Ibadhi Au Uibadhi Tofauti Za Itikadi Zao Na Za Sunni
Ibadhi Au Uibadhi Tofauti Za Itikadi Zao Na Za Sunni
Maelezo kuhusu tofauti zilizopo kati ya Uibadhi na Ahlus-Sunnah ni tofauti ambazo mtu anapaswa kusoma kwenye vitabu vya pande hizo, kwani kuna mengi ya kujua na kujifunza na hutoweza kuyajua yote kwa kujibiwa katika swali moja.
Ibadhi na Shia wamefanana sana katika itikadi zao. Ushia kama ulivyouona au kuusoma kwenye makala mbalimbali zilizomo kwenye ALHIDAAYA, ni kundi ambalo limekwenda mbali kabisa na njia ya haki na lina itikadi za kikafiri zenye kuwatowa kwenye Uislamu.
Kuhusu tofauti za Uibadhi na Ahlus-Sunnah, tunakuwekea hapa tofauti zao kwa mukhtasari kama visemavyo vitabu vyao.
Wa Allaahu A'lam
Orodha Ya Baadhi Ya Tafauti Kati Ya Itikadi Za Kiibadhi Na Za Kisunni
1. Ghayb
Mafundisho ya Uibadhi
Maibadhi hufuata utaratibu wa kuzifanyia ta-awiyl aya zote za Qur-aan zinazozungumzia sifa za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).
Mafundisho ya Usunni
Sunni wanasema ni lazima kwa Muislamu kuamini yote yaliyotajwa katika Qur-aan na Hadiyth za Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu ghaibu. Masunni huamini kwamba kukataa jambo lililothibitishwa na Allaah au kubadilisha maana yake ni kuzungumza kuhusu Allaah bila elimu, na hii ni katika madhambi makubwa.
2. Kumuamini Allaah, Allaah Yuko Wapi?
Mafundisho ya Uibadhi
Imani kwamba Allaah ‘Yuko juu ya ‘Arshi Yake’ isichukuliwe kwa maana yake halisi bali maana yake ya kweli ni utawala wake juu ya ulimwengu mzima. ‘Hakuna sehemu mbinguni na ardhini iliyoachwa bila ya uangalizi wake… Amekaa juu ya ‘arshi yake, anashuhudia kila kitu na amezingira kila kitu bila muundo, mpaka, shabihi, ta’awiyl au dhana.’ (Rabi’i bin Habiyb)
Mafundisho ya Usunni
Imani kwamba Allaah yuko juu ya viumbe vyake kwa dhati na sifa zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ ۖ ﴿٣﴾
‘Ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha Akawa juu (Istawaa)[1] ya ‘Arsh. Anaendesha mambo yote.’ [Yuwnus :3] Kukaa kwake ‘juu ya ‘Arshi Yake’ ina maana kwamba Amekaa juu ya ‘Arshi Yake kwa dhati Yake kwa namna ambayo inalingana na ukubwa na utukufu Wake. Hakuna zaidi Yake Yeye mwenyewe Anayejua kikamilifu Amekaaje.
