Hawezi Kujizuia Kufanya Zinaa, Je Anaweza Kufanya Ndoa Ya Siri Bila Wazazi Kujua?

SWALI:
 
Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28. Nipo katika tatizo kubwa linalo nisumbua sana. Ndugu zangu katika Uislam niko katika zinaa na nashindwa kujizuia nataka kuacha nashindwa naombeni msaada wenu. nataka kufunga ndoa ya siri bila kumjulisha mzazi wangu mpaka pale mambo yakiwa tayari. Je shekhe au imam anaweza kuwa walii wangu je marafiki zangu wanaweza kuwa shahidi zangu. kama point ya walii ni kuhakikisha mume anayekuoa ni mwenye hekima huyu niliye naye ana hekima. je nikifanya hivyo ni halali. Kuna dua ambazo naweza kusoma nikaacha zinaa. Nifanye kitu gani kukontrol nafsi yangu.
 
 
 
JIBU:
 
 
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihiwasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
 
 
 
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Mwanzo ieleweke kuwa zinaa ni miongoni mwa madhambi makubwa ambayo Muislamu anafaa atie juhudi kujiepusha nayo. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuhimiza hata tusiikaribie seuze kukifanya kitendo chenyewe. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
 
Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).
 
Adhabu yake pia ni kali kwa kufanya kitendo hicho kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
 
Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini” (24: 2).
 
Tufahamu kuwa hii ni adhabu kwa wanaofanya hivyo ikiwa hawajaoa au kuolewa.
 
Hakika ni kuwa hilo lako ni tatizo kubwa kama ulivyosema hasa unapojua kuwa hiyo ni dhambi kubwa, yenye adhabu kali na pia ukumbuke kuwa hapa duniani pia kuna adhabu ya yale magonjwa yanayosababika kutokana na kitendo hicho. Fahamu dada yetu kuwa kujua tatizo ni nusu ya kulitatua lakini inahitajia hima na shauku kubwa kutoka kwako. Hatudhani kama kuna tatizo ambalo mwanaadamu mwenye nia atashindwa nalo. Ikiwa kweli nia ipo basi Allaah Aliyetukuka Atakusaidia kwani Anatuambia:
 
 
Hakika Allaah Habadili yaliyoko kwa watu mpaka wabadili wao yaliyomo nafsini mwao” (13: 11). Lazima ufanye juhudi kubwa ndio uafikiwe bila ya hivyo tatizo hilo litakuandama mpaka kaburini.
 
Msaada tunaoweza kukupatia ni kuachana haraka sana na huyo kijana, na kurudi kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa kufanya toba ya kweli kabisa na kuzidisha sana Ibaadah, kukaa na wasichana wa Kiislamu walio wema, kuwa na marafiki wazuri, kuolewa haraka ndoa ya sawa, kuleta istighfaar, kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa wingi akuondolee shida hiyo, inuka usiku kwa ajili ya Tahajjud na umlilie Mola wako Mlezi Akutoe katika janga ulilo nalo. Katika suala hilo hakuna upenyo wala njia ya mkato wala miujiza, kunatakiwa juhudi na tawfiki inayotoka kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala).
 
Tuna mashaka kama umeshindwa kuacha bali tunahisi kuwa hujataka kidhati kuacha madhambi hayo ya zinaa. Kama kweli ungekuwa unataka, ungekuwa ushachukua uamuzi kabla hata hujaleta swali lako hili. Lakini hata hivyo, bado hujachelewa sana, bado unaweza kuoa maamuzi haraka baada ya kupata haya majibu yetu inshaAllaah na ukafanya toba ya dhati na kufuata hayo maelekezo hapo juu.
 
Shaykh au Imaam hawezi kuwa walii wako kwani sheria ya Kiislamu imeweka mfumo wake wa uwalii. Walii mwanzo anakuwa baba, akiwa hapatikani au amefariki basi babu mzaa baba, ikiwa naye hapo utashikwa uwalii na kaka zako shakiki (Shaqiyq), ikiwa huna basi ami zako (ndugu wa babako). Ikiwa hawa hawapatikani au wamefariki basi jamaa zako wa karibu. Ikiwa huna kabisa wote hao basi Qaadhi, Shaykh au Imaam wa Msikiti unaoswali atakuwa walii wako.
 
Bila shaka ndoa kama Ibaadah nyingine yoyote ina masharti kwa kusihi kwake. Miongoni mwa masharti ya kusihi ndoa ni yafuatayo:
 
  1. Walii wa mwanamke kupatikana.
  2. Mashahidi wawili waadilifu.
  3. Kukubali kwa mume na pia mke.
  4. Mume kulipa mahari waliyokubaliana na mkewe.
 
Ikiwa hao marafiki zako ni waadilifu katika muono wa Kiislamu wanaweza kuwa mashahidi katika ndoa yako.
 
Ama kuhusu ibara yako kuwa kama point ya walii ni kuhakikisha,fahamu kuwa suala la walii si kuhakikisha tu bali ni kuhakikisha kwanza mume atakayekuoa ni barabara na kuona haki zako umepatiwa. Na hapa tunaona kulingana na swali kuwa wewe hukuweza kuhakikisha wala hao unaotaka wawe mawalii wako. Wewe kisha utahakikishaje na ilhali umempenda huyo mvulana na ukasahau kuwa hata hekima unayosema anayo kuwa hana? Vipi atakuwa na hekima ilhali amevuka mpaka uliowekwa na Allaah Aliyetukuka? Au kwako hekima ni nini? Kama kweli huyo umtakaye angekuwa na hekima basi hangezini nawe hata siku moja bali angetumia kila njia kuepukana na dhambi hilo kubwa.
 
Jambo ambalo ni busara kwako la kufanya ni wewe kuwaambia wazazi wako kuwa unataka kuolewa na hapo uolewe kulingana na sheria ya Allaah Aliyetukuka. Usiendelee kubaki katika dhambi na jaribu uzungumze na huyo kijana ikiwa naye pia ana busara kwa kumwambia kinaganaga kuwa hamuwezi kuendelea katika hali ya madhambi na mshauri afanye toba haraka kama ambavyo unatakiwa nawe ufanye.
 
Tambua na ufahamu dada yetu kuwa unachofaa kuangalia kwa mume ambaye unataka akuoe ni zaidi Dini yake na maadili yake. Ikiwa anatekeleza Ibaadah, anajiepusha na maasiya au ni kinyume na sifa hizo alizotuarishia Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
 
Ama kutaka kwako kufanya hivyo (kuolewa) bila idhini ya wazazi (hasa baba) si halali kwako ikiwa kweli unamcha Allaah Aliyetukuka.
 
Hakuna du’aa maalumu ya kusoma ili uache zinaa bali unatakiwa umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Akuepushe na hilo baada ya kila Swalah na mengineyo ya kufanya kama tulivyotaja hapo juu. Hakika ni kuwa ukiifuata sana nafsi yako basi utakuwa umeifanya ni mungu na hilo ni jambo ambalo Muislamu hafai kuridhika nalo. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:
Je! Umemwona aliyefanya matamanio yake kuwa ndiye mungu wake” (45: 23).
 
Kwa hiyo, wewe kama Muislamu usiingie katika sifa hiyo mbaya ambayo inamuweka mtu mahali pabaya sana.
 
Mambo ambayo unahitajika kufanya mojawapo ni kufanya Ibaadah sana na kujaribu sana kujiepusha na maasiya aina tofauti pamoja na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala)kwa dhati mno Akuepushe na madhambi hayo na mengineyo. Pia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia dawa kabambe ya zinaa pale aliposema: “Enyi kongamano la vijana! Mwenye uwezo wa kuoa basi afanye hivyo, kwani huko kutamsaidia kuinamisha macho (chini) na kuhifadhi tupu. Kwa yule asiyeweza basi afunge, kwani hiyo ni kinga kwake” (al-Bukhaariy na Muslim).
Hapa tunaelezewa mambo mawili muhimu sana kuweza kujizuilia na zinaa:
 
  1. Kuoa au kuolewa kunamkinga mvulana au msichana na mengi ya madhambi. Kwako dada yetu ufanyie haraka hilo kwa kuwaambia wazazi.
  2. Kufunga Swawm, nayo ni kinga nzuri sana.
 
Tunakuombea kila la kheri kuweza kupambana na mtihani ulionao. Na tunakunasihi tena na tena achana haraka na kijana huyo na urudi kwa Mola wako na ukithirishe sana du’aa na Ibaadah.
 
Na Allaah Anajua zaidi
 
Share