Mwanamke Aliyefanya Maasi Ya Zinaa Anaogopa Kuolewa

SWALI:

 

Assalaam aleykum.

Kwanza ningependa kutoa shukurani zangu kwa kuweza kutuelimisha kwenye masuala haya ya dini.

 

suali langu:nini ushauri kwa mwanamke ambaye alifanya zinaa na akajutia na kutorudia tena, na kuzidisha ibada kwa sala, sadaka na kufanya hijja, lakini anaogopa kuolewa (na umri unakwenda) kwa kuhofia kuwa ataonekana hana bikira na labda kuchukiwa na mumewe.

 

Natanguliza shukrani

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuogopa kwa mwanamke aliyefanya uzinzi kuolewa.

Mwanzo tunamuombea kila jema limfikie na kumuombea apate Maghrifah ya kutoka kwa Mola wetu Mlezi. Ikiwa ni kama mlivyosema kuhusu huyo mwanamke basi tunatarajia kuwa atakuwa mahali pema na pazuri Peponi. Hii ni kwa kauli ya Aliyetukuka:

Na wale wasiomuomba mungu mwingine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini; na atakayefanya hayo atapata madhara. Na atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaamah na atakaa humo kwa kufedheheka milele. Ila yule atakayetubia na kuamini na kufanya vitendo vizuri; basi hao ndio Allaah Atawabadilishia maovu yao kuwa mema; na Allaah ni Mwingi wa kusamehe na Mwingi wa kurehemu. Na aliyetubia na kufanya mema, basi kwa hakika yeye anatubu kweli kweli kwa Allaah. … Hao ndio watakaolipwa ghorofa za Peponi kwa kuwa walisubiri na watakuta humo heshima na amani. Wakae humo milele: kituo kizuri na mahali pazuri pa kukaa” (Al-Furqaan: 68 – 76).

 

Ama kwake yeye kukataa kuolewa kwa ajili siri hiyo isije ikafichuka yuko katika usawa na kwa kufanya hivyo Allaah Aliyetukuka Atamfichia Siku ya Qiyaamah pia mbele ya umati wa watu. Njia bora ya yeye kuweza kuingia katika unyumba ni kutokea Muislamu ambaye hatofichua siri hiyo lakini amsitiri katika hali hiyo aliyokuwa nayo huyo dada. Na atakayefanya hivyo basi atakuwa na fungu kubwa mbele ya Muumba wake.

 

Ikiwa hakutapatikana mwenye kujitokeza kumuoa, hakuna ubaya kwake kukaa bila kuolewa maadam hatoshawishika kuingia kwenye uzinifu. Azidishe ibada sana na funga za Sunnah na Allaah Atamuhifadhi inshaAllaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share