Swahaba Walikuwa Waaminifu Hakukuweko Na Mnafiki Kati Yao?

SWALI

 

Assalamu Aleikum warahmatullahi wabarakatuhu, niliwahi kusoma katika kitabu cha mwanachuoni Al-Qanduuzil-Hanafiyyi kinachoitwa Yanaabiul-Mawaddah kuwa swahaba mtukufu Abdurahman ibn Awfi aliwahi kutoa maneno ya kibaguzi kwa swahaba mweusi Bilali ibn Rabah kwa kumwambia yaa ibnu Saudaa! Ninapenda kuuliza kuwa je? Huu si ubaguzi ambao umeonyeshwa na swahaba mtukufu ambae ni miongoni mwa waliobashiriwa pepo! Je kutokana na ubaguzi huu swahaba huyu ni mwadilifu kweli? Na je ni kweli kuwa maswahaba wote walikuwa waislamu na hapakuwa na wanafiqi miongoni mwao.


 

JIBU

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu uaminifu wa Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum). Kweli kisa kama hiko kilitokea lakini si ‘Abdur-Rahman bin ‘Awf (Radhiya Allaahu ‘anhu) kama ulivyotaja. Muhimu hilo linatakiwa lifahamike na liwe wazi kwako na kila mmoja wetu. Mabishano yalitokea baina ya Abu Dharr al-Ghifaariy na Bilaal bin Rabaah (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambayo yalimpelekea Abu Dharr (Radhiya Allaahu ‘anhu) kumwambia Bilaal (Radhiya Allaahu ‘anhu) maneno hayo ya mtoto wa mama mweusi.

 

Baada ya maelezo hayo inafaa ifahamike kuwa mambo kadhaa yaliwapitia Maswahaba baada ya kusilimu kwao. Walikuwa na madhambi tofauti na sifa mbaya nyingine ambazo walikuwa wakiishi nazo kutoka katika ujahiliya kwa hivyo nyengine waliendelea nazo walipoingia katika Uislamu kabla ya kuharamishwa. Katika hayo ilikuwa ni unywaji wa pombe ambao wengi wao waliendelea kunywa baada ya kusilimu kabla ya kushushwa Aayah kukatazwa ambayo ni Aayah ya Suratul Maaidah (5): 90-91, na hapo hapo wote wakaacha.

 

Na mara nyingine ni makosa kama haya yanayofanywa kwa ubinaadamu ndio hufanya hukumu iteremshwe na Allaah au itolewe na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Na baada tu ya kupatikana hukumu Maswahaba wote huachana na jambo hilo kabisa. Kwa hiyo, kutokana na kutojua kuwa hilo ni kosa wakati huo Swahaba huo anabakia kuwa ni mwadilifu.

 

Maswahaba wote walikuwa si Waislamu tu bali ni Waumini. Labda tukielewa maana ya Swahaba ndio tutaweza kufahamu kipengele cha mwisho cha swali lako. Swahaba ni yule aliyemuona Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuamini na kufa katika Imani. Unafiki ni kinyume cha Imani na wanafiki walijiingiza katika Uislamu lakini hawakuwa ni Waislamu. Dalili ya hilo ni Aayah inayosema:

 

Na miongoni mwa watu wapo wanaosema kuwa tunamuamini Allaah na Siku ya Mwisho, na ilhali wao si Waumini” (2: 8).

 

Kwa hivyo, hao wanafiki akiwemo mkubwa wao, ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul, hawakuwa Maswahaba. Na hata baadaye, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikatazwa na Allaah Aliyetukuka kuwaswalia wanapokufa (9: 84).

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share