3. Wasifu Wa Allaah
Mafundisho ya Uibadhi
Itikadi ya Uibadhi kwa kawaida ni kuondosha sifa zote zinazopelekea kumfananisha Allaah na viumbe Vyake katika sifa Zake na aya na Hadiyth za Nabiy zenye sifa hizo zinatakiwa kufanyiwa ta’awiyl kulingana na hali yenyewe ili kusiwe na tashbihi yoyote. Hakuna kiumbe chochote kinachofanana Naye na Yeye hafanani na kiumbe chochote; chochote kilichokuja katika Qur-aan na Hadiyth za Rasuli wa Allaah kinachopelekea kumfananisha Yeye na kiumbe chochote katika sifa yoyote inafanyiwa ta’awiyl ili kuondosha tashbihi yoyote.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini sifa zote Allaah Alizojisifia nazo na kukataa sifa zote Alizokataa na vilevile sifa ambazo Rasuli Wake kamsifu nazo zikiwemo sifa za majina na dhati. Wanaamini kwamba Yeye kajisifu na kauli hiyo, na kwamba Yeye Anajijua vizuri zaidi, na wanakwepa majadiliano kuhusu sifa ambazo Allaah na Rasuli Wake hawakuzitaja. Wanaamini kwamba ni lazima kuamini Aayah na Hadiyth zinazotaja sifa za Allaah kijuujuu bila kuangalia kwa undani, na wanakataa tabia ya wale wanaoghairi maana za nusuus hizo (maandiko hayo) au kuyapa maana isiyokusudiwa na Allaah na Rasuli Wake. Vilevile wanakataa msimamo wa wale wanaotafsiri Aayah na Hadiyth hizo tafsiri inayopelekea kumfananisha Allaah na viumbe Vyake.
ۚ لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ﴿١١﴾
‘Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.’ [Ash-Shuwraa :11]
Wanaamini yaliyoteremshwa na Allaah katika Qur-aan bila kubadilisha au kukataa na wala kuuliza vipi? (takyiif) au kufananisha (tamthiyl).
4. Mikono Na Uso Wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)
Mafundisho ya Uibadhi
Wanaamini kuwa ‘uso’ wa Allaah una maana ya dhati Yake. ‘Mikono’ Yake ni nguvu na utawala Wake
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini Allaah Ana uso mtukufu.
وَيَبْقَىٰ وَجْهُ رَبِّكَ ذُو الْجَلَالِ وَالْإِكْرَامِ ﴿٢٧﴾
‘Na utabakia Wajihi wa Rabb wako Mwenye Ujalali na Taadhima.’ [Ar-Rahmaan:27]
Allaah Ana mikono miwili Karimu:
بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ ۚ ..﴿٦٤﴾
‘Bali Mikono Yake (Allaah) imefumbuliwa Hutoa Atakavyo.’ [Al-Maaidah:64]
وَمَا قَدَرُوا اللَّـهَ حَقَّ قَدْرِهِ وَالْأَرْضُ جَمِيعًا قَبْضَتُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَالسَّمَاوَاتُ مَطْوِيَّاتٌ بِيَمِينِهِ ۚ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ﴿٦٧﴾
‘Na hawakumkadiria Allaah kama inavyostahiki kumkadiria; na hali ardhi yote itatekwa Mkononi Mwake Siku ya Qiyaamah; na mbingu zitakunjwa Mkononi Mwake wa kulia. Subhaanahu wa Ta’aalaa (Utakasifu ni wa Allaah na Ametukuka kwa ‘Uluwa) kutokana na yale yote wanayomshirikisha..’
[Az-Zumar:67]
5. Macho Ya Allaah
Mafundisho ya Uibadhi
‘Jicho’ Lake lina maana ya elimu na hifadhi Yake.
وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۚ ..﴿٣٧﴾
‘Na unda jahazi mbele ya macho Yetu na ufunuzi wa Wahy Wetu,..’ [Huwd:37]
وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِّنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي ﴿٣٩﴾
‘...Na Nikakutilia mahaba kutoka Kwangu, na ili ulelewe Machoni Mwangu..’ [Twahaa:39]
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini Allaah Ana macho mawili ya kweli. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema,
‘Hijabu (kizuizi kati yake na viumbe Vyake) ni nuru. Akiiondoa (kizuizi hicho) utukufu wake ungeunguza kila kitu kinachoonekana na macho Yake.’ [Muslim na Ibn Maajah]
Masunni wote wamekubaliana kuwa ana macho mawili. Hii inatiliwa nguvu na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu Dajjaal kwamba,
‘...yeye ana jicho moja, Mola wenu hana jicho moja.’ (Al-Bukhaariy na Muslim)
6. Kumuona Allaah
Mafundisho ya Uibadhi
Maibadhi wanaamini Allaah Haonekani hapa duniani wala hatoonekana kesho Akhera. Kuhusu Aayah inayosema Allaah Ataonekana basi ‘kuona’ katika hiyo Aayah imepewa tafsiri ya kusubiri rukhsa kutoka kwa Mola kuingia peponi. Suala hili limejadiliwa kikamilifu katika Musnad ya Rabi’i bin Habiyb.
