Kutoa Aibu Ya Mtu Bila Ya Kumtaja Ni Kusengenya?

SWALI:

 

 

Allah ajaalie kila la kheri kwa kuweka nafasi hii ya kuweza kuuliza maswali. Suala langu ni hili. Ikiwa umekaa na wenzio na ukatoa aibu ya mwengine kwa wale wenzio lakini hukuwatajia jina. Je nini hukumu yake? Yaani itakuwa ndo ushasengenya hapo au vipi. Naomba jibu

 


 

 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutoa aibu ya mtu bila ya kumtaja jina lake.

 

 

Hakika ni kuwa ikiwa mtu huyo ni mwenye kufanya maasiya ya wazi kabisa na amezungumziwa bila ya kujirekebisha na huenda akawaathiri wengine, basi kumtaja kwa jina ili kuwatahadharisha wengine wasikumbwe na anayofanya wala kuathiriwa naye itakuwa inakubalika kisheria. Kwa ajili hiyo Allaah Aliyetukuka Akawataja watu wa maasiya kama Abu Lahab kwa jina. Na pia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawataja watu hao wa maasiya kwa majina yao kwa Hadiyth zake kadhaa.

 

Ama kwa kawaida, Muislamu haifai kumtaja Muislamu mwenziwe kwa yale anayofanya hasa ikiwa anafanya kwa siri. Na ndio Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawa anawarekebisha watu kwa kupiga mifano bila ya kutaja majina yao. Kwa mfano, inakuwaje watu wanaendelea kufanya kadhaa na kadhaa, au wale wenye kufanya kadhaa si miongoni mwa wa bora wenu. Hivyo, ikiwa utazungumza makosa ya mtu bila ya kumtaja mtu kwa jina lake haina neno kabisa katika Uislamu na sheria.

 

Na Imaam an-Nawawiy ana mlango katika kitabu chake cha Riyaadhw asw-Swaalihiyn (mlango wa 256) – Mlango kwa Yanayoruhusiwa katika Kusengenya. Hapo ndani zipo Hadiyth nyingi miongoni mwayo ni ile ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kuwa Hind, mke wa Abu Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alimwambia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

Hakika Abu Sufyaan ni mtu bakhili, naye hanipatii pesa za kunitosha mimi na watoto wangu ila ninachochukua kutoka kwake, naye hajui?” Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Chukua kinacho kutosha kwa wema” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa faida zaidi kuhusu mada ya usengenyaji, soma makala ifuatayo:

 

Madhara ya Ghiybah

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share