Nimekwenda Nje Ya Ndoa, Nimjulishe Mume Wangu?
SWALI:
Kwaza kabisa ningependa kumskuru mwenyeezi mungu kwa kuwajaalia kufungua website hii. Kwani ni moja ya misaada kwa waislam waliopotea kuwakumbusha kurudi kwa mola wao. Mimi msichana ambae nimeolewa kwa muda wa miaka kumi ilio pita. Baada ya kuolewa nikaja urope na mume wangu. baada ya kipindi mume wangu aka badilika akawa hanijali yuko bize na shughuli zake za kibiashara. Hata kwa tendo la ndoa akawa hanijali mpaka kunakipindi ikawa ina fikia mwezi mzima hatukutani.Kitendo hicho kiliniumiza na ibilisi akaningia nikajikuta nimeenda nje ya ndoa. Kitendo ambacho nakijutia mpaka hivi sasa baada ya kutubu kwa mola wangu. Je mwenyeezi mungu atanisamehe mtu kamam mimi? Natatizo jengine kubwa zaidi ni Kwamba baada ya kwenda nje ya ndoa nilipata uja uzito nikaogopa zambi ya kutoa mimba ni kama ya kuua, Na mume wangu hajui kitu hicho. Kitu hichi kinaniuma sana na haswa baada ya kurudi kwa mola wa wangu na kutubu nakujaribu kumpa mume wangu mawaidha ili atulie tujenge ndoa yetu japokuwa ilichukua muda lakini mweyeezi mungu muweza alinijaalia na kusikia dua yangu na mume wangu tunasikilizana. Najitahidi kumuomba mwenyezi anipe uamuzi uliomwema kwani maisha yangu yote sijawahi kudanganya na wala kufanya kitu kibaya kama hichi. Mpaka sasa ninachofikiria ni kumuambia mume wangu ukweli lakini naogopa kuharibu ndoa yetu kwani nampenda mume wangu nanina penda kuishi nae. Na sipendi kitendo cha kuswali na kumuomba mwenyezi mungu anisamehe huku bado kuna uongo ndani yake. Kwani kutubu na kuendelea kumuaaswi mweyezi mungu kwa kuficha ukweli si kutubu, Naninamuomba mwenyezi mungu kila wakati azisikilize dua zangu japokuwa nimerejea kwa muumba wangu lakini bado sina raha kwani sijui mwenyezi mungu ananiangalia kwa jicho gani mtu kama mimi na sijui kama mwenyezi mungu anaweza kumsamehe mtu kama huyo. Ndugu zanguni naomba msaada au ushauri bora kutoka kwenu kupata jibu la swali la mitihani migumu iliyo nikabili. Namuomba Allaah aweze kujaalia kupata jibu au ushauri mzuri kutoka kwenu ndugu zangu waislam. Shukran na Mwenyezi mungu atawazidishia.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Tunashukuru dada yetu kwa swali lako zito na linalosikitisha.
Wamesema Wanachuoni: “Toba (tawbah) ni wajibu kwa kila dhambi. Ikiwa dhambi alilolifanya mja ni baina mja na Allaah aliyetukuka haliingiliani na haki ya binadamu, litakuwa na sharti tatu:
Ya kwanza: Kuacha maasiya.
Ya pili: Kujuta kwa kufanya hayo maasiya.
Ya tatu: Kuazimia kutorudia tena kosa lile milele. Likikosekana sharti moja katika hizi tatu basi toba haitosihi”.
Na ikiwa dhambi lililofanywa lina mafunagamano na mwanadamu sharti za kupata toba zinakuwa ni nne: “Sharti hizi tatu zilizotajwa hapa juu na ya nne ni kuirudishia haki ya yule mtu, ikiwa ni mali au kitu chengine chochote umrudishie. Ni wajibu kwa Muislamu kutubu (kuomba msamaha) kwa madhambi yote. Ikiwa atatubia baadhi ya dhambi husihi toba yake kwa dhambi ile na zinabaki zile zilizobakia. Zimedhihiri dalili katika Kitabu na Sunnah na Ijmaa’ ya Ummah katika uwajibu wa toba.
Ni hakika isiyopingika kuwa Uislamu umeacha wazi mlango wa toba kwa dhambi lililofanywa ikiwa aliyefanya ataweza kutekeleza masharti ya kusamehewa. Hakuna dhambi ambayo haisamehewi na Allaah Aliyetukuka, kwani Anasema:
“Sema: Enyi waja Wangu waliojidhulumu nafsi zao, msikate tamaa na rahmah ya Allaah. Hakika Allaah Husameheme dhambi zote” [39: 53].
