Anaishi Na Kuzini Na Mtu Asiyemuoa Lakini Anaswali, Je, Swalah Zake Zinakubaliwa?

SWALI:

 

Je mtu aliezini akiswali swala yake inakubaliwa? Mfano mtu anaishi na mtu ambaye hajamuoa lakini anajitahidi kusali swala tano je hukumu inakuwaje?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuishi na kuzini na mwanamume. Hakika hili ni swali ambalo halifai kabisa kuulizwa na Muislamu. Hata hivyo, huenda katika kuuliza huku kukaleta faraja na kumtoa mtu katika maasiya ambayo yanampeleka mwanaadamu Motoni.

 

Ifahamike kuwa zinaa ni kitendo cha madhambi na tena ni miongoni mwa madhambi makubwa katika Dini yetu. Hata hivyo, dhambi hilo halikuvui wewe kutoswali na kutekeleza Ibaadah nyingine. Kutofanya Ibaadah hizo kunamaanisha kuwa unachuma madhambi zaidi. Hata hivyo, kufanya kwako zinaa inamaanisha kuwa Swalah yako haitekelezwi inavyotakiwa. Kwani ikiwa itafanyika katika njia ya sawa sawa itakuepusha na machafu na maovu:

 

“Soma uliyofunuliwa katika Kitabu, na usimamishe Swalah. Hakika Swalah inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Allaah ndilo jambo kubwa kabisa. Na Allaah Anayajua mnayoyatenda.” (29: 45).

 

Machafu yanayokusudiwa hapa ni zinaa na uchafu mwengineo. Allaah Aliyetukuka Amewaamuru Waislamu wasithbutu hata kuwa karibu na zinaa kwani ni njia chafu kabisa:

 

“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32). Hivyo, ili Swalah iwe ina athari katika maisha yako inatakiwa uwe mbali na mambo ya madhambi na maasiya yakiwemo zinaa. Ni ajabu mtu atakuwa haoni hasikii mpaka azini ilhali anaweza kuolewa kisheria na mwanamume na akapata starehe hizo anazozipata kwa njia ya madhambi na maasiya.

 

Ikiwa kweli unajitahidi kuswali Swalah tano kwa nini pia hujitahidi katika kuacha zinaa. Kutekeleza Swalah tano huwa unapata thawabu na kuzini unapata madhambi. Kama vile ukiacha kuswali unapata madhambi na ukiacha kuzini unapata thawabu. Ndugu yetu fanya juhudi uwe ni mwenye kuacha zinaa. Hata tukisema ya kwamba utakuwa ni mwenye kupatiwa thawabu kwa Swalah unazoswali, thawabu hizi zitafutwa kabisa na madhambi unayofanya. Ndio Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati mmoja aliwauliza Maswahaba zake:

 

Je, mwamjua muflis?” Wakajibu: “Ni yule asiye na dirham wala dinaar”. Akawaambia: “Ama kwa ummah wangu ni yule atakayekuja Siku ya Qiyaamah na amali ya Swalah, Zakaah, Funga na kadhalika lakini amemtusi huyu, akala mali ya huyu, akampiga huyu. Hivyo, thawabu zake zitachukuliwa na kupewa aliowadhulumu. Na pindi thawabu zake zitakapomalizika, atabandikwa madhambi ya aliowadhulumu” (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewausia Waislamu kwa kuwaambia:

 

Mcheni Allaah popote mlipo, na fuatishaneni baya kwa zuri. Zuri litafuta baya” (at-Tirmidhiy).

 

Na fahamu kuwa hakuna lisilowezekana, ukifanya juhudi kuacha ovu hilo Allaah Aliyetukuka Atakusaidia.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share