Shida Wanazopata Masunni Huko Iran
Shida Wanazopata Masunni Huko Iran
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi
Yafuatayo ni mahojiano aliyoulizwa Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi alimaliza masomo yake ya sekondari nchini Iran kisha akaelekea Madinah kwa ajili ya kujiendeleza na masomo ya juu katika chuo kikuu cha Al Madinah al Munawarah katika mwaka 1979. Amechukua degree yake katika chuo kikuu cha Damascus mwaka 1984 na mara baada ya kumaliza masomo hayo akaelekea Beirut – Lebanon kwa ajili ya kuchukua shahada ya Masters katika chuo kikuu cha Awzaiy, kisha akajiandikisha katika chuo kikuu hicho hicho kwa ajili ya shahada ya PHD katika mwaka 1995 na thesis aloandika ilikuwa juu ya “Kuzigeuza fikra za kiislamu katika nchi ya Iran kutoka madhehebu ya Sunni na kuzielekeza katika madhehebu Kishia katika utawala wa Safawi (Mashia).
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi hivi sasa ni kiongozi wa Ahlus-Sunnah wa Iran na Ofisi yake ipo mjini London.
Suali:
Unaweza kutuelezea juu ya historia ya watu wanaofuata madhehebu ya Sunni huko Iran?
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi:
Ni uhakika unaojulikana na kila mtu kuwa nchi ya Iran ilikuwa ikifuata madhehebu ya ki Sunni mpaka katika karne ya kumi al Hijri. Katika wakati huo Iran iliweza kutoa wanavyuoni wengi sana katika nyanja mbali mbali za elimu, na ushahidi ulio dhahiri kabisa ni vile vitabu muhimu sana vinavyoaminika katika Uislamu kama vile Bukhari, Muslim, Abdu Dawood nk. Vitabu hivyo vimeandikwa na wanavyuoni kutoka nchi ya Iran au wale waliochukuwa masomo yao katika nchi ya Iran. Hata hivyo mara baada ya Mashia kuchukua hatamu huko Iran na hii ilikuwa baada ya kuwauwa wanavyuoni na wanasheria wengi wa ki Sunni na kuwalazimisha wengine kufuata madhehebu yao na wengine wakalazimika kukimbilia milimani na kuifanya nchi ya Iran kuwa ni makao makuu ya kufanya njama mbali mbali dhidi ya Uislamu na Waislam.
Ferdinand ambaye ni balozi wa mfalme wa Austria aliwahi kusema:
“Ingelikuwa si Mashia wa Iran tungelikuwa sote tunaisoma Qurani kama watu wa Algeria”, akimaanisha kuwa ingekuwa si kwa msaada wa Irani nchi yake ingeliweza kutekwa na utawala wa kislamu wa Ottoman, lakini utawala wa ki Shia ulishirikiana na wakristo katika kufanya njama iliyowawezesha kuuzuwia Uislamu usiweze kusonga mbele na kuzifikia nchi za Ufaransa na Vienna.
Suali:
Vipi zilikuwa hali za Masunni kabla ya mapinduzi, na je wao walishiriki katika kuyafanikisha, na nini yalikuwa malipo yao baada ya kushiriki katika kuleta mapinduzi hayo?
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi:
“Watu wanaofuata madhehebu ya ki Sunni wengi wao wanatokana na asili zisizokuwa za ki Irani na kwa ajili hiyo hata wakati wa utawala wa Shah wao walikuwa wakitendewa kama kwamba ni wananchi wa daraja la pili hasa kwa vile wengi wao wanaishi vijijini na pia kutokana na uhakika juu ya hitilafu iliyopo katika itikadi yao ambayo ni tofauti na ile ya ma Shia. Baadhi ya wanavyuoni wa Ahli Sunnah kama vile Shaykh Ahmad ambaye ni mufti wa Zadah na wengineo walikuwa wakiupinga utawala wa Shah na wakawa wanamuunga mkono Khomeni (Mwenyezi Mungu Awasamehe). Shaykh Ahmed alikhitilafiana na Khomeni mara baada ya mapinduzi, akakamatwa na kutiwa jela miaka kumi ingawaje alihukumiwa na mahakama kifungo cha miaka mitano tu, na hakuachiliwa ila baada ya wakubwa wa serikali kutambuwa kuwa hali yake inazidi kuzorota na kwamba anakaribia kufa.
Serikali ilianza kazi ya kuwakamata wote wale waliojaribu kudai haki zao na kuwaadhibu au kuwatia jela au kuwauwa au kuwadhalilisha kama ilivyokuwa katika kesi ya Shahiyd Bahman Shakoury. Ma Shaykh wengi wa ki Sunni walitiwa jela na wengine ikawabidi kuihama nchi, na wengine wakaadhibishwa na kudhalilishwa kama vile mjumbe wa baraza la uwakilishi wa mkoa wa Baluchistan Mawlawi Nathar Mohammad na Shaykh Mawlawi Muhyiddin na Shaykh Dost Mohammed Sirawani aliyetiwa jela kisha akahamishwa na kupelekwa mji wa Najaf Abad. Yupo pia Shaykh Ibrahim Dammini ambaye bado anaendelea kuteswa akiwa yumo jela mwa muda wa miaka zaidi ya mitano sasa.
Chini ya utawala huu wa kimadhehebu, watu wa Ahli Sunnah walitunukiwa zawadi ya kudhalilishwa na vitisho, na hali yao kama ninavyoielewa mimi ni mbaya zaidi kuliko ile ya wa wa Palastina.