Mafundisho ya Usunni
Masunni wanaamini kwamba Waumini watamuona Allaah kesho Akhera.
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَّاضِرَةٌ﴿٢٢﴾إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ﴿٢٣﴾
‘Nyuso siku hiyo zitanawiri. Zikimtazama Rabb wake.’ [Al-Qiyaama:22-23]
Na kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam),
‘Mtamuona Mola wenu kama mnavyouona mwezi mpevu. Na hakuna kitu kitakachowazuia kumuona siku hiyo; kwa hiyo kama mnaweza kusimamisha Swalah ya Al-Fajiri na Adhuhuri basi fanyeni.’ [Al-Bukhaariy na Muslim]
7. Imani Kuhusu Qur-aan
Mafundisho ya Uibadhi
Maibadhi wanaamini Qur-aan ni neno la Allaah aliloliumba na iliyoteremshwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kidogo kidogo. Si sifa miongoni mwa sifa za Allaah za dhati au za vitendo.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini Qur-aan ni neno la Allaah lililoteremshwa kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na haijaumbwa. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Aliizungumza kumuambia Jibriyl ambaye aliishusha kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
8. Makhalifa Wa Nne Waliongoka
Mafundisho ya Uibadhi
Maibadhi wanawatambua Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) kama Makhalifa walioongoka na pia ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) katika miaka sita ya kwanza ya Ukhalifah wake. Maibadhi walichukulia harakati zao kuwa ni mwendelezo wa upinzani uliomuondoa ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) madarakani na kusababisha kifo chake, upinzani wao ulikuwa ni wa Kiislam dhidi ya mambo ya uzushi aliyozua. Maibadhi waliukubali Ukhalifah wa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu), lakini baadaye hawakuridhika wakati ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipokubali hukmu ya mahakimu wawili katika vita vyake na Mu’awiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na waliwahesabu wale waliokataa hukmu hiyo ndiyo Waislam wa kweli.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini kwamba katika Maswahaba, bora wao na aliyestahiki kuwa Khalifah baada ya Rasuli wa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha ‘Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu), kisha ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu). Kwa hiyo Ukhalifah wao ulilingana na ubora wao.
9. Maswahaba
Mafundisho ya Uibadhi
Kuhusu Swahaba, Maibadhi wamewafanyia Jarh (kuwakosoa). Swahaba wote ni waadilifu ila wale waliotajwa na Qur-aan kwamba ni waasi. Riwaya zao zinakubalika ila wale waliofanya maasi. Lengo la Maibadhi ni kufuata mfano mwema wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), Makhalifa wake wawili (Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) na Swahaba wengine waadilifu, na kujenga jamii ya Kiislam kwa misingi ileile ya jamii ya Kiislam ya kwanza. Al Saalimy, mwanachuoni wa Kiibadhi ameandika katika kitabu chake ‘Twala’at ash-Shams’, ‘Ama kuhusu Swahaba, yeye ni muadilifu hadi hapo atakapofanya maasi. Kwa hiyo, kama walivyo watu wengine, watahukumiwa.’
Kwa hiyo Ibadhi hawamkubali kikamilifu na wanawasema vibaya Swahaba kama 'Aliy wala 'Uthmaan wala Mu'aawiyyah wala Az-Zubayr wala Twalhah wala 'Amru bin Al-Aasw, Abuu Muwsaa Al-Ash'ariy na wengineo (Radhwiya Allaahu 'anhum).
