Kundi Tabliygh Liko Katika Shari'ah Ya Kiislam?

 

 Kundi Tabliygh Liko Katika Shari'ah Ya Kiislam?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Hivi kundi la Tabligh ambalo watu wake huzunguka huku na huko kwa ajili ya daawa na kuwataka Waislamu wajitolee baadhi ya siku zao ili wakafundishwe namna ya kujenga na kuimarisha Imani na wakati huohuo kufanya kazi za daawa, kundi hili ni halali kwa mujibu wa sheria za Kiislamu?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Kikundi hiki kilianzishwa na Muhammad Ilyaas ibn Muhammad bin Ismaa‘iyl al-Hanafiy al-Chistiy al-Kandlahawiy huko Sohanpur, India. Yeye mwenyewe alizaliwa mwaka 1303 H (1884 M) na kuaga dunia mwaka 1364 (1944 M).

 

Wao wanasema lengo MOJA kuu katika 'amali zao za kulingania ni “Kuamrisha Mema”.

 

Fikra Na Misingi Yao:

 

a.   Taqliyd (kufuata kibubusa) ni lazima kwa kila mfuasi kufuata wanavyoelezwa na wakubwa zao bila kuhoji wala kutaka dalili.

 

b.  Wanaamini kuwa kutekeleza Usufi ni njia ya kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na kupata ladha na utamu wa Iymaan.

 

c.  Hawakatazi mabaya na maovu, kwani wanasema ya kuwa wakati si muwafaka na munasibu kwa sasa kufanya hivyo. Watakapopata tu wafuasi wengi ndio wataanza shughuli hiyo ya kukataza maovu.

 

d. Hawalinganii katika 'Aqiydah na Tawhiyd. Wanaona mas-alah ya 'Aqiydah yanafarakanisha watu.

 

e.    Ulinganizi wao unategemea kwa kiwango cha juu mno kitabu kinachoitwa 'Fadhwaail Al-A'maal ambacho kimetungwa muasisi wao na kimejaa visa vya kutungwa na Ahaadiyth za uongo na kutungwa.

 

f.  Wanategemea pia zaidi usulubu wa kuhamasisha kwa kutoa visa au Ahaadiyth za kuraghibisha na zile za kukhofisha. Japo Ahaadiyth nyingi wanazotumia na visa hivyo, si sahihi na ni vya uongo.

 

g.  Kila wanapokusanya watu na kutoka kwenda kulingania, huruhusu yeyote kusimama Msikitini na kuanza kulingania japo hana elimu kabisa, hajui hata kusoma Qur-aan wala hata hafahamu kile anachokieleza ilimradi amejaza kichwani anakimwaga hivyo hivyo.

 

h.   

Wanasema wana misingi sita katika ulinganizi wao na mawaidha yao, yaani:

 

[i] Tawhiyd;

[ii] Swaalah;

[iii]Elimu na Dhikr;

[iv] Kumkirimu Muislamu;

[v] Ikhlaasw na Niyah na

[vi] Kutenga wakati kwa sababu ya kutoka (khuruuj fiy sabiyliLlaah).

 

i. Hawaruhusu wafuasi wao kuongeza elimu na wanatazama falsafa za jamii zinazowazunguka.

 

j.  Wanaigawa Dini na kuiweka mbali na siasa. Hivyo, hairuhusiwi kwa wafuasi wao kuzungumzia mambo yanayohusu siasa au yaliyowazunguka katika jamii.

 

k.   Mtu hafanyi Da‘wah katika sehemu yake anayoishi kwa sababu zifuatazo:

 

Allaah Anasema:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ

Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; [Aal-‘Imraan: 110], Yaani nje ya sehemu anayoishi.

 

Wanaona bora zaidi kuwafanyia Da‘wah watu wasiojua udhaifu wao kwani huenda wakakosolewa na kupingwa, hivyo wanakwenda kwa watu wa mbali kwa sababu wanaona hao wasiowajua wanaweza kujibu mwito haraka zaidi.

 

I.    Wana misimamo ya kuwatweza shakhsiya wa Da‘wah ya kweli na Wanachuoni walioleta mabadiliko wa Kiislamu walioleta mabadiliko makubwa Ulimwenguni, mfano Muhammad ibn ‘Abdil-Wahhaab, na kadhalika.

 

Njia Wanazotumia:

 

i.    Wamejiwekea nidhamu maalum ya kutoka kufanya Da'wah yao kwa kujiwekea masiku maalum, kuanzia ima siku tatu, au arubaini au miezi minne.

 

ii.   Msafara: Baada ya kusajili majina kwa ajili ya programu za Da‘wah, wanagawanywa makundi na kuambiwa sehemu watakayo kwenda kwa muda uliopangwa au waliojitolea.

 

iii.  Jawlah: Kwa kawaida katika ada zao baada ya Swaalah ya Al-‘Aswr wanakwenda kuwatembelea Waislamu katika nyumba zao na kuwaalika kwa ajili ya muhadhara baada ya Maghrib.

 

Kasoro:

 

  • Wanatilia maanani zaidi misingi sita, hivyo kuifanya Da‘wah yao kuwa finyu isiyokamilika.
  • Taqliyd inayofuatwa na wafuasi wao inakwenda kinyume na amri ya al-Ittibaa‘(kufuata kama ilivyokuja katika Qur-aan na Sunnah)
  • Kukataza Ijtihaad ni kinyume na ukamilifu wa Dini hii ya Kiislamu ya kutatua matatizo mapya yanayochepuza kila wakati.
  • Wanawawaidhia watu ambao wanasimamisha Swalah vilivyo, badala ya wale wasiofuata Dini.
  • Hawajishughulishi na mambo ya msingi ya Dini kama 'Aqiydah na Tawhiyd na aghlabu wanakubaliana na kila kundi potofu na hata kushirikiana nao.
  • Kufuata amri ya Jihaad kwao wanailetea taawili na ufahamu ulio kinyume unaoleta tashwishi katika akili za Waislamu.
  • Kule kuruhusiwa wafuasi wao kuzuru Israel bila ya matatizo yoyote inatia wasiwasi katika nyoyo za watu.
  • Kutohimiza kutafuta elimu kunakwenda kinyume na kiini cha Uislamu ambayo inasisitiza kusoma.
  • Kutokataza kwao maovu kunakwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah.
  • Wengi wanaotoka kufanya Da‘wah hawana elimu hivyo kutopata faida ya elimu. Mara nyingi wanatumia visa visivyokuwa na msingi wowote na wanatumia sana kitabu chao kiitwacho ‘FADHWAAIL AL-A’MAAL’ ambacho kimejaa visa vya uongo na Hadiyth nyingi sana dhaifu na za kutungwa.

 

Da‘wah na Tabliygh (ufikishaji) ni jambo muhimu sana kwa Muislamu kutekeleza lakini lina masharti yake, moja wapo ikiwa ni elimu ya Uislamu na uwe na elimu vilevile na lile unalowawaidhia watu. Kundi hilo la Tabliygh lina vikwazo vya elimu sahihi ya kuutangaza Uislamu. Mara nyingi wanatoa tafsiri au maelekezo yaliyo kinyume na Uislamu sahihi. 

 

Na zaidi wana mielekeo ya kisufi kama alivyokuwa muasisi wao. Hivyo, ni bora mtu kuchukua tahadhari na kujiweka mbali nao isipokuwa yule mjuzi wa Dini awalinganie ili kuwapatia elimu na kurekebisha makosa yao. 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

Share