Mashia Ithna ‘Ashariyah (Wenye Kufuata Maimamu Wao Kumi Na Mbili) Na Hadhi Ya Maimamu Wao
Mashia Ithna ‘Ashariyah (Wenye Kufuata Maimamu Wao Kumi Na Mbili) Na Hadhi Ya Maimamu Wao
Hadhi Ya Maimamu Kumi Na Mbili Wa Kishia - Ithna ‘Ashari Shi’ah
Je, wana umuhimu gani Maimamu Kumi na Mbili wa Kishia haswa wa mwishoni?
Kwanza:
Mashia Maraafidhah, Imaamiyah ama Ithna ‘Ashariyah (“Wafuasi wa Imaam Kumi na Mbili”) ni miongoni mwa matawi ya Ushia. Wanaitwa Maraafidhah kwa sababu wamewakataa (rafadha) Swahaba walio wengi na kuukataa utawala wa Swahaba wawili Abu Bakr na ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa), au kwa sababu wamekataa Uimamu wa Zayd bin ‘Aliy (Imaam wa Mashia Zaydiyah), na kumpiga pande. Wanaitwa watu wenye (imani ya) Kiimamu kwa sababu lengo lao kuu ni kwenye suala la Uimamu, na wamelifanya suala hili kuwa ni msingi mkuu wa dini yao, au kwa sababu wanadai kwamba Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba ‘Aliy na kizazi chake ndio watakuwa Maimamu. Wanaitwa Ithnaa ‘Ashariyah (“Kumi na Mbili”) kwa sababu wanaamini Uimamu wa watu kumi na mbili kutoka kwenye ukoo wa Nabiy (Ahlul-Bayt), ambaye wa mwanzo wao alikuwa ni ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na wa mwisho wao alikuwa ni Muhammad bin al-Hasan al-‘Askariy (wanamwita Imamu Mahdi), Imamu mtarajiwa aliyejificha, ambaye wanasema ameingia kwenye ‘Pango la Samurra’ mnamo miaka ya kati kati ya karne ya tatu Hijriyyah na bado yuhai, na wanamsubiria atoke nje! Wana itikadi na misingi ambayo ni kinyume na ile ya Uislamu, kama ifuatayo:
1. Wamevuka mpaka katika (kuwapa sifa) Maimamu wao, wakidai kwamba ni wasio na kasoro, na kwamba wametumia vitendo vyao vingi vya ibada kwa ajili yao kama vile maombi, msaada, kufanya kafara na Twawaaf (kuyazungukia makaburi yao). Hii ni shirki kubwa ambayo Allaah Hatatusamehe. Matendo haya ya shirki yanafanywa na wanazuoni wao na pia mila zao, bila ya mtu yeyote miongoni mwao kuyapinga.
2. Wanasema kwamba Qur-aan Tukufu imeharibiwa, na kwamba kuna vitu ambavyo vimeengezwa na vyengine kupunguzwa. Wana vitabu vyao ambavyo vinatambuliwa na wanazuoni wao na mila zao, wanafikia kusema kuwa imani ya kwamba Qur-aan imeharibiwa; hiyo ni kanuni kuu ya imani zao.
3. Wanaamini kuwa wengi katika Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) ni makafiri, na kuwapinga, na wanajaribu kuwa karibu na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwa kuwalaani na kuwatusi. Wanadai kwamba wamertadi baada ya kifo cha Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) isipokuwa kwa baadhi yao (saba tu). Hili ni kuikana Qur-aan ambayo inakubaliana na sifa zao, na inasema kwamba Allaah Alikuwa radhi nao na Amewachagua kuwa washirika wa Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Pia inamaanisha utovu wa adabu dhidi ya Qur-aan yenyewe, kwa sababu imeshushwa kupitia kwao; iwapo walikuwa ni makafiri basi hakuna ithibati kwamba hawakuiharibu ama kuibadilisha. Hata hivyo, hili ndilo wanaloliamini Maraafidhah, kama ilivyoelezwa hapo juu.
Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) anasema:
“Ama kwa yule ambaye anachupa mpaka na kudai kwamba (Swahaba) wamertadi baada ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kufariki, ingawa ni kwa idadi yao chache, wasiozidi kumi au mfano wake, au kwamba wamekuwa ni watu waovu, hakuna shaka yoyote kwamba huyo ni kafiri, kwa sababu anakataa (yale yanayosemwa) katika sehemu zaidi ya moja ndani ya Qur-aan, kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amekuwa radhi nao na kuwasifu. Hakika, yeyote mwenye shaka kwamba mtu huyo ni kafiri basi yeye mwenyewe aitwe kuwa ni kafiri, kwa sababu wazo kama hili lina maana kwamba wale walioipokea Qur-aan na Sunnah walikuwa ni makafiri ama ni wasio waadilifu wenye matendo maovu. Aayah inasema:
كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ ۗ وَلَوْ آمَنَ أَهْلُ الْكِتَابِ لَكَانَ خَيْرًا لَّهُم ۚ مِّنْهُمُ الْمُؤْمِنُونَ وَأَكْثَرُهُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿١١٠﴾
Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa (mfano) kwa watu; mnaamrisha mema na mnakataza munkari na mnamwamini Allaah. Na lau wangeliamini Ahlul-Kitaabi ingelikuwa ni bora kwao, miongoni mwao wanaoamini na wengi wao ni mafasiki. [Al-‘Imraan:110]
na wabora wao walikuwa ni kizazi cha mwanzo. Lakini kwa mujibu wa fikra hii, wengi katika hao walikuwa ni makafiri na wasio waadilifu wenye matendo maovu, na ummah huu ni mbaya katika mataifa na kizazi cha mwanzo cha ummah huu kilikuwa ni kiovu katika ummah huu. Ukweli kwamba hii ni kufru na ni jambo ambalo hakuna Muislamu aliye uwa na udhuru wa kutolielewa.”
Mwisho wa nukuu kutoka as-Swaarim al-Masluul ‘ala Shaatimir-Rasuul, uk. 590.
4. Wanaruhusu kufanya badaa’ kwa Allaah, yaani kutengeneza fikra mpya ambayo haikuwepo hapo kabla. Hii ina maana ya kumpa Allaah Aliye Mtukufu (pasi na kasoro yoyote) sifa ya ujahili.
5. Wanaamini kuhusu Taqiyah (unafiki) wenye maana kuonesha nje kitu tofauti na vile hisia zake zilivyo ndani. Ukweli kwamba tabia hii ni uongo na unafiki na njia ya kuwadanganya watu. Jambo hili sio kwamba linafanyika kipindi cha mtu kuwa na hofu; bali wanaamini matumizi ya Taqiyah kama ni wajibu wa kidini kwenye masuala makuu na madogo, kwenye vipindi vya hofu na salama. Ukweli wowote ambao umeelezwa kutoka kwa Maimamu wao, kama vile sifa kwa Swahaba wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), au kukubaliana na Ahlus-Sunnaah, hata kwenye masuala ya kujitakasa au chakula na kinywaji, yanakataliwa na Shi’ah wanaosema kwamba Imamu hakusema hayo isipokuwa kwa njia ya taqiyah.
Imani kuhusu raja’ah: Ni imani ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na watu wake wa nyumbani (Ahlul-Bayt), ‘Aliy, al-Hasan, al-Husayn na Maimamu wengine watarudi. Wakati huo huo, Abu Bakr, ‘Umar, ‘Uthmaan, Mu’aawiyah, Yaziyd, Ibn Dhi’l-Juushan na watu wote waliowadhuru Ahlul-Bayt – kwa mujibu wa madai yao – pia watarejea.
