Wasiwasi Wa Shaytwaan Unamfanya Afikirie Mambo Ya Kufru, Afanyeje?
SWALI:
ASALAMU ALAYKUM.
Swali Langu hili, kwa kawaida huwa ninaposoma, mambo ya dini kwa mfano makala ua ninapo sikiliza mawaidha au kusoma Qur-ani hutokezea ndani ya nafsi yangu kusema jambo hili ni uongo yaani huwa sitamki mdomoni mwangu moyo tu hunipiga paa nakusema iwe Mtume Swala lwahu Alayhi Wasalamu amesema hivi haiwezekani. Halafu hushtuka na kusema ASTAHAFIRULLAH. Naomba jawabu ndugu zanguni Waislamu. NIFANYE NINI MIE JAMANI? Kwa sababu hujihisi ibada zangu zote zinaharibika.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutiwa katika wasiwasi. Hakika wasiwasi huu unaingizwa bila ya kuwa na haja katika hilo. Hata hivyo, wanadamu huwa wanaingia katika mtego huo kwa sababu moja au nyingine. Wasiwasi huu huingia kwa mwanaadamu, hasa akiwa:
- Hakupata malezi mazuri ya Kiislamu.
- Hasomi adhkaar zinazotakiwa kusomwa kila siku.
- Kusoma Qur-aan bila kuelewa.
- Marafiki wabaya ambao wanamuamrisha maovu na mabaya.
- Kufuata matamanio yake mwenyewe.
Kitu ambacho unatakiwa kufanya ni kama ifuatavyo:
- Kujiweka katika kundi la watu wema wenye kufanya ‘Ibaadah inavyotakiwa.
- Kusoma Qur-aan kila wakati pamoja na kujua maana yake na kufanya juhudi ya kufuata yaliyo ndani yake.
- Kusoma adhkaar za asubuhi na jioni. Ingia katika kiungo kifuatacho:
027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni
Na du’aa zote nyinginezo unazohitaji katika hali yako utazipata katika kitabu kifuatacho:
Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)
- Kusoma asubuhi, jioni na hata wakati wa kulala Suratul Iklaasw na Mu'awadhdhatayn (Qul A’udhu birabbil Falaq, na Qul A’uudhu birabbin Naas) mara tatu tatu.
- Kusema A'udhu Billaahi unapoingia wasiwasi.
- Kuzidisha ‘Ibaadah kama ya Swalah na funga.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akuondoshe katika wasiwasi ulionao na akuweke katika hali ya Imani ya daima na Akuongoze wewe na sisi katika njia Yake nyoofu.
Na Allaah Anajua zaidi