Upo mji wowote duniani isipokuwa Teheran mji mkuu wa ma Shia ambao ndani yake hauna hata msikiti mmoja wa ma Sunni? Mji huu una makanisa yapatayo arubaini kwa ajili ya wa Kristo, yapo pia makaburi ya wa Bahai. Hata makafiri walio wachache sana wana mahekalu yao na sehemu zao za kufanyia ibada na wana uhuru wao wa kuabudu, isipokuwa ma Sunni, wao hawaruhusiwi kujenga misikiti yao wala makaburi yao.
Hata hivo utawala huu wenye sura mbili chini ya kisingizio cha kuisimamisha bendera ya umoja wa Kiislamu umefanikiwa kuweza kuwadanganya Wasilamu wengi walio nje ya Iran kwa kuwaalika kuhudhuria mikutano na wakaweza kuwabadilisha fikra zao katika muda mchache sana wakawa mashahidi wa uongo dhidi ya watu wao wenyewe huku wakiwadanganya kutokana na yale waliyofundishwa juu ya utukufu wa umoja wa Uislamu wakiwa hawaelewi lolote katika yale maovu wanayofanyiwa watu wa Ahlus Sunnah wanaoishi ndani ya Irani. Utawasikia wakirudia rudia kwa urahisi kabisa kauli isemayo. “Sisi ni ndugu na hapana tofauti baina yetu.
Suali:
Unaweza kuelezea juu ya hali ya Ahlus Sunnah hivi sasa huko Iran?
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi:
“Ahlus Sunnah wananyimwa haki zao za asili katika mahitajio yao ya vijijini, ya kijamii na haki za kibinadamu, hii ukiweka upande kuwa wananyimwa haki yao ya kushiriki katika mambo ya kisiasa kama Mashia wanavyoruhusiwa. Ujengaji wa skuli za Kisunni unahesabiwa kuwa ni uhalifu usiosameheka. Masunni wengi wanaounga mkono ujenzi kama huo wanakamatwa na kutiwa jela hata kama walifanya hivyo tokea zamani. Wengine wanauliwa na wengine wananyolewa ndevu zao, eti kwa sababu walitoa mchango katika ujenzi wa msikiti au kwa ajili ya jambo lolote linalowahusu watu wa Ahlus Sunnah.
Wapo pia wengi wanaotiwa jela kwa muda mchache na wengi wameuliwa kwa sababu wametiliwa shaka tu. Wengi miongoni mwa wanavyuoni maarufu wametekwa nyara, na wengine wametiliwa sumu au kuuliwa.
Yafuatayo ni majina ya baadhi tu misikiti na skuli za Ahlus Sunnah zilizobomolewa;
- Msikiti wa Al Sunnah wa Ahwaz uliogeuzwa kuwa kituo cha Polisi
- Msikiti mwingine uliopo Ahwaz katika mji wa Khurasan
- Msikiti na skuli katika mji wa Lakour
- Msikiti wa Al Sunnah uliopo Shiraz
- Msikiti wa Shaykh Faydh – serikali iliubomoa msikiti huo katika mwaka 1993 kutokana na amri iliyotolewa na Khameni mwenyewe ambaye hivi sasa yeye ni kiongozi wa kiroho huko Iran.
- Msikiti wa Ahlus Sunnah katika mji wa Talish
- Msikiti wa Aaban uliopo mji wa Mashhad. Umebomolewa kisha ardhi yake ikataifishwa na kuta zake zikabomolewa na wanaousimamia wakafukuzwa nchini.
Suali:
Tueleza juu ya uhakika wa uwakilishi wa Ahlus Sunnah katika madaraka mbali mbali serikalini huko Iran kama vile ndani ya bunge pamoja na wizara nk.
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi:
Ahlus Sunnah ambao idadi yao ni theluthi moja ya watu wa Iran (one third) kusema kweli haina muwakilishi yeyote. Hapana hata Sunni mmoja aliyeshika madaraka ya ukurugenzi katika idara yoyote ile ya serikali wala katika wizara wala ubalozi wala hata madaraka ya mikoani. Hapana aliyepewa hata cheo kidogo kabisa serikalini huko Iran. Jambo hili ni aibu kubwa kabisa, kwani wakati sisi tunaishi katika karne ya ishirini tunashuhudia theluthi nzima ya wananchi wakinyimwa haki zao zilizo duni kabisa. Ipo nchi yoyote duniani inayowanyima watu wake haki ya kuchagua majina wanayoyataka, majina kama vile Omar, Aisha, Hafsah, abubakar, Zubeir na mengi kati ya majina ya Masahaba kumi waliobashiriwa Pepo (na Mtume (Swalla Llaahu 'alayhi wa sallam)?
Suali:
Una ujumbe wowote unaotaka kuwapelekea Waislamu wanaofuata madhehebu ya Sunni ulimewenguni?
Shaykh ‘Abdur-Rahmaan Al-Baluchi:
Nina neno la mwisho ninalotaka kuwaambia wale tunaoshirikiana katika itikadi, wale ambao hutembelea Iran mara kwa mara, napenda kuwaambia kuwa ziara zao hizo ni dalili dhidi yetu, zinatudhuru na kusababisha kuuwawa kwa wengi miongoni mwa wanachama wenzetu. Watu hao wanakuwa mfano wa vikaragosi mikononi mwa serikali, na hii ni kwa sababu serikali inatuambia;
“Hawa ni maimamu wenu na wanavyuoni wenu na ma Shaykh wenu wanasali nyuma yetu, wanalitembelea kaburi la Imaam na wala hawaombi kujengewa msikiti wao peke yao mjini Teheran, wanasema sisi tusali pamoja ndani ya msikiti mmoja, sasa kwa nini mnakhitalifiana na wanavyuoni wenu? Bila shaka nyinyi ni mawahabi”.