Amemkhini Mumewe, Amefanya Machafu Mengi, Kazini Katoa Mimba Huku Mume Hajui, Je,Talaka?

SWALI:

 

Mimi nina suala rafiki yangu kanituma nimuulizie suala lenyewe ni hili anasema yeye sasa hivi kashaolewa lakini katika utoto wake alifanya mambo mengi machafu ya kuwa na wanaume pamoja na kuzini nao, na na akawahi kuchukuwa mimba ya mwanamme wake mmoja kabla hajaolewa kwa bahati nzuri, akapata rizki ya mume na akaolewa lakini ile mimba alikuwa nayo bado baada ya wiki alikwenda kuitowa jee ndoa yake ina sihi ama vipi, hiyo mimba sio ya huyo mume alomuowa ni ya mtu mwengine lakini mumewe mpaka leo hajamwambia kuhusu kitu hicho, sasa kama nilivokwambia kuwa kashaolewa kakaaa na mumewe kwa muda kama wa mitano akakutana na bwana wake wa zamani kwa bahati mbaya akazini nae mara mbili, lakini mumewe hajui alikuwa ana wasi wasi mkubwa kuhusu suala hilo akamwambia kama kashawahi kumuendea kinyume ndani ya ndoa yake hamsamehe na tokea siku alomuendea kinyume si mke na mume wanazini tu na anaogopa kwa sababu mumewe anampenda mpaka leo jee ndoa anayo na afanye nini naomba jawabu


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu zinaa kwa mwanamke aliyeolewa. Awali ya yote ni kuwa huyo rafiki yako amefanya madhambi kabla ya kuolewa na hata baada ya kuolewa. Kisha amemwendea kinyume mume ambaye anampenda sana kama ulivyoandika, ingawa hatudhani kuwa ni hivyo kwa sababu vipi ampende mumewe kisha amuendee kinyume?

 

Maasi hayo aliyoyafanya, inafaa yeye afanye yafuatayo ili apate kusamehewa na Allaah Aliyetukuka:

 

1.     Kuacha maasiya.

2.     Kujuta kwa kufanya kosa hilo.

3.     Kuazimia kutorudia tena kosa hilo.

4.     Na ikiwa kosa lenyewe linamhusu mwanaadamu ni lazima apate msamaha kutoka kwa aliyemfanyia.

 

Sharti moja likikosekana basi toba yake haikubaliwi. Kwa sababu hapa kosa alimfanyia mumewe inabidi apate msamaha kutoka kwake. Hata hivyo, suala hilo linakuwa ni shida kwani linaweza kutokea lolote endapo atataka kumweleza mumewe ukweli. Hivyo anachotakiwa kufanya ikiwa atachelea madhara kutoka kwa mumewe, inabidi awe ni mwenye kumtendea wema kila wakati ili Allaah Aliyetukuka Amtazame kwa jicho la huruma na kumsamehe.

 

Mwanzo inatakiwa mwanamke huyo apewe nasaha kuhusu aliyoyafanya na awe na nia ya kujirekebisha na kufanya mema kwa wingi sana kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Mche Allaah popote ulipo na fuatisha baya kwa zuri, nalo litafuta (hilo baya)" (at-Tirmidhiy).

 

Tunatumai kwa kufanya hivyo kwa ikhlaas na nia nzuri basi Allaah Aliyetukuka Atamsamehe na kumsaidia katika kubadili aliyo nayo.

 

Ama kuhusu ndoa yao ni sahihi wala mke hawi ameachwa kwa kufanya makosa kama hayo ya zinaa. Ndoa itakuwa ipo lakini mwanamke atakuwa amefanya madhambi makubwa na lau kutakuwa na sheria ya Kiislamu basi alikuwa auawe kwa kosa hilo. Tafadhali mpe majibu yafuatayo apate kuzingatia maasi makubwa hayo:

 

Nini Hukumu Ya Mwenye Kuzini Kwa Siri?

 

Kutoa Mimba - Hukmu Na Kafara Yake

 

Nimekwenda Nje Ya Ndoa, Nimjulishe Mume Wangu?

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share