Linalotakiwa ni kama alivyosema Allaah Aliyetukuka:
“Na tubuni nyote kwa Allaah, enyi Waumini, ili mpate kufanikiwa” [24: 31].
Mafanikio yetu hapa duniani na kesho Aakhirah ni kufanya hilo alilosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala), kurudi na kutubia Kwake.
Ili toba kukubaliwa tunatakiwa tuwe wakweli na wenye ikhlaasw na niyyah safi katika hilo. Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema:
“Enyi mlioamini! Tubuni kwa Allaah tawbah iliyo ya kweli” [66: 8]
Muislamu anapotubia kweli kweli basi natija yake ni kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):
“Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Allaah, wala hawaui nafsi Aliyoiharimisha Allaah isipokuwa kwa haki, wala hawazini - na atakayefanya hayo atapata madhara, Atazidishiwa adhabu Siku ya Qiyaamah, na atadumu humo kwa kufedheheka. Isipokuwa atakayetubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Allaah Atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Allaah ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Allaah” [25: 68 – 71].
Katika haya yote dada yetu uko sawa kabisa kwani kulingana na maelezo yako ni kwamba umeacha maasiya hayo ya zinaa, umejuta kwa kufanya zinaa na umeazimia kutorudia tena kosa hilo.
Ama huyo mtoto, hatohusishwa na huyo mwanamme aliyezini na we, bali mtoto atahesabika kuwa ni mtoto wa mume wako japo umezaa nje ya ndoa. Na dalili ni kauli yake Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema:
“Mtoto atahusishwa na mume (mwenye kitanda cha ndoa) na mzinifu hastahiki chochote.” [Al-Bukhaariy na Muslim]
Hivyo, mumeo ndiye mwenye kuhusishwa na huyo mtoto na hilo halitofutika hadi mume amkatae huyo mtoto kuwa si wake kishariy’ah kwa njia ya Li’aan (taratibu za kishariy’ah za mtu kumkana mtoto kuwa si wake). Hilo ni kwa sababu misingi ya asli ya kishariy’ah, mtoto anahesabika ni wa yule mwenye kitanda (akikusudiwa mume halali wa mke wa ndoa) kama ilivyotangulia Hadiyth hapo juu.
Wanachuoni wa Baraza La Kudumu La Utoaji Fatwa Na Tafiti Za Kielimu waliulizwa:
“Kuna mwanamke aliyeolewa ambaye amefanya zinaa hali ya kuwa yuko kwenye ndoa (kaolewa). Akapata mimba na akazaa mtoto. Je, mtoto huyo ataishi na nani? Je, ataishi na mume kama inavyoeleza Hadiyth ((Mtoto ni wa (mwenye) kitanda (mume) na mzinifu hapati chochote)) au sivyo? Na ikiwa ataishi na mume wa mama yake, je (huyo mume) atamfanya kama mtoto wa kupanga na kumfanya ni kama mtoto wake pamoja na kupata haki zote anazostahiki, au atakuwa chini tu ya uangalizi wake? Na ikiwa (mtoto) atahusishwa kuwa ni wa mzinifu, je, (huyo mzinifu aliyezaa na mwanamke aliyeko kwenye ndoa) atakuwa na haki za kumfanya huyo mtoto kuwa wake halisi, au ataishi naye tu kama mtoto asiye halali?”
Wakajibu (Kamati ya Kudumu Ya Utoaji Fatwa):
“Ikiwa mwanamke huyo aliyeolewa, kafanya zinaa na akapata mimba kisha akazaa, basi huyo mtoto atakuwa ni wa (mwenye) kitanda (mume), kwa mujibu wa Hadiyth sahihi. Na ikiwa mwenye kitanda ataamua kukataa kuwa mtoto si wake kwa kufanya Li’aan, basi anaweza kufanya hivyo kwa Qaadhwi, na akishafanya hivyo, basi mtoto atakuwa si wa yeyote yule kwa mujibu wa makubaliano ya Wanachuoni wa Kiislamu ‘Ijmaa’’.
Lakini mtu akitaka kumfanya huyo mtoto kuwa ni wa kupanga, hilo halitohalalisha mtoto kuwa wake kihalali.
Na Allaah ni Mwenye Kuleta Tawfiyq.
[Fataawaa Al-Lajnah Ad-Daaimah, mj. 20, uk. 339]
Na Allaah Anajua zaidi