'Aaishah Bint Abi Bakr (رضي الله عنها)
Al-Mubaraatu min fawqi sab’ah As-Samaawaat
(Aliyetakaswa Kutoka Mbingu Ya Saba)
Haliymah ‘Abdullaah Husayn
Naye ni Mama wa Waumini ‘Aaishah Swiddiyqah bint Swiddiyq (mkweli mtoto wa mkweli) Khaliyfah wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) Abu Bakr As-Swidiyq bin Abiy Quhaafah ‘Uthmaan bin ‘Aamir Al-Qurayshiya At-Taymiyah Al-Makiyah Ummu Al-Muuminiyn mke wa Bwana wa watoto wa Aadam na mke wake mpenzi, mtoto wa baba ampendaye aliyetakaswa kutoka juu ya mbingu saba. Mwalimu wa Wanaume.
Alikuwa na elimu kuliko wanaume jambo linaloonesha toka karne kumi na nne kwamba mwanamke anaweza kuwa na elimu zaidi ya wanaume, kuwa mwanasiasa na mpiganaji.
Bibi huyu alitoka Madrasah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Madrasah ya Imaan na Ushujaa. Alilelewa udogoni na Baba yake kisha kuwa mke wa Mtume wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) akakusanya elimu ubainifu adabu zinazosomeshwa hadi leo katika vyuo vya elimu.
Kuolewa kwake na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ilikuwa kwa Amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kufa Mama wa Waumini Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha).
Wamepokea Al-Bukhaariy na Muslim katika Swahiyh zao kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) amesema, amesema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Nilikuona katika ndoto siku tatu, aliniijia nawe malaika katika kipande cha kitambaa cha hariri anasema: “huyu mke wako”, nafunua uso wako nakukuta ni wewe…”
Lakini alimuoa Sawdah na baada ya miaka mitatu akamuoa (dukhuul) Mama wa Waumini ‘Aaishah mwezi wa Shawwaal baada ya vita vya Badr katika nyumba miongoni mwa nyumba zilizozunguka Msikiti zilizojengwa kwa udongo na kuezekwa na minazi, godoro la ngozi lililojazwa majani. Katika nyumba hii yah al ya chini (baswiyt, mutawaadhwi’u) alianza Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) maisha mapya ya ndoa huku akiwa kiliwaza mwenye kumuingizia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) furaha katika moyo wake na kumuondoshea yanayomkwaza katika maisha na Da’awah.
Alikuwa mke mwema mkarimu alisubiri pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika ufakiri na njaa mpaka ikawa yanapita masiku na moto hauwashwi ndani ya nyumba yao; wakiishi kwa tende na maji.
Waislamu walipopata faraja kuna siku aliletewa Dirham laki moja huku akiwa amefunga aliigawa yote hali nyumbani kwake hakuna kitu.
Akamwambia kijakazi wake:
“Hukuweza kujinunulia dirhamu moja nyama ukafuturia” akasema: “lau ungenikumbusha ningefanya” Mustadrak Al-Haakim
Alikuwa mke bora aliyetukuka nafsi yake asiyejali maisha ya ulimwengu, na ufakiri haukuwa kikwazo kwake bali alifanya hima kupokea elimu kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akafikia mpaka kuwa mwalimu anawafundisha wanaume na marejeo (reference) katika Hadiyth, Sunnah, na Fiqh.
