Kulala Pamoja Bila Ya Kufunga Ndoa

SWALI LA KWANZA:

Ni ipi hukumu ya mtu anayelala chumba kimoja na mchumba wake na kufanya nae mambo yote bila ya kuoana?.

 

SWALI LA PILI:

Jee kijana mwana mme kama anataraji kumuoa binti wa kike lakini bado hajakubaliwa na wazze wa mwanamke vipi ni vizuri kuwa wana fanya kila kitu pamoja, kwa mfano kulala chumba kimoja, na tuna ambiwa kuwa mwana mke anatakiwa astiri body yake yote ispokuwa viganja na uso tu. Na watu hawa wana lala chumba kimoja sasa itakuwa vipi hukumu ya watu hawa wawili

 

 


JIBU:

Sifa zote njema anastahiki Allah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum)  na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Jambo hili hakika ni la kusikitisha kuona ndugu zetu hawatambui sheria za Mola wao, na hii bila shaka ni kutokana na kuigiza makafiri mila na desturi zao ambazo kwao ni kawaida kuishi kama wanyama bila ya kutambua mipaka katika maisha yao.

Mtu huyo kisheria anahesabika kuwa ni mzinzi kwa kukiuka kwake agizo la Mwenyezi Mungu la kutokuikurubia zinaa, na yeye ameikurubia. Mwenyezi Mungu Anasema: "Wala msiikaribie zinaa kwani hiyo zinaa ni uchafu na ni mwenendo mbaya" (Al-Israa : 32).

Na imepokewa riwaya kutoka kwa Ibnu ‘Abbaas (radhiya Allahu 'anhu) isemay, amesema Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) "Asikae faragha mwanamume na mwanamke ila awe pamoja na mahram" (Al-Bukhaariy Hadiyth Namba 3006 na Muslim Hadiyth Namba 1341).

Na wakati huo huo anahesabika mtu huyo kuwa ni muasi wa amri ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) inayotukataza kukaa faragha na wanawake kando kama tulivyoshuhudia. Kwa maana hiyo fanya haraka kuachana na kitendo hicho na urejee kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya toba.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share