumpakia mtu) bali nimeumbwa kwa ajili ya kuambua ardhi". Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaongeza: ((Mimi, Abu Bakar na 'Umar tumeamini kisa (hiki) )). Kisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akaendelea: ((Mbwa mwitu alimteka kondoo na mchungaji alipomfukuza, mbwa mwitu alisema, "Nani atakayekuwa mlinzi wake siku itakayokuwa ya wanyama wa pori wakati hakutakuweko  wachungaji isipokuwa mimi?". Baada ya kusimulia, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Mimi, Abu Bakar na 'Umar pia tumeamini (kisa hiki))). Abu Salama (msimulizi mwingine alisema: "Abu Bakar na 'Umar hawakuweko (wakati huo)"

 

 

Vile vile  imesimuliwa kuwa mbwa mwitu pia alizungumza na mmoja wa maswahaba wa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) karibu na Madiynah kama ilivyohadithiwa na Fat-h al-Baariy.

 

 

Imetoka kwa Unays bin 'Amr:  "Ahban bin Aws  alisema:   'Nilikuwa na kondoo wangu. Mara mbwa mwitu alimteka kondoo nikampigia kelele. Mbwa mwitu akaukalia mkia wake na kuniambia: 'Nani atakayemchunga (yaani kondoo) siku ambayo utakuwa umeshughulika na hutoweza kumchunga? Je unanizuilia rizki ambayo Allah Ameniruzuku?' Ahban akaongeza: "Nilipiga makofu na kusema: Naapa kwa Allah, sijapata kuona jambo la kushangaza na la ajabu kama hili! Hapo mbwa mwitu akasema: 'Kuna maajabu zaidi ya haya, nayo ni Mjumbe wa Allah katika ile mitende akiwaita watu kwa Allah (Kuingia Uislamu)' Unays bin 'Amr aliendelea kusema, "Kisha Ahban akaenda kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumwambia yaliyotokea na akaingia Uislamu". [Sahiyh Al-Bukhaariy Mjalada wa 3 Nambari 517]

 Kisa kama hicho kimesimuliwa kwa usimulizi mwingine kama ifuatavyo:

 

 

Kutoka kwa Sa'iyd al-Khudriyyi (Radhiya Allahu 'anhu) kwamba (mchungaji alipokuwa na kondoo wake) mara mbwa mwitu alimteka kondoo na kukimbia. Mchungaji akamkimbiza mbwa mwitu na akamkamata kondoo wake. Mbwa mwitu akaukalia mkia wake na akamwambia mchungaji: "Mkhofu Allah, unanichukulia rizki yangu Aliyoniruzuku Allah". Mchungaji akasema: "Maajabu haya! Mbwa mwitu amekalia mkia wake na kunisemesha mimi kwa lugha ya binaadamu". Mbwa mwitu akasema: "Nikuambie yaliyo maajabu zaidi kuliko haya? Kuna Muhammad yuko Yathrib (al-Madiynah) anawajulisha watu khabari za kale". Mchungaji akaelekea (Madiynah) akimuendesha kondoo wake hadi akaingia (mji wa) Madiynah. Akamuweka kondoo wake pembezoni akaenda kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuelezea kisa chote. Mjumbe wa Allah, akaamrisha Swalah ya jamaa kisha akamwambia mchungaji awaelezee watu (kisa chake) naye akawaelezea. Kisha Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Yeye (mchungaji) amesema ukweli. Naapa kwa Yule (Allah) Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, Siku Ya Kufufuliwa (Qiyaamah) haitofika hadi wanyama wa kuwinda watasema na binaadamu na fimbo pamoja na nyuzi za viatu vya mtu vitazungumza naye na mapaja yake yatamjulisha kuhusu yanayotokea kwa familia yake (nyumbani kwake) akiwa yeye hayupo)) [Musnad Ahmad Mjalada wa 3]

 

Na Allah Anajua zaidi

 

Share