Zingatio: Mwanamme Ndio Kiongozi Wa Mwanamke

 

Zingatio: Mwanamme Ndio Kiongozi Wa Mwanamke

 

Naaswir Haamid

 

  

Alhidaaya.com

 

 

Haikuwa ni bure kuwapatia uongozi wanaume juu ya wanawake ndani ya Uislamu. Huu ni uongozi wa kimaumbile ambao unakubalika ndani ya makabila na mataifa mengi duniani; kwamba mwanamme ndio mkuu wa shughuli za mwanamke.

 

Allaah Anasema ndani ya Qur-aan Tukufu (tafsiri):

 

الرِّجَالُ قَوَّامُونَ عَلَى النِّسَاءِ بِمَا فَضَّلَ اللَّـهُ بَعْضَهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ وَبِمَا أَنفَقُوا مِنْ أَمْوَالِهِمْ ۚ

Wanaume ni wasimamizi juu ya wanawake kwa kuwa Allaah Amefadhilisha baadhi yao kuliko wengine na pia kwa ambayo wanatoa katika mali zao. [An-Nisaa: 34]

 

Waislamu tofauti wamekuwa wakifanya harakati za kurudisha utamaduni wa Kiislamu. Hata hivyo, kibarua hichi kimeonekana kuwa ni kigumu mno. Tatizo kubwa linalotukabili ni wanaume wenyewe kukosa muelekeo pamoja na kuacha muongozo sahihi wa Uislamu.

 

Wanawake wamekosa hayaa hadi kutembea utupu. Heshima baina ya mume na mke zimeporomoka, halikadhalika baina ya baba na binti. Haya yote yanasababishwa na mwanamme mwenyewe. Yareti kama mwanamme atakuwa na msimamo mbele ya mwanamke, hatayumbishwa.

 

Ni nani anayemvizia mwanamke hadi kumuingiza ndani ya mtego wa panya? Nani anayemfadhili na kumtembeza mwanamke mithili ya kinyago? Bila ya shaka yoyote, majibu ya masuala haya ni mwanamme! Kwani mwanamke anapovaa Hijaab, ni mwanamme ndiye aendae kumwambia yu mshamba. Anapovaa jeans na mini skirt, mwanamme atampigia kofi za kila namna. Sasa mwanamke anapotembea bila ya kufuata misingi ya Kiislamu nani tumlaumu? Wa kwanza ni mwanamme.

 

Hivyo sivyo kwa upande wa Uislamu, kwani mwanamme ndio anatakiwa kuwa kinara wa tabia nzuri. Hapo inakuwa ni rahisi kufuatwa tabia hizi njema kwa mwanamke: “Muumini aliyekamilika kwa imani ni yule mwenye tabia njema, na mbora wenu ni yule aliye mbora kwa wake zake kwa tabia.” [Abu Daawuud na At-Tirmidhiy].

 

Wahenga walituambia: "Mti hawendi ila kwa nyenzo." Ukweli ni kwamba, mwanamke ni mwepesi wa kuiga mambo kama alivyo mtoto. Hivyo, yahitajika muongozo sahihi na hoja nzuri za kumridhisha. Iwapo atapatiwa wigo wa Uislamu, hiyo itakuwa ni nyenzo tosha kwake. Pia tufahamu kuwa haitakikani kutumia nguvu na mabavu kumfunza mwanamke. Hekima na busara zaidi zitumike kumfahamisha. Hii ni kwa mujibu wa maneno ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyesema:

 

"Mwanamke Ameumbwa kwa ubavu, na sehemu iliyopinda ya ubavu ni juu yake, ukijaribu kuunyoosha utauvunja, na lau utauacha utaendelea kupinda, nakuusieni (kuwafanyia wema) wake zenu.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Lawama za kuporomoka maadili kwa wanawake kwanza kabisa ziwaendee wanaume wenyewe! Na ndio maana hata Siku ya Hesabu mume ataulizwa juu ya mkewe, baadae ndipo ataulizwa mke mwenyewe juu ya mumewe. La muhimu, ni mashirikiano mema baina ya mume na mke.

 

Juu ya kukosa muongozo na ulinzi tosha kutoka kwa mwanamme, bado mwanamke anatakiwa kujituliza na kujiheshimu, kwani hiyo ni amri ya Rabb Mlezi:

 

فَالصَّالِحَاتُ قَانِتَاتٌ حَافِظَاتٌ لِّلْغَيْبِ بِمَا حَفِظَ اللَّـهُ ۚ

Basi wanawake wema ni wale watiifu wenye kujihifadhi katika hali ya kutokuweko waume zao kwa kuwa Allaah Ameamrisha wajihifadhi. [An-Nisaa: 34]

Share