Naogopa Kuolewa Kwa Sababu Ya Maumivu Baada Ya Kitendo Cha Ndoa

SWALI

 

Asalam alaikum. Nashukuru mungu kupata fursa ya kukuandikieni. Mimi mi mwana mama wa miaka 28 na nina watoto watatu na ni meisha olewa mara mbili sasa nimeachika hivi nimepata watatu anataka kuniowa ila naogopa kutokana na matatizo nilio nayo. Tatizo langu nipale tunapo taka kufanya tendo landowa basi niumivu makali ninabaki nayo sehe zangu za siri hata mara yapili sikubali hadi nishikwe kwa nguvu. Nami yaniuma sana hiyo nimetembea sana kwa madaktari ila sijafanikiwa wananambia sina tatizo. Nami hamu ya mume naisikia ila tatizo ni hilo sijuwi niolewe ama niache na tena. Hizi nchi za ulaya wanajitahidi kwa matibabu lakini imeshindikana. Je nitapata zambi nikikata kuolewa.


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuolewa na kuwa na maumivu wakati wa kufanya kitendo cha ndoa. Ni vyema tufahamu kuwa ndoa katika Uislamu imegawanyika katika vigawanyo vifuatavyo:

 

  1. Faradhi ya Lazima: Ikiwa mwanamme au mwanamke hawezi kujizuilia bila ya mke au mume basi kumuondosha kuingia katika uzinzi inakuwa lazima kwake aoe au aolewe.

 

  1. Haramu: Ikiwa mwanamme au mwanamke hawezi kumtazama kindoa wa pili wake na kumtosheleza kistarehe basi kwa njia hiyo inakuwa kuoa au kuolewa ni haramu. Sababu kubwa ni kuwa mmoja ikiwa hataweza kumtosheleza mwingine, basi wa pili anaweza kuingia katika madhambi ya zinaa.

 

  1. Sunnah Kubwa: Kwa yule ambaye anaweza kujizuilia lakini ana uwezo wa kuoa au kuolewa basi ni vyema afanye hivyo kwani hiyo inamleta karibu na maelekezo ya Mitume na watangu wema. Na kuiacha bila sababu ni dhambi kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amehimiza sana.

 

Tukija kwa swali lako, dada yetu ni muhimu kabla ya kuingia katika ndoa hii ya tatu utafute matibabu tena ili uwe katika hali nzuri. Inaonekana pia kuwa hizo ndoa mbili za mwanzo zilivunjika kwa kutoweza kuwatimizia waume zako.

 

Ni nasaha zetu kuwa usiingie katika ndoa hii mpaka upate matibabu. Na hakuna ugonjwa isipokuwa una dawa yake. Huenda tu madaktari hao hawajaweza kujua sababu ya maumivu yako. Mara nyingine madaktari hawa wa Ulaya waliobobea katika nyanja nyingi hushindwa kutibu magonjwa mengine. Na magonjwa hayo ya kike kama yako hutibiwa na matabibu wa Kiislamu kutumia elimu pana ya matibabu ya Kiislamu. Tungekunasihi lau utakuwa na safari ya kwenda nyumbani, kwani tunaona kuwa labda unatoka Afrika Mashariki na matibabu haya hupatikana. Ikiwa huwezi kwenda unaweza ukazungumza na jamaa yako sehemu hizi ili aende kwa tabibu aina hiyo na suala lako likawa rahisi.

 

Pia tungekunasihi kuwa kabla ya kukubali au kukataa, taka shauri kutoka kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuswali Swalah ya Istikhaarah. Pia inuka usiku wa manane uswali Swalah ya Tahajjud, na unyenyekee mbele ya Allaah Aliyetukuka umuombe Akupe takhfifu na dawa kwa ugonjwa wako. Tuna hakika kuwa ukifanya hivyo, basi utapata ufumbuzi wa tatizo lako.

 

Ikiwa hukupata nafuu basi huo ni mtihani kutoka kwa Allaah Aliyetukuka na unatakiwa usubiri kwa kiasi kikubwa katika mtihani huo. Sasa ikiwa utabaki katika hali hiyo na unaona huwezi kukaa bila ya mume, inatakiwa mume aelewe hali yako kwa kumuelezea kwa uwazi hali hiyo ili msiwe ni wenye kusumbuana baada ya kuoana.

 

Twakutakia kila la kheri pamoja na ufumbuzi wa ugonjwa wako huo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share