Watu wote hawa watarudi – kwa mujibu wa imani zao – watarudi tena duniani kabla ya Siku ya Hisabu, ambapo Mahdi atatokeza, kama alivyowaambia Ibn Saba’ - adui wa Allaah(Subhaanahu wa Ta'aalaa) ; watarudi ili waje kuadhibiwa kwa sababu ya kuwadhuru Ahul-Bayt na kuwakatalia utawala na kuzikandamiza haki zao, hivyo wataadhibiwa vilivyo, baadaye watakufa, kisha watafufuliwa tena Siku ya Hisabu kwa malipo ya mwisho, hili ndilo wanaloamini.
Halikadhalika, kuna imani mbaya ambazo mtu anaweza kupata maelezo zaidi ndani ya vitabu vifuatavyo, vinavyoeleza ni kwa namna gani walivyo waongo:
Al-Khutwuutw al-‘Ariydhwah cha Muhibbud-Diyn al-Khatwiyb (kinapatikana kwa Kiingereza, kimetafsiriwa na Abuu Bilaal Mustwafa al-Kanadiy).
Uswuulul-Madh-hab ash-Shi’ah al-Imaamiyyah cha Dkt. Naaswir al-Qaafari.
Firaaq Mu’aaswirah Tantaswib ilaal-Islaam cha Dkt. Ghaalib bin ‘Aliy ‘Awaaji (1/127-269).
Al-Mawsuu’ah al-Muyassarah fil-Adyaan wal-Madhaahib wal-Ahzaab al-Mu’aasirah (1/51/57).
‘Ulamaa wa Al-Lajdan Ad-Daaimah waliulizwa:
Je, Maimamu wa Kishia ni sehemu ya njia ya Uislamu? Nani aliyeitengeneza? Kwa sababu, wao, yaani Mashi’ah, wanajinasibisha dhehebu lao kwa ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhu).
Jibu: Madhehebu ya Kiimamu ya Kishia ni dhehebu lililozushwa ambalo limeanzishwa [limenasibishwa] ndani ya Uislamu. Tunakushauri kusoma kitabu cha al-Khutwuutw aa-‘Ariydhwah na Mukhtasar at-Tuhfah al-Ithna ‘Ashariyyah na Minhaaj as-Sunnah vya Shaykh al-Islaam (Ibn Taymiyah), ambavyo vinaeleza mengi kuhusiana na uzushi wao.
[Fataawa al-Lajnah ad-Daa’imah (2/377) Abdul-‘Aziyz bin ‘Abdilllaah bin Baaz, ‘Abdur-Razzaaq ‘Afiyfiy, ‘Abdullaah bin Ghadyaan. Mwisho wa nukuu].
Pili:
Baada ya maelezo hayo juu, inaonesha wazi kwamba dhehebu hili ni la uongo na kwamba linakwenda kinyume na imani za Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah, na kwamba imani zake haziwezi kukubalika na yeyote, iwapo ni kwa wanachuoni wao ama tamaduni zao. Ama kwa Maimamu ambao wanadai kuwanasibisha, walio safi na wapo mbali na uongo na uzushi huu, ni:
1. ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyekufa shahiyd mwaka 40 AH.
2. Al-Hasan bin ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) (3-50 AH).
3. Al-Husayn bin ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) (4-61 AH).
4. ‘Aliy Zayn al-‘Aabidiyn bin al-Husayn (38-95 AH), ambaye wanamwita as-Sajjaad.
5. Muhammad bin ‘Aliy Zayn al-‘Aabidiyn (57-114 AH) ambaye wanamwita al-Baaqir.
6. Ja’afar bin Muhammad al-Baaqir (83-148 AH) ambaye wanamwita asw-Swaadiq.
7. Muusa bin Ja’afar asw-Swaadiq (128-148 AH) ambaye wanamwita al-Kaadhwim.
8. ‘Aliy bin Muusa al-Kaadhwim (148-203 AH) ambaye wanamwita ar-Ridhwa’ (Riiza).
