Mume Anamuingilia Njia Isiyo Ya Halali Kwa Nguvu, Anaogopa Kudai Talaka Asije Kuzini

SWALI:

 

Assallam allaykum warahmatullah wabarakatu. Napenda kumshukuru muumba aliyenipa uwezo wa kuandika swali hili leo hii. Mimi mume wangu anatabia hiyo ya kuniingilia kinyume na maumbile, humkatalia lakini ananifanya kwa nguvu na pia nilisha jaribu kudai talaka lakini hataki kunipa na pia kinachoniogopesha nisije nikaachwa halafu ikapelekea kufanya maovu eidha kuzini na mengineyo maana sisi wanaadamu hatuko sawa. Pia mume wangu nampenda isie akanipa talaka halafu nikazini nae je nifanye nini? Naomba ushauri wenu. Mungu anajua zaidi.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola

i wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuingiliana kinyume na maumbile baina ya mume na mke. Kulingana na swali lako ni kuwa wewe hutaki kufanya hivyo lakini ni mume ndio mwenye kukufanya hilo kwa nguvu. Ikiwa hivyo unavyosema ni kweli basi wewe utakuwa huna madhambi na mumeo ndio atakayebeba dhambi la kutekeleza hilo. Tufahamu kuwa jambo hili lina madhambi makubwa na wala tusichukulie mzaha. Katika Hadiyth kadhaa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia yafuatayo:

1.      "Allaah Hatomtazama mwanamume mwenye kumuingilia mkewe kwa nyuma" (an-Nasaa'iy na Ibn Hibbaan kwa Isnadi nzuri).

 

2.      "Amelaaniwa mwenye kumuingilia mwanamke kwa nyuma" (Ahmad, Abu Dawuud na Ibn 'Adiy).

 

 

3.      "Mwenye kumuingia mwenye hedhi au mwanamke kwa nyuma au kumwendea mchawi na kumuamini kwa anayosema basi amekufuru kwa aliyoteremshiwa Muhammad" (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah, na Isnadi yake ni Sahihi).

 

4.      "Twaawuus amesema: 'Ibn 'Abbaas aliulizwa kuhusu mtu anayemuingilia mkewe kwa nyuma'. Akasema: 'Huyu ananiuliza kuhusu ukafiri'" (an-Nasaa'iy).

 

Kwa njia hiyo utakuwa huna budi kukataa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo ni,

"Hakika utiifu ni katika wema".

Na pia, "Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba".

Na kwa nini ukhofu kuwa ikiwa utaachwa hutoolewa tena. Muislamu mwenye Imani yake kikamilifu huwa hakhofu katika mas-ala ambayo ni ya kumtii Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani anajua kuwa hataachwa kuteseka.

Hebu fikiria sana kabla ya kuolewa na mumeo huyo, je, ullijua kuwa yeye ndiye atakayekuwa mumeo?

Na ujue ya kwamba, hutoacha kitu kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka isipokuwa utapatiwa badali ambayo ni bora zaidi. Hiyo ndiyo iliyokuwa dhana ya Ummu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipoaga dunia mumewe Abu Salamah (Radhiya Allaahu ‘anhu), yeye alidhania kuwa hatopata mume kama huyo mumewe wa kwanza lakini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia aombe kwa Allaah Aliyetukuka Ampe mume bora kuliko aliyeondoka. Du’aa yake ilijibiwa na akawa ni mwenye kuolewa na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

Nawe lazima upige moyo konde na utafute njia ya kuepukana naye kwani kukaa naye inaonyesha unaridhia madhambi hayo na huenda ukawa unapata madhambi sawa na mumeo. Msamaha wa Allaah Aliyetukuka hauji ila mtu anapojiondosha katika maasiya.

 

Yale ambayo unafaa uyafanye ni kama yafuatayo:

 

1.      Uzungumze tena na mumeo kuhusu hilo na kuwa kama Waislamu hamufai kufanya hilo.

 

2.      Ikiwa bado anaendelea itabidi ulifikishe jambo hilo kwa wazee wako na wake na muwe ni wenye kufanya mkutano kuhusu suala hilo na pia umhame katika malazi ili asije akakuingilia kwa nguvu. Ikiwa bado inaonekana kuwa hataki kufuata wasiya wa wazee basi idai talaka ili usiwe tena chini ya amri yake.

 

3.      Ikiwa hakukupatikana ufumbuzi wowote itabidi uende kwa Qaadhi au Shaykh kwenye eneo lako ili asikilize kesi yenu na atoe uamuzi.

Ikiwa anaendelea na hilo utakuwa dada yetu huna budi kuomba talaka kutoka kwake. Inabidi uchague mambo mawili: ima umridhishe yeye au Allaah Aliyetukuka, Muumba wako. Je, wewe umechagua nani kati ya hao wawili? Uchaguzi ni wako wala sisi hatuwezi kukulazimisha, ila tu tunaweza kukunasihi katika njia iliyo bora duniani mwako na Akhera.

Ikiwa kwa hakika utaweza kufanya hivyo basi Imani yako itakuwa ni thabiti na hutoingia kwenye zinaa pia InshaAllaah. Allaah Atakupatia badali ambayo ni bora zaidi na mume aliye bora kabisa kuliko huyo wako wa awali. Huu ni mtihani kwako, je, utaupita? Au utafeli.

Kuweka dhana zako na imani kuwa ukiachwa utatumbukia kwenye zinaa, huo ni udhaifu wa kiimani na kukosa elimu ya ubaya na madhara ya zinaa. Kama utakuwa na elimu nzuri ya ubaya na makatazo na uharamu wake, hatudhani kabisa kama unaweza kulifikiria jambo hilo kabisa.

Soma kuhusu ubaya, madhara na uharamu wa zinaa katika viungo hivi:

Binti Mwenye Kufanya Maasi Ya Zinaa

Pia soma haya hapa chini kuhusiana na Liwati na umpe mumeo asome vilevile ili aone makemeo na laana zilizomo za kitendo hichi kichafu kabisa:

Kuharamishwa Liwati

Mume Wangu Ananitaka Njia Isiyo Ya Halali

Amemuingilia Mkewe Kimakosa Nini Hukmu Yake?

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share