Anasema Az-Zuhriy: “Lau ingekusanywa elimu ya Mama wa Waumini ‘Aaishah na elimu ya wanawake wote ingekuwa elimu ya Mama wa Waumini ‘Aaishah zaidi”. Mustadrak Al-Haakim
Anasema Hishaam bin ‘Urwah kutoka kwa baba yake amesema:
“Nilisuhubiana na Mama wa Waumini ‘Aaishah sijaona yeyote katu mwenye kujua zaidi yake katika Aayah iliyoshuka wala Faradhi wala Sunnah wala Shairi wala Upokezi wala historia siku katika masiku ya Waarabu wala nasabu wala kadha… wala kadha… wala kwa Qadhwaa (hukumu) wala Utabibu (Udaktari), nikamwambia ewe Khalat wapi umejifunzia udaktari? Akasema, “nilikuwa nikiumwa natajiwa dawa, na akiugua mtu anatajiwa dawa nami nahifadhi, na nawasikia watu wakitajiana nami nahifadhi”. Hulyatu Aw-Liyaa
Na sehemu muhimu katika maisha ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ni tuhuma mbaya kabisa aliyotuhumiwa Hadiyth al-Ifki (Masimulizi ya uongo) ambayo yuko mbali nayo kama mbingu na ardhi. Na kutokana na tukio hili kuna wanaojinasibisha na Uislam wanaipigia debe na kutumia kila njia kutaka kuthibitisha ni kweli alifanya machafu (Tunataka kinga kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na dhana hii mbaya) na kumtia dosari Mama wa Waumini hali Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Mwenye Amemtakasa na kushusha Aayah za kuonyesha utakaso wake.
Hadiyth al-Ifki ni mazungumzo yaliyozushwa na kuenezwa na wanafiki kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Mkubwa wa wanafiki alikuwa ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul kiongozi wa Khazraj Madiynah alikuwa mashuhuri baina ya watu wake na wagomvi wake kwa uongo, unafiki na chuki yake kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Da’awah.
Hivyo alikuwa anakaa na maadui wa Waislam na kuwachonganisha na kuwahimiza wamuue Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na haya yote ni kutokana na kupoteza taji na ufalme baada ya kudhihiri Uislam (Allaahu A’alam) hivyo si ajabu akawa na lengo la kuuchafua Uislam kutokana na Hadiyth al-Ifki na hadi leo wanaouchafua Uislam na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) haswa Mustashriqiyna (waliousoma Uislam katika nchi za Kiarabu kwa lengo la kuubomoa tangu vita vya msalaba mpaka sasa) wanatumia njia hizi hizi za kutia dosari Utume wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumtuhumu mkewe kwa uzinifu mwanamke safi asiye na dhambi wala doa.
Ilianza Hadiyth al-Ifki baada ya kurejea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika vita vya Bani al-Mustwaliq, ilibidi kubadilika wakati wa kurejea kwa jeshi kutokana na Fitnah iliyoenea baina ya Waislam na wafuasi wa ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul kiongozi wa wanafiki na Khazraj, waligombania watu wawili maji kama inavyotokea katika kila kisima au sehemu ya maji yenye watu wengi… aliita mmoja “Enyi Khazraj” akaita wa pili “Enyi Kinaanah, enyi Quraysh”, akatoka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amekasirika kutokana na ubaguzi huu wa kikabila akauliza:
“Vipi (mnaleta) wito wa kijahilia? Acheni hakika huo ni uvundo”.
Akapata fursa Rais wa wanafiki na hakuachia ugomvi huo upite bali alizidi kuchochea na kuzunguka huku akisema: “WaLlaahi hatukuona Quraysh na maguo yao (joho) ila kama ilivyosemwa (mnenepeshe mbwa wako aje akung’ate), Ama WaLlaahi tukirejea Madiynah wenye nguvu (anakusudia yeye na wenyeji) watawatoa wanyonge (Waislamu waliotoka Makkah)”.
Kisha akawaelekea watu wake anawachochea na kuwaambia: “Hivyo ndivyo mlivyofanya kwa nafsi zenu… mmewahalalishia mji wenu, mkagawana nao mali zenu… kisha hamkuridhika kwa mliyoyafanya bali mlihatarisha nafsi zenu kwa kushirikina naye (anamkusudia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ) kupigana katika vita…
Ikaenea habari akatoa idhini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ya kuondoka na haikuwa kawaida yake kuondoka katika wakati wa joto mchana.
Akauliza Usayd bin Hudhayr (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Ewe Mtume wa Allaah umeondoka mapema katika muda usio wa kawaida yako? Akasema Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam):
“Je haijakufikia aliyosema jamaa yenu!! Anaashiria maneno ya Ibn Saluul”.