9. Muhammad al-Jawaad bin ‘Aliy ar-Rida’ (195-220 AH) ambaye wanamwita at-Taqiy.
10. ‘Aliy al-Haadi bin Muhammad al-Jawaad (212-254 AH) ambaye wanamwita an-Naqiy.
11. Al-Hasan al-‘Askariy bin ‘Aliy al-Haadi (232-260) ambaye wanamwita az-Zakiy.
12. Muhammad al-Mahdi bin al-Hasan al-‘Askari, ambaye wanamwita al-Hujjah al-Qaa’im al-Muntadhwar. Wanadai kwamba ameingia kwenye tundu (pango) huko Samarra’, lakini watafiti walio wengi wana maoni kwamba wala hakupata kuwepo hata kidogo, na kwamba ni tungo za uongo za Kishia.
Angalia: Al-Mawsuu’ah al-Muyassarah (1/51).
Ibn Kathiyr amesema kwenye al-Bidaayah wan-Nihaayah (1/177):
“Ama kwa yale wanayoyaamini kuhusu tundu la Samarra’, hii ni Hadiyth ya kutungwa ambayo kwa ukweli haina thibati na ushahidi au mashiko madhubuti.” Mwisho wa nukuu.
Ibn Taymiyah (Rahimahu Allaah) amewagawa Maimamu Kumi na Mbili wa Kishia katika makundi manne:
1 – ‘Aliy bin Abii Twaalib, al-Hasan na al-Husayn (Radhwiya Allaahu ‘anhum). Hawa ni Swahaba watukufu na wala hakuna yeyote mwenye shaka na sifa na uongozi wao, lakini wapo wengine ambao wameshirikiana nao (walikuwa pamoja) kwenye sifa ya Uswahaabah na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na miongoni mwa hao Swahaba wapo ambao walikuwa ni wachaji Allaah zaidi kuliko wao, kwa mujibu wa ushahidi sahihi kutoka kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
2- ‘Aliy bin al-Husayn, Muhammad bin ‘Aliy al-Baaqir, Ja’afar bin Muhammad asw-Swaadiq na Muusa bin Ja’afar. Hawa ni miongoni mwa waaminifu na wanachuoni wenye kutegemewa. Minhaaj as-Sunnah (2/243, 244).
3- ‘Aliy bin Muusa ar-Ridhwa, Muhammad bin ‘Aliy bin Muusa al-Jawaad, ‘Aliy bin Muhammad bin ‘Aliy al-‘Askariy, na al-Hasan bin ‘Aliy bin Muhammad al-‘Askariy. Kuhusiana nao, Shaykh al-Islaam (Ibn Taymiyah) amesema: Hawakuonesha kuwa na sifa nyingi za elimu ambayo ummah unaweza kunufaika na wao, wala hawakuwa na mamlaka kwa namna ambayo itausaidia ummah. Isipokuwa walikuwa ni watu wa kawaida wa Kihaashimiy, walikuwa na hadhi ya heshima, na walikuwa na maarifa tosha kwa kile kinachohitajiwa na wao na kile kinachotegemewa na watu kama wao; ni elimu ambayo inapatikana kwa mapana na Waislamu wa kawaida. Lakini elimu mahsusi ambayo walikuwa nayo wanachuoni hawa haikuwepo kwa kundi hili. Hivyo utafutaji wa elimu haukupokewa na wao kwa yale waliyopokea kutoka kwa watatu wengine (waliotangulia). Kama wangelikuwa na kile ambacho kina manufaa kwa watafiti wa elimu, wangelinufaika nao, kwani watafutaji wa elimu wanaelewa fika ni wapi pa kuitafuta elimu.
4- Muhammad bin al-Hasan al-‘Askariy al-Muntadhwar (mwenye kusubiriwa). Hakuwepo kabla hata kidogo.
Na Allaah Anajua zaidi