Anapata Dhambi Akimkatalia Mumewe Kitendo Cha Ndoa Kwa Ajili Ya Machofu Ya Kazi?

SWALI:

 

Asalam alaikum warahma tullah wabarakat

 

Ama baad, Mimi ni mfanyakazi nimeajiriwa natoka kazini nimechoka sana na mume wangu anataka jimai kila siku mimi nakataa kwa kuwa nahitaji huruma yake ikiwa mimi ndio natoa mchango mkubwa katika familia je napata dhambi au niko sawa maana nimesikia mungu hakalifishi nafsi ya mtu inakuwaje binadam anikalifishe hili ni tatizo kwangu


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Asli katika kustarehe na kuingiliana baina ya mume na mke ni kuwa hakuna siku maalumu au mara maalum, bali kila ikiwepo hamu ndio vizuri tendo la ndoa kupatikana, na kama mmoja hayuko na hamu  kwa sababu yoyote ile basi huwa hakuna raha katika tendo hilo. Hata hivyo wako Maulamaa waliosema kuwa ni wajibu wa mume kumuingilia -kima cha chni - japo mara moja mkewe katika kila miezi minne ikiwa hana udhuru wowote ule, vyenginevyo atakuwa amekwenda kinyume na mafundisho ya dini.

 

Hata hivyo hilo tendo la ndoa ni haki ya kila mmoja wenu kwa mwenziwe na ikiwa mumeo ni mtu ambae anahitaji jimaa kila siku basi lililobora na ndio mafundisho ya Uislamu kumtafutia mke mwengine ili asije kuingia katika uchafu kama wewe huwezi kukidhi haja yake kwa sababu moja au nyingine. Vinginevyo unaweza ukawa miongoni mwa wenye kulaaniwa na Malaika kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

“Atapomwita mume mkewe kuelekea kwenye kitanda chake -kwa tendo la ndoa- basi mke akikataa kuitikia wito huo na mume akalala hali ya kuwa ameghadhibika -hakuridhia- basi mwanamke huyo huwa analaaniwa na Malaika mpaka kupambazuke” Imepokelewa na Muslim, kitabu cha ndoa, mlango uharamu wa kujizuilia mke na firaashi ya mumewe.

 

Hivyo basi ni wajibu wa mke kumkubalia mumewe anapomwita kitandani kwa ajili ya tendo la ndoa, isipokuwa akiwa mgonjwa ama hali yako wewe ya kuchoka kwa sababu ya kuchapa kazi bila ya kujifikiria majukumu yako mengine. Kufanya kazi ni jambo zuri lakini jifikirie pia kuwa na wakati wa kupumzika; kwani ikiwa hiyo ndio sababu ya kutoweza kuitikia wito wa mume basi yawezekana ikawa kila siku wewe ni mja wa kuchoka kwa kufanya kazi, na fahamu kuwa si wajibu kwako kutoa mchango wowote ule katika familia hilo ni jukumu la huyo mume; na huenda ikawa sababu moja ya kuwa mumeo anataka kila siku ni kuwa yeye hana la kufanya ila hilo na kama akifanya kazi basi huenda akapunguza siku ya kutaka tendo la ndoa badala ya siku zote.

 

Pia mshauri mumeo awe anafunga Swawm za Sunnah ili apunguze matamanio yake, na mpunguzie vyakula vyenye kuongeza nguvu mwilini na mpendekezee kujitafutia cha kufanya kama kuogelea, kukimbia, au mazoezi mengineyo ili achoke na kasi yake ipungue.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share