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini kuwa ikhtilafu na vita zilizotokea miongoni mwa Maswahaba yalikuwa ni matokeo ya ijtihadi zao walizofanya kwa nia nzuri. Yeyote aliyekuwa juu ya haki miongoni mwao atapata ujira wake mara mbili, na aliyekosea atapata ujira mmoja na makosa yake yatasamehewa. Wanaamini kwamba inawapasa Waislam kuacha kuzungumzia makosa yao na badala ya kufanya hivyo wanatakiwa kutaja fadhila zao, na kutakasa nyoyo zao na chuki yoyote dhidi yao (Swahaba), kwani Allaah Amesema kuhusu wao:
ۚ لَا يَسْتَوِي مِنكُم مَّنْ أَنفَقَ مِن قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ ۚ أُولَـٰئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِّنَ الَّذِينَ أَنفَقُوا مِن بَعْدُ وَقَاتَلُوا ۚ وَكُلًّا وَعَدَ اللَّـهُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١٠﴾
‘Hawi sawa miongoni mwenu aliyetoa kabla ya Ushindi (wa Makkah) na akapigana. Hao watapata daraja kuu kabisa kuliko wale waliotoa baadae na wakapigana. Na wote Allaah Amewaahidi malipo mazuri kabisa. Na Allaah kwa yale myatendayo ni Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.’ [Al-Hadiyd:10]
Wanaamini kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
‘Msiwatukane Swahaba wangu. Naapa kwa Allaah ambaye nafsi yangu iko mikononi Mwake! Kama mmoja wenu atatoa dhahabu mfano wa mlima Uhud hawezi kufikia kibaba cha mmoja wao au nusu yake.’ [Al-Al-Bukhaariy, Muslim, Abu-Dawuud, at-Tirmidhiy Ibn Majah, Ibn Hanbal]
‘...Wao ni kizazi bora.’ [Al-Bukhaariy na Muslim]
na,
‘...kibaba cha sadaka cha mmoja wao ni bora kuliko dhahabu mfano wa mlima Uhud unaotolewa na yeyote anayekuja baada yao.’ [Al-Bukhaariy na Muslim]
10. Mizani
Mafundisho ya Uibadhi
Wanaamini mizani si kitu kinachotambulika kwa hisia tano za binadamu bali ni kipimo adilifu cha vitendo vya viumbe.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini mizani itasimamishwa siku ya Qiyaama, na hakuna nafsi itakayodhulumiwa:
فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٠٢﴾وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾
‘ Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni ambao wamekhasirika nafsi zao; katika Jahannam ni wenye kudumu.’ [Al-Muuminuw:102-103]
11. Swiraat (Daraja)
Mafundisho ya Uibadhi
Wanaamini kwamba Swiraat siyo daraja itakayowekwa juu ya Jahannam siku ya Qiyaama, bali ni Uislam na dini ya Allaah Aliyowaridhia waja Wake. Ameitaja kuwa na ncha kali kuliko upanga na sahihi kuliko nywele. Maana yake ni ugumu wa kufuata Uislam na njia yake iliyonyooka kwani kuna vishawishi vingi vinavyotukabili katika hii dunia.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini Swiraat ni daraja itakayowekwa juu ya Jahannam siku ya Qiyaama. Watu watapita juu yake kulingana na amali zao: wa kwanza kwa kasi kama ya radi, wa pili kwa kasi ya upepo, halafu wengine kwa kasi ya ndege na wengine kwa kasi ya mtu anayekimbia. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa amesimama juu ya hiyo Swiraat akisema,
‘Yaa Rabb wangu! Waokoe! Waokoe!’
wakati amali za watu wengine zitakapokuwa pungufu. Wengine wataipita hiyo daraja wakitambaa. Pande zote mbili za hiyo daraja kuna kulabu zinazowavuta anaowataka Allaah: wengine wanaokoka (wakati wakivutwa na kulabu hizo) lakini wanajeruhiwa; wengine wanatupwa Motoni. [Al-Bukhaariy na Muslim]
12. Shafaa’ah Ya Rasuli wa Allaah (swalla Allaahu ‘alayhi Wa Aalihi Wa Sallam).
Mafundisho ya Uibadhi
Shafaa’ah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) imethibiti, na kuna aina mbili: Shafaa’ah kubwa Siku ya Qiyaama ya kuwaombea Waumini kuingia Peponi, na hii ni makamu (na cheo) aliyotengewa Rasuli wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) peke yake. Shafaa’ah ya pili ni Shafaa’ah ndogo kwa ajili ya Waumini wenye daraja za ziada tu. Shafaa’ah siyo kwa wenye maasi ambao hawakutubu kabla ya kufa.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini Shafaa’ah makhsusi ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Siku ya Qiyaama. Atawaombea, baada ya kuruhusiwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa), baadhi ya Waumini ambao watakuwa wakipelekwa Motoni. Shafaa’ah hii amepewa Rasuli wa Allaah(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Rusuli wengine, Waumini na Malaika.
13. Madhambi Makubwa
Mafundisho ya Uibadhi
Tawbah ndiyo msingi wa Msamaha. Allaah Hasamehi madhambi makubwa ila kama mtu atatubu kabla ya kufa. Ama madhambi madogo, hayo yanasamehewa kwa kukwepa kutenda madhambi makubwa, na kwa kutenda mambo mema. (Matendo mema hufuta matendo mabaya) Atakayekuwa na furaha Akhera hatokuwa na huzuni, na atakayekuwa na huzuni hatakuwa na furaha; furaha na huzuni hazitajumuika katika mtu mmoja. Kuhusu madhambi makubwa, Wao wanasema mtu huyo ni Mnafiki au Kafiri wa neema, na ni muhali kwake yeye katika hali hiyo ya kuyatenda madhambi hayo makubwa na kuendelea na hali hiyo, kuingia Peponi kama hatotubu. Wengine wanafasiri madhambi makubwa kuwa ni yale yaliyokatazwa katika Qur-aan na madhambi madogo ni yale yaliyokatazwa katika Sunnah.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini kwamba Allaah Atawaokoa baadhi ya Waumini kuingia Motoni bila ya Shafaa’ah ya yeyote yule kwa rehema na ukarimu Wake. Wale wafuasi wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) waliyotenda madhambi makubwa wataingia motoni, lakini si milele ikiwa watakutana na Mola wao wakimpwekesha bila kumshirikisha na yeyote hata kama hawakutubu na madhambi hayo (makubwa). Wao wako chini ya ridhaa na matakwa Yake. Akitaka, Atawasamehe kutokana na ukarimu Wake, kama ilivyotajwa katika Qur-aan:
إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ .. ﴿١١٦﴾
‘Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae..’ [An-Nisaa 4: 116]
na akitaka Atawaadhibu Motoni kwa uadilifu Wake na kisha kuwatoa hapo kwa rehema Zake, au kwa Shafaa’ah ya wale waliokuwa watiifu kwake, na kuwapeleka Peponi. Hii ni kwa sababu Allaah ni Mhifadhi wa Waumini na Hatawatendea Akhera Atakavyowatendea wale waliomkataa na wasiokuwa na mwongozo Wake na walioshindwa kupata hifadhi Yake. Masunni hawasemi kuhusu mtu yeyote kama ataenda Motoni au Peponi na wala hawamtuhumu yeyote kuwa ni Kafiri au Mshirikina au Mnafiki ila kama mtu huyo atayatenda matendo hayo waziwazi au atajitangaza kuwa katika vikundi hivyo.
14. Adhabu Ya Kaburi
Mafundisho ya Uibadhi
Wanathibitisha adhabu ya kaburi na maswali ya Malaika wawili kama ilivyothibiti katika Hadiyth nyingi sahihi.
Mafundisho ya Usunni
Wanaamini maswali/adhabu ya kaburi, zinazohusu maiti kuulizwa kuhusu Rabb wake, dini yake na Rasuli wake. Wanaamini kwamba Waumini watastarehe kaburini na makafiri wataadhibiwa.
15. Kupigana (Qitaal)
Mafundisho ya Uibadhi
Wanaamini kuwa si halali kupigana dhidi ya kiongozi muadilifu. Kupigana dhidi ya kiongozi asiyekuwa muadilifu si wajibu; na wala haikatazwi. Kiongozi dhalimu ataombwa kwanza kuwa muadilifu, akikataa ataombwa kujiuzulu; akikataa basi inaruhusiwa kupigana nae na kumuondoa kwa nguvu hata kama kufanya hivyo kutasababisha kifo chake. Lakini inapendelewa kutokupigana na kiongozi dhalimu na kubaki chini ya utawala wake kama inahofiwa kuwa kupigana naye hakutofanikiwa au kutawaathiri Waislam na kuwadhoofisha dhidi ya Maadui zao katika nchi yoyote ya Kiislam.
Mafundisho ya Usunni
Masunni hawatambui uasi dhidi ya Imaam au viongozi hata kama wao si waadilifu, na wala hawakatai kuwafuata. Wanaamini kwamba kuwatii ni sehemu ya kumtii Allaah, na kwa hivyo ni wajibu ili muradi wasiwaamuru kutenda madhambi. Wanawaombea du’aa waongoke na msamaha kwa madhambi yao. Kuhusu kiongozi anayekufuru waziwazi, msingi mkubwa wa Masunni ni kwamba hairuhusiwi kuondoa shari kwa shari kubwa zaidi. Kama Waislam wataweza kumuondoa huyu kiongozi kafiri na kumuweka kiongozi muadilifu bila kusababisha shari kubwa kuliko shari ya huyo kiongozi kafiri basi itaruhusiwa. Lakini kama itasababisha shari kubwa zaidi na vurugu na damu ya watu wasio na hatia kumwagwa basi haitaruhusiwa.
16. Hadiyth
Mafundisho ya Uibadhi
Musnad Ar-Rabi’i bin Habiyb (SAHIH), imeandikwa karne ya pili Hijriyah, na ni kitabu cha rejea kinachotegemewa na Maibadhi katika Hadityh, na ina daraja ya juu kwao kuliko Al-Bukhaariy na Muslim.
Mafundisho ya Usunni
Al-Bukhaariy na Muslim ndiyo vitabu vyenye kutegemewa zaidi kwao kuliko vitabu vingine ingawa Hadiyth sahihi zinapatikana katika vitabu vingine vya Hadiyth pia. Masunni hawahesabu Hadiyth za Ar-Rabi’i bin Habiyb kuwa ni sahihi.
17. Sunnah
Mafundisho ya Uibadhi
Vitendo vya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vya Ibadah alivyotenda kwa ajili ya kufundisha au aliyatenda mara moja tu kisha hakuyarudia tena, au yale ambayo haikuthibiti kwamba aliendelea navyo, si Sunnah kwa Maibadhi; bali wao huyachukulia ni matukio yaliyotokea kwa sababu maalum katika hali maalum. Katika kumfuata Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawayachukulii vitendo vifuatavyo kuwa ni Sunnah: Qunuut katika Swalah, kutikisa kidole katika Tashahhud, kusema ‘Amiyn’ baada ya kusoma Suratul-Faatiha katika Swalah, kuongeza "As-Swalaat Khayrun minan Nawm" katika adhana ya Swalah ya Al-Fajiri.
Mafundisho ya Usunni
Allaah Anasema:
لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ ..﴿٢١﴾
‘Kwa yakini mna kigezo kizuri kwa Rasuli wa Allaah …’ [33:21]
Masunni wanaamini ni wajibu kufuata yote yaliyonasibishwa na kuthibiti kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumwa tu kuleta Qur-aan bali hata kuitafsiri, kuielezea na kufafanua namna ya kuifuata. Dalili yenye nguvu kuhusu kufuata mfano wake ni:
وَمَا آتَاكُمُ الرَّسُولُ فَخُذُوهُ وَمَا نَهَاكُمْ عَنْهُ فَانتَهُوا ۚ ..﴿٧﴾
‘...Na lolote analokupeni Rasuli(صلى الله عليه وآله وسلم )basi lichukueni, na analokukatazeni, basi acheni.….’ [Al-Hashr:7]
18. Hijrah
Mafundisho ya Uibadhi
Hakuna Hijrah baada ya Fat-hu Makkah (kufunguliwa Makkah) na hairuhusiwi kukimbia nchi ya adui kwenda nchi ya makafiri kwa kuchukulia (kufanya hivyo) ni Hijrah.
Mafundisho ya Usunni
Maana ya Hijrah ni kuhama kutoka katika nchi ya makafiri kwenda katika nchi ya Waislam au kuhama kutoka nchi moja ya makafiri kwenda nchi nyingine ya makafiri ambapo kuna shari kidogo na hatari kidogo kwa Waislam, kwa ajili ya Dini yako. Hijrah, kwa maana hii ni wajibu juu ya Waislam mpaka Siku ya Qiyaama. Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kwamba:
“...nanajiweka mbali na Muislam anayeishi miongoni mwa makafiri.”
Kama Muislam anaweza kuhama kutoka katika nchi za makafiri basi Allaah Anamkataza kuendelea kukaa hapo. Anaweza kukaa kama atalingania watu katika Uislam na kufanya Da’wah, na kuonyesha dini yake waziwazi bila kuficha. Allaah Anasema:
إِنَّ الَّذِينَ تَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ قَالُوا فِيمَ كُنتُمْ ۖ قَالُوا كُنَّا مُسْتَضْعَفِينَ فِي الْأَرْضِ ۚ قَالُوا أَلَمْ تَكُنْ أَرْضُ اللَّـهِ وَاسِعَةً فَتُهَاجِرُوا فِيهَا ۚ فَأُولَـٰئِكَ مَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿٩٧﴾
‘Wale ambao Malaika wamewafisha, hali wamedhulumu nafsi zao, (kwa kutohajiri; Malaika) watawaambia: ‘Mlikuwa katika hali gani (katika jambo la Dini yenu?)’ Watasema: ‘Tulikuwa madhaifu katika ardhi hiyo (kwa hiyo hatukuweza kufanya ibada yetu).’ (Malaika) watasema: ‘Ardhi ya Allaah haikuwa na wasaa na nyinyi, kuhamia humo?’ Basi hao makazi yao ni Jahannam; nayo ni marejeo mabaya kabisa.’ [An-Nisaa:97]
19. Kufuta Soksi
Mafundisho ya Uibadhi
Wanachuoni wa Kiibadhi wanaamini kwamba Hadiyth ya kufuta soksi ilifutwa na aya ya wudhuu:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا قُمْتُمْ إِلَى الصَّلَاةِ…﴿٦﴾
‘Enyi walioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swalaah; ...’ [Al-Maaidah:6]
Mafundisho ya Usunni
Masunni wanaruhusu kufuta soksi za ngozi (katika wudhuu) safarini au vinginevyo, kama ilivyowaridi katika Hadiyth sahihi.
20. Swalah
Mafundisho ya Uibadhi
1. Maibadhi wanaona kuwa hakuna kunyanyua mikono wakati wa takbira ya kwanza na wakati wowote mwingine katika Swalah.
2. Maibadhi hawafungi mikono katika Swalah, bali huiachia ikining'inia.
3. Maibadhi wanaona kuwa Suratul-Faatiha tu ndiyo inatakiwa kusomwa katika Swalah za Adhuhuri na Alasiri.
3. Maibadhi wanakataa Qunuut na wanaona kuwa Swalah iliyoswaliwa nyuma ya Imaam aliyesoma Qunuut ni batili na inatakiwa kuswaliwa tena.
4. Maibadhi hawasemi ‘Aamiyn’ baada ya kusoma Suratul-Faatiha katika Swalah.
Mafundisho ya Usunni
1. Masunni wanaona kwamba mikono inatakiwa kunyanyuliwa wakati wa kusema takbira ya kwanza na pia katika sehemu zingine za Swalah kama vile kabla na baada ya rukuu.
2. Masunni wanafunga mikono katika Swalah na wanaamini kuwa hiyo ni Sunnah ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama Hadiyth ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilivyosema. Na pia Swahaba wamesimulia katika Hadiyth mbalimbali sahihi kuwa walimuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifunga mikono.
3. Masunni wanaona kwamba Aayah zingine za Qur-aan zinatakiwa kusomwa baada ya Suratul-Faatiha katika rakaa mbili za mwanzo za Swalah za Adhuhuri na Alasiri.
4. Masunni wanakubali uhalali wa kusoma Qunuut (An-Nawaazil [wakati wa matatizo]) katika Swalah. Na pia Qunuut katika Swalah ya Witr.
5. Masunni wanasema ‘Aamiyn’ baada ya kusoma Suratul-Faatiha katika Swalah kwa sababu imethibiti hivyo katika mafundisho kadhaa ya Rasuli (Swalah Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).
21. Swawm
Mafundisho ya Uibadhi
1. Maibadhi wanaona kwamba ni lazima mtu awe katika hali ya Twahara kubwa (yaani asiwe na janaba) wakati wa Swawm kama vile katika Swalah. Kwa hiyo anayefunga lazima awe katika hali hiyo ya Twahara kubwa funga inapoanza.
2. Maibadhi wanaona kwamba madhambi makubwa yanabatilisha Swawm.
3. Maibadhi wanaona kwamba mtu anatakiwa kulipa kwa kuzifunga kwa mfululizo siku za Ramadhaan ambazo hakuweza kufunga.
Mafundisho ya Usunni
1. Masunni wanaona kwamba kufunga wakati wa kuwa na janaba haiathiri Swawm ya mtu, lakini ni lazima kuwa katika hali ya Twahara kubwa kwa ajili ya Swalah. Mwenye kufunga lazima awe katika hali ya Twahara wakati wa Swalah ya Al-Fajir.
2. Masunni wanaona kwamba mtu anaweza kuendelea na Swawm yake hata kama atatenda madhambi.
3. Masunni wanaona kwamba si lazima kulipa kwa kuzifunga kwa mfululizo siku za Ramadhaan ambazo mtu hakuzifunga (alizokosa).
Mafundisho ya Uibadhi
Ibadhi wanafuata itikadi za Khawaarij na wanawapenda na kudai kuwa walikuwa katika haki wakati walipopigana na Khalifa wa Waislamu 'Aliy bin Abiy Twaalib (Radhwiya Allaahu 'anhu) na Ibadhi wanaamini kuwa 'Aliy bin Abiy Twaalib ndiye aliyekuwa katika makosa na alifanya dhulma!
Mafundisho ya Usunni
Ahlus Sunnah wanaamini kuwa Makhawaarij ni kundi potofu na Wanachuoni wa Ahlus Sunnah wametofautiana kuhusu Ukafiri wa Makhawaarij; kuna walioona ni kundi potofu na kuna waliowaona ni Makafiri kutokana na Hadiyth ya Rasuli (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) isemayo:
"Watatoka katika Dini (katika riwaya nyingine, 'watatoka katika Uislamu') kama mshale unavyopenyeza na kutoka kwenye kiwindwa..."
Lifahamu Kundi La Khawaarij