Kisha likaondoka jeshi na akawa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) anamharakisha mnyama wake, ikapita siku na usiku mpaka siku ya pili na jua linawaka wakashuka watu hawakukaa ila walijikuta wamelala.
Walipoanza kuelekea Madiynah ilikaribia usiku msafara ukapumzika akatoka Mama wa Waumini ‘Aaishah kwa ajili ya kujisaidia (Ilikuwa kawaida ya Mtume wa Allaah kupiga kura kwa wakeze wa kumfuata katika vita, na safari hii ilimuangukia kura Mama wa Waumini ‘Aaishah) wakati anarejea ukakatika mkufu wake a kudondoka, akachelewa katika kuutafuta aliporudi katika kipando chake (Haudaj yaani juu ya mnyama anayejengewa ju ya mgongo wake kama nyumba na inafunikwa kwa ajili ya kuwasitiri wanawake) akakuta wameondoka hali wakidhani yumo ndani ya kipando. Akakaa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) sehemu yake akidhani watamrejea watakapohisi hayupo katika Haudaj yake.
Alikuwa Safwaan bin Al-Mu’atwal (Radhiya Allaahu ‘anhu) kawaida yake anabaki nyuma ya jeshi ili kuangalia kama kuna kilichosahauliwa au kudondoka, aliponyanyuka kuanza kufuata nyuma ya jeshi aliona kitu cheusi kwa umbali akajua ni Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) Kwani alikuwa akimjua kabla ya Hijaab, akawa anasema: Inna Lilaahi wainaa Ilayhi Raaji’uun (sisi ni wa Allaah na Kwake tutarejea na neno hili husemwa wakati wa tatizo)… akawa anakariri maneno hayo ili amtanabahishe na hakutamka neno bali alimuweka chini mnyama wake akashika kamba ya ngamia, akapanda Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kisha Safwaan akaanza msafara mpaka akalikuta jeshi, Akapata matumaini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa kumpata akiwa salama (hakupata tatizo lolote) na akamsikiliza kisa cha kuachwa kwake wala hakumpinga kwa neno.
Lakini Ibn Saluul adui wa Allaah akakataa ipite ila aitie kasoro akawa amepata fursa akasema: “WaLlaahi hakusalimika kila mmoja kwa mwenzie”,
Anataka kumgonganisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na mtu wake wa karibu zaidi Abu Bakr au awatilie shaka waumini katika heshima ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Anasema Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Alikuwa aliyetawalia uzushi ‘Abdullaah bin Ubay bin Saluul”, Tulirudi Madiynah nikawa mgonjwa muda wa mwezi na watu wamezama katika mazungumzo ya uzushi nami sijui na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawa anaingia kwangu na kunisalimu kisha anatoka wala sioni upole aliokuwa nao mwanzo nikiugua likanitia wasiwasi wala sikuhisi shari mpaka nikatoka na Ummu Mistwah na tulikuwa hatutoki ila usiku kabla hatujaweka choo karibu na nyumba yetu.
Tulipomaliza haja yetu tunarudi akajikwaa Ummu Mistwah akasema: “Aangamie Mistwah. Nikamwambia: “ubaya ulioje wa uliyoyasema, unamtukana mtu aliyeshuhudia Badr?... akasema: hivi hujasikia aliyosema? Nikasema: Kwani amesema nini? Akanipa habari ya maneno ya wazushi, yakazidi maradhi yangu juu ya maradhi.”
Niliporudi nyumbani aliingia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasalimia na kuuliza hali, nikamjibu niruhusu niende kwa wazazi wangu nami nakusudia kuhakikisha habari kwao, akanipa idhini Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) nikawajia wazazi wangu nikamwambia mama yangu: “Ewe mama yangu nini watu wanaongelea? Akajibu, ewe binti yangu tuliza nafsi yako, WaLlaahi ni mara chache mwanamke anayependeza zaidi kwa mumewe naye anampenda huku ana wake wenzie ila watamzidishia, nikasema SubhanaAllaah!! Wamezungumza watu hili? Nikalia huo usiku mpaka ikawa siwezi kulala, nikalia masiku mawili na siku mpaka wakahofia wazazi wangu kilio changu kitaniumiza…
Walipokuwa wamekaa nami wazazi wangu, nami nalia akaingia mwanamke katika Answaar akakaa na kuanza kulia nasi tulipokuwa katika hali hii akaingia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akasalimia kisha akakaa sehemu unayomuona, kisha akasema: “Ama baad ewe ‘Aaishah hakika imenifikia kuhusu wewe kadha na kadha, ikiwa umetakasika Atakutakasa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na ikiwa umefanya dhambi mtake msamaha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) na utubie kwake, Kwani mja akikiri kosa lake akatubia Atamsamehe Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala)… Alipomaliza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mazungumzo yake ilikauka machozi yangu mpaka sihisi hata tone, nikamwambia baba yangu: “Nijibie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika aliyosema”, akasema WaLlaahi sijui la kumwambia, nikamwambia mama yangu: “Nijibie Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kwa aliyosema”, akajibu WaLlaahi sijui la kumwambia.
Nikasema hakika mimi WaLlaahi nimejua kwamba mmesikia wanayonizungumzia watu mpaka ikatulia katika nafsi zenu mkayasadiki hata nikiwaambia mimi nimetakasika na hayo hamtonisadiki kwa hilo, na ikiwa nitakiri hilo jambo (Na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anajua nimetakasika) mtalisadiki, WaLlaahi sipati kwangu wala kwenu mfano ila wa Baba yake Nabii Yuusuf pindi aliposema:
“…Lakini subira ni njema; na Allaah Ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyaeleza.” Yuusuf: 18
Kisha nikageuka nikajilaza katika godoro langu na mimi WaLlaahi najua nimetakasika na Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) atanitakasa ila sikujua kama Atashusha Wahy utakaokuwa unasomwa nilijidharau nafsi yangu kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ataongelea jambo langu lakini nilitarajia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ataona ndoto usingizini ya kuonyesha utakasifu wangu.
WaLlaahi hakunyanyuka Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) sehemu aliyokaa wala hakutoka yeyote ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Alishusha kwa Nabii wake Wahy akafurahi Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawa anacheka ikawa neno lake la mwanzo alilotamka kwangu: “Bishara njema Mama wa Waumini ‘Aaishah, ama WaLLaahi Amekutakasa”. Akaniambia mama yangu: msimamie Mtume wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala), nikasema WaLlaahi simsimamii na wala simshukuru ila Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Naye ndiye Aliyeshusha utakasifu wangu, Akashusha Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Aayah kumi katika Surat An-Nuur:
“Hakika wale walioleta uongo ni kundi miongoni mwenu. Msifikiri ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mtu katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao, atapata adhabu kubwa.
“Kwa nini mliposikia khabari hii, wanaume Waumini na wanawake Waumini hawakuwadhania wenzao mema, na kusema: Huu ni uzushi dhaahiri?
“Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na ilivyokuwa hawakuleta mashahidi wane basi hao mbele ya Allaah ni waongo.
“Na lau kuwa si fadhila ya Allaah juu yenu na Rahmah Yake katika dunia na Aakhirah, bila ya shaka ingelikupateni adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.
“Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mlifikiri ni jambo dogo, kumbe mbele ya Allaah ni kubwa.
“Na kwa nini mlipoyasikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya. Subhaanak Umetakasika! Huu ni uzushi mkubwa!
“Allaah Anakuonyeni msirejee tena kufanya kama haya kabisa, ikiwa nyinyi ni Waumini!
“Na Allaah Anakubainisheni Aayah. Na Allaah ni Mjuzi Mwenye hikima.
“Kwa hakika wale wanao penda uenee uchafu kwa walio amini, watapata adhabu kali katika dunia na Aakhirah. Na Allaah anajua na nyinyi hamjui.” An-Nuur: 11-19
Aliudhika Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Hadiyth al-Ifki ikampitia muda mrefu katika tabu hajui afanye nini akashauriana na Maswahaba zake katika jambo hili akasema ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Nani amekuozesha ewe Mtume wa Allaah, akajibu: Allaah! Akasema: unadhani Allaah Amekupa kitu kibaya, Ametakasika Allaah huu ni uzushi mkubwa”.
Akawaita Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ‘Aliy na Usaamah bin Zayd awashauri kutengana na mke wake.
Akasema Usaamah bin Zayd (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Mke wako Mtume wa Allaah na hatujui ila kheri”.
Akasema ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu): “Ewe Mtume wa Allaah, Allaah hakukudhikishia na wanawake wengineo ni wengi na ukimuuliza kijakazi yaani Bariyrah (kuhusu tabia zake) atakusadikisha.”
Akamuita na kumuuliza: Bariyrah je umemuona na kitu kinachokutia shaka? Akasema Bariyrah: “Hapana naapa kwa Aliyekutuma kwa haki sijaona kwake baya ila ni msichana mdogo analala akiwa anatazama mkate uumuke anakuja kuku kuula.”
Kisha akamuuliza kuhusu jambo la Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) lililozuliwa akasema: “Ewe Mtume wa Allaah najilinda kuona kwangu na kusikia, WaLlaahi sikujua kwake ila kheri na siongei kwa vile mimi ni Muhaajirah (aliyehama kutoka Makkah kuja Madiynah), lakini sikuwa ni mwenye kusema ila haki”.
Huu ni ufupisho wa Hadiyth al- Ifki kwa maelezo zaidi tazama kwa Imamu Al-Bukhaariy Tafsiri ya Surat An-Nuur mlango (لولا اذ سمعتموهم ظن المؤمنون والمؤمنات بأنفسهم خيرا ) na Kwa Muslim katika Tawbah 2770, Siyrah Ibn Hishaam 3/210 na Taariykh Atw-Twaabariy 3/68
Ni juu yako Ndugu Muislam ujue kiwango cha uzushi huu na utajua uhakika kwa namna ilivyokuzwa kutokana na ugomvi wa kidini, kisiasa, uongo na unafiki.
Nawe dada katika Iymaan ni juu yako ujue njia ya peponi imejaa tabu na hapana budi kupata mitihani na maudhi katika mali na nafsi inachotakiwa ni subra na azma huu ni mwendo (Sunnah) ya Allaah kwa watu wenye Iymaan.
Tukirudi kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipougua Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) baada ya kurejea katika Hijatu al-Wada’i na akahisi wakati wa kuondoka umefika alikuwa anasema hali akiwazuru wakeze: niko wapi kesho? Nipo wapi baada ya kesho? Anafanya taratibu ili afikie siku ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), Wakamtaka wakeze wote augulie anapopenda wakajitolea siku zao kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha). Akafariki kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).
Anaelezea Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha): “Alifariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika nyumba yangu katika siku yangu akiwa baina ya mapaja yangu na kifua, aliingia ‘Abdullaah bin Abi Bakr naye ana mswaki laini akawa anautazama mpaka nikadhani anautaka, nikauchukua nikaulainisha kwa kutafuna kisha nikampa akapiga mswaki vizuri kisha akanirudishia, nikawa namuombea du’aa alizokuwa anamuombea Jibriyl na alizokuwa akijiombea alipokuwa mgonjwa na hakuacha kujiombea katika maradhi hii, ikarejea macho yake mbinguni na kusema: Rafiki aliye juu (Rafiyq al-‘aala) na ikatoka nafsi yake, Namshukuru Allaah Aliyejaalia mate yangu kuchanganyikana na yake siku yake ya mwisho duniani”. Musnad Ahmad 6/48, Al-Haakim Ma’arifatu Swahabah 4/7.
Alizikwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika nyumba ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alipotolewa roho yake, na aliishi Mama wa Waumini ‘Aaishah (Rasdiya Allaahu ‘anha) baada yake akifundisha wanawake na wanaume na akashiriki katika kuwekwa Historia ya Uislam mpaka alipofikiwa na mauti siku ya Jumanne tarehe kumi na saba Ramadhaan mwaka hamsini na saba akiwa na umri wa miaka sitini na sita. Al-Isti’aab 4/1885, Taariykh Atw-Twabariy Hawadiyth Sanat 58 Hijriy.