Anaishi Nchi Zenye Maasi Anajizuia Anaomba Toba Lakini Anasumbuliwa Na Khofu Aliyonayo

 

SWALI:

 

Asalamu aleikum swali langu ni juu ya mimi kijana wa umri 28 na sina mke nafuata dini yangu alhamdulilah lakini shida niko nayo ni kuwa nchi hii holland kuna maasi nyenge sana kwenye tv, internet na pia njiani najaribu sana kujizuia na pia kufunga naafila pia lakini mara kwa mara naingia maasi ya fahisha lakini siyo zina naomba toba kila mara lakini baada ya muda tena vili vili na toba tena, lakini sasa naogopa kwa sababu imekuwa kama kawaida na ina nisumbua kwa ibada naona kwamba hii ni tabia ya kimunafiiq.

Naomba advice yenu kidugu inshaallah.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuingia katika maasiya.

Hakika ni kuwa mara nyingi watu hufanya makosa kwa kuamua kuhama nchi zao na kukimbilia Ulaya. Nchi ambazo kabla hatujakwenda tunajua dhahiri kuwa maasiya ni mengi na hakuna nidhamu kabisa ya kimaadili mbali na kuwa wameendelea kimada. Tunakuja kujipata mashakani baada ya muda wa kuishi huko na hatuna njia ya kujitoa.

 

Kuna njia nyingi ya kujiepusha na maasiya kabla hujatumbukia ndani yake na hasa hali uliyo nayo. Njia ni kama zifuatazo:

 

1.     Kuoa, nayo ni amri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ndio njia nzuri kabisa ya kukuwezesha kujizuilia na maasiya hayo. Hivyo, nasaha yetu ni kuwa ikiwa una uwezo wa kumueka mke basi fanya hima utekeleze hilo.

 

2.     Kufanya usuhuba mkubwa na Kitabu cha Allaah Aliyetukuka na Sunnah za Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani kufanya hivyo kutakupatia kinga. Unatakiwa usome, uelewe na ujue maana ya unayosoma na kujitahidi sana kufuata kimatendo unayosoma.

 

3.     Kusoma visa vya Maswahaba na watangu wema wa zamani na sasa jinsi walivyoepukana na maasiya katika maisha yao.

 

4.     Kufunga, japokuwa unasema unafunga lakini inaonyesha unahitaji kufanya bidii kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuambia kuwa kufanya hivyo ni kinga.

 

5.     Kufanya urafiki na marafiki wema na wazuri na hata kuishi nao katika nyumba moja, kwani Muislamu ni kioo kwa Muislamu mwenziwe. Ukiwa na marafiki hao watakusaidia sana katika kujiepusha na maasiya.

 

6.     Jaribu kujishughulisha na mazoezi na michezo inayokubalika kisheria, Unaweza kwa wakati wa faragha kufanya zoezi la kukimbia, au kwenda gym, ilimradi ujishughulishe.

 

7.     Kujifungamanisha na Msikiti au Markazi ya Kiislamu hata kama iko mbali kidogo kwani hapo mtakuwa mnatapa darsa ya kuwaepusha na maradhi na ugonjwa wa maasiya.

 

8.     Kukumbuka mauti na kuwa utakutana na Mola wako Mlezi.

 

Ama kuhusu kukosea na kurudia tena maasiya ni ada ya mwanaadamu na Allaah Aliyetukuka Anampenda Anayefanya makosa sio kwa makusudi anayerudi haraka kutaka msamaha. Na mara nyingine zinakuwa ni pepesi za Shaytwaan hivyo unatakiwa usome Adhkaar na asubuhi na jioni kila siku na nyinginezo ambazo zinapatikana katika kitabu hiki ndani ya Alhidaaya:

 

Hiswnul